Operesheni ya Makonda imeibua udhaifu wa baadhi ya watendaji serikalini

Muktasari:

  • Hata hivyo, lengo la mkuu huyo wa mkoa likitazamwa kwa kina, ni jema sana licha ya kuwapo kwa kasoro ndongondogo za kiutekelezaji.

Operesheni ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ya kuwasaidia watu wanaodai kutelekezwa na wenza wao imepata umaarufu mkubwa nchini, lakini pia imefunua udhaifu mkubwa wa kiutendaji kwa baadhi ya watendaji serikalini.

Hata hivyo, lengo la mkuu huyo wa mkoa likitazamwa kwa kina, ni jema sana licha ya kuwapo kwa kasoro ndongondogo za kiutekelezaji.

Nasema hivyo kwa sababu tatizo la watu kutelekeza watoto kwa sasa hapa nchini ni kubwa na baadhi ya asasi za kiraia zimekuwa zikilipigia kelele kila kukicha.

Wapo baadhi ya watu wanaosema kuwa njia inayotumiwa imeonekana kwenda kinyume na utaratibu unaotumiwa na taasisi husika hususani Idara ya Ustawi wa Jamii iliyo chini ya Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto.

Kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya viongozi na wadau wengine kuhusu uvunjwaji wa haki za binadamu hasa kutokuwapo kwa usiri katika usikilizwaji wa malalamiko hayo, huku pia haki za watoto zikivunjwa.

Kwa mfano, Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile alilalamikia uvunjwaji wa haki za watoto huku pia akitaka njia mahsusi zifuatwe katika usikilizwaji wa malalamiko hayo.

Sasa ukiona viongozi wa Serikali moja wanakosoana hadharani, ujue tayari kuna udhaifu mkubwa wa kiutendaji. Tatizo la kwanza ninaloliona hapa ni kutokuwapo kwa mawasiliano kati ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Wizara ya Afya inayosimamia Ustawi wa Jamii, hata kama maofisa wa idara hiyo ngazi ya mkoa wameshirikishwa kwenye operesheni hiyo.

Nashawishika kuamini hivyo kwa sababu kama wangeshirikishwa, nadhani Wizara ya Afya ingeshatoa mwongozo wa jinsi ya kufanya na tusingesikia malalamiko hayo kutoka Wizara ya Afya.

Licha ya dalili za kutokuwapo kwa mawasiliano, operesheni hiyo imeonyesha jinsi mifumo na taasisi za Serikali zilivyo dhaifu au kutoaminika.

Kwa mfano, kama Idara ya Ustawi wa Jamii ipo, kwa nini bado kuna malalamiko mengi ya wanandoa kiasi kwamba wanafurika kwa mkuu wa mkoa?

Hiyo ni ishara ya kuwapo ombwe kwenye idara hiyo. Inawezekana wananchi hawaamini kama inaweza kuwasaidia kutokana na mwenendo wake.

Kama mtu anapeleka shauri lake la kutelekezwa na mumewe. Mume anaitwa na kuamriwa kulipa fedha za matumizi, hivi mtu huyo asipotekeleza maagizo hayo idara inamchukulia hatua gani?

Akipelekwa mahakamani, huko nako kesi zinachukua muda mrefu. Hii inasababisha watu kukata tamaa.

Ndiyo maana wakitokea watu kama kina Makonda, wengi wanakimbilia wakiamini kupata msaada wa haraka. Wanaamini mkuu wa mkoa atatoa amri za haraka na zitakazowapatia zao haraka.

Ndiyo maana utaona hata kwenye ziara za viongozi kama Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu, watu wengi wanataka kueleza shida zao hadharani licha ya kuwapo kwa viongozi wa ngazi kadhaa katika eneo husika.

Wengine wanabeba mabango na wengine wanadiriki hata kukimbilia mbele ya hadhara kueleza shida zao mbele yao wakiamini kwamba wanayo mamlaka ya kutoa maagizo na yakatekelezwa haraka.

Ni kweli, Rais na viongozi hao wengine wana mamlaka makubwa, lakini bado wananchi wanapaswa kufuata mfumo wa sheria na kitaasisi kutatua kero zao.

Mifumo hiyo ipo na sheria zipo, tatizo linakuja kwenye utekelezaji na hapa siwezi kuwalaumu watendaji wa Serikali kwa sababu taasisi zinazohusika zinapaswa kuwezeshwa.

Inawezekana Idara ya Ustawi wa Jamii haipati bajeti ya kutosha kuweza kusikiliza kesi za kijamii au haina rasilimali watu wa kutosha.

Ni wajibu wa Serikali kuiimarisha idara hii. Viongozi wa Serikali kama wakuu wa mikoa nao wanapaswa kuwaelekeza wananchi kutumia idara hizo, badala ya kupoka madaraka yake na kutoa huduma hizo kama fadhila.

Operesheni hii ya Makonda itoe somo kwa idara ya Ustawi wa Jamii kujiimarisha kwa kusikiliza kero za kijamii haraka nchi zima.

Suala siyo tu kusuluhisha migogoro ya ndoa na waliotelekezwa baada ya kupewa mimba au kuwa na watoto tu, bali pia kutoa elimu ya jinsia, uhusiano na malezi ili kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima.

Siyo ustawi wa jamii tu, Serikali pia iimarishe mfumo wa kitaasisi tangu ngazi ya vijiji na mitaa kwenda kata, wilaya hadi mikoani.

Watu waanze kupata misaada ya kisheria tangu mitaani, wakishindwana waende kwenye ngazi za Mahakama za Mwanzo, wilaya na kuendelea.

Naamini kwamba haya yote yakifanyika kwa utaratibu huu, kila kitu kitakwenda sawa na mkuu wa mkoa atakuwa na kazi nyepesi ya kusimamia na kuratibu utekelezaji wake.

0754 897 287