PIRAMIDI YA AFYA: Saikolojia inavyoathiri nguvu za kiume

Muktasari:

Na ili uweze kufanya matukio haya, kuna hitajika kusiwe na mwingiliano wa shughuli za mfumo wa fahamu.

Leo tunageukia matatizo ya kisaikologia yanavyoweza kuathiri nguvu za kiume.

Kama nilivyowahi kueleza hapo awali kuwa tendo la ndoa linahusisha mtiririko wa matukio mengi ya kimwili, huku ubongo ndio mhimili mkuu wa jambo hilo kuweza kutendeka.

Ubongo ndio unaopokea na kutafsiri mambo ya kimwili ikiwamo hisia za kimwili na kufanya uamuzi wa nini kifanyike.

Na ili uweze kufanya matukio haya, kuna hitajika kusiwe na mwingiliano wa shughuli za mfumo wa fahamu.

Matatizo ya kisaikologia yanachangia tatizo la nguvu za kiume kwa kati ya asilimia 10-20. Huwa ni matokeo baada ya kuwapo kwa chanzo kingine, mfano unaweza ukajikuta umefukuzwa kazi hivyo ukawa una mawazo mazito. Mawazo hayo yanakufanya usiwe na utulivu wakiakili hali inayoathiri  hisia zako.

Mara nyingi matatizo yakisaikologia yanaweza kuanza nyakati za utotoni baada ya kunyanyaswa kijinsia au kuumizwa kimapenzi.

Matatizo hayo ambayo yanajitokeza katika jamii yetu ni pamoja na kupewa malezi mabaya, kufanyiwa vitendo viovu, mifarakano ya wazazi, kulawitiwa na kuona matukio ya kutisha utotoni.

Ukiacha hayo, yapo matatizo yakisaikologia ambayo ndio mara nyingi huchangia uwapo wa tatizo hili ikiwamo haya yafuatayo;

Shinikizo la kiakili (stress) ni tatizo ambalo lipo katika jamii na linaweza kumuathiri mtu ikiwamo matatizo ya kazini, kifedha, mifarakano ya ndoa/mapenzi na maudhi mbalimbali.

Pale mwanaume yeyote anapojikuta amepata tatizo hili kwa mara ya kwanza, hujikuta ana kuwa mwoga na mwenye wasiwasi pale anapokutana na mtu kwa mara nyingine.

Huwa anakuwa amejenga dhana akilini mwake kuwa huenda atashindwa tena na kuabika kwa mwenza wake. Mwanaume huyo hujikuta akijihisi kuwa yeye ni mkosaji kwa kushindwa kumridhisha mwenza wake.

Sonona/mfadhaiko wa kiakili ni tatizo linalowakuta wanaume ambao hujikuta wakiathiri nguvu zao za kiume. Uwapo wa tatizo hili humuathiri mtu kiakili na kimaumbile.

Pia, linaweza kumuathiri hata akiwa amepata utulivu wa kuweza kujamiana na mwenza wake.

Kutojiamini kwa mtu ni chanzo kingine cha kushindwa kuwa na nguvu za kiume, kujiona kuwa hamtoshelezi mwenza wake.

Kujiona ukotofauti; huwapata watu wenye umri mkubwa wakiwamo wazee kabisa. Kwani umri unaposogea, mtu hukosa mwamko wa kuhitaji tendo la ndoa.

Hujaribu kukumbuka kipindi akiwa kijana na mwenye nguvu zilizomfanya aweze kutenda tendo hilo kiufasaha. Sasa wanapo kuwa wazee hujikatia tamaa na kujiona wadhaifu na hapo ndipo huweza kujiathiri zaidi na zaidi.

Mara nyingine watu wenye umri mkubwa huwa na matatizo mbalimbali ya kiafya yanayochangia kudhoofika mwili na hasa kukiwa na mifarakano inayoweza kusababisha vurugu kwenye uhusiano.

Mtu anaweza akawa amefiwa na mkewe, hujikuta akipata hali ya simanzi kwa muda mrefu. Hali hiyo nayo inaweza kumsababishia kukosa mwamko wa tendo.

Usikose toleo lako wiki ijayo kwani tumefikia hatua muhimu ya uchunguzi na matibabu ya kupungua/kukosa nguvu za kiume.