Panya wafanya maajabu maabara ya kifua kikuu

Panya aina hii hutumika kubaini mabomu yaliyotegwa ardhini

Muktasari:

  • Kwani akiingia ndani ya nyumba hutafuna nguo, vyakula na vitu vingine vingi zikiwamo nyaraka mbalimbali.

Panya ni mnyama anayejulikana na kila mtu katika familia na kwa kawaida akionekana machoni pa mwanadamu lazima atauawa ama kwa kutegwa na mitego ili anase kisha auawe au hutegewa chakula chenye sumu ale afe. Na yote hii husababishwa na tabia yake ya uharibifu.

Kwani akiingia ndani ya nyumba hutafuna nguo, vyakula na vitu vingine vingi zikiwamo nyaraka mbalimbali.

Kutokana na tabia hiyo, watu wengi huwachukia na hufanya juhudi za kuwaangamiza mara wawanapowabaini kuwapo ndani ya nyumba.

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ni miongoni mwa watu ambao wameshuhudia balaa la panya kwani hivi karibuni alikwama kutekeleza majukumu yake ya urais.

Buhari alikwama baada ya vifaa kadhaa vya ofisi yake ya Ikulu kuharibiwa na wanyama hao, zikiwamo samani za viyoyozi.

Uharibifu huo ulifanywa na panya wakati Rais huyo alipokuwa safarini Jijini London, Uingereza alikokaa kwa siku 103.

Hata hivyo, baadhi ya wasomi huwathamini wanyama hao kwa sababu ni nyenzo za kufanyia kazi zao za utafiti wa aina ukiwamo wa mafunzo ya tiba.

Kuna aina nyingi za panya ambao ni pamoja na Zucker wanaotumika kwenye maabara.

Panya hao wanaaminika kuwa huugua kifua kikuu na magonjwa mengine ya binadamu.

Akizungumza na Gazeti hili, Mtafiti wa Kituo cha Udhibiti wa viumbe hai waharibifu wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA- Apopo), Dk Georgies Mgode anasema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazonufaika na panya hao ambao tayari wamesaidia utambuzi wa wagonjwa 10,000 wenye TB.

“Panya walibaini wagonjwa hao wana vimelea vya TB, wakati kipimo cha hospitali kilionyesha hawana. Hata hivyo kati ya wagonjwa 10,000, wagonjwa 3,600 ndiyo walipatiwa matibabu,” anasema Dk Mgode. Dk huyo alifafanua kwa nini wagonjwa 6,400 hawakupatiwa matibabu.

Anasema; “Makohozi tunayapata kutoka hospitali mbalimbali, hivyo sisi hatuwasiliani na wagonjwa, kwa hiyo hata baada ya kupata majibu, tuliyarejesha hospitalini tukiweka msisitizo kwa wahusika kuwapata wagonjwa hao ili watibiwe.”

“Lakini baadhi ya hospitali walishindwa kuwapata kwa madai kuwa taarifa zao za makazi hazijulikana.”

Anasema takwimu za 2011, panya waligundua makohozi ya watu 386 yaliyokuwa na vya TB, na mgonjwa mmoja laipatikana na akapatiwa matibabu na 2012 makohozi ya wagonjwa 555 yalibainika kuwa na TB na waathirika 47 pekee ndiyo walipatiwa matibabu.

Mwaka 2013 panya hao walibaini wagojwa 1,807 na waliotibiwa ni 1,020, huku 2014 wagonjwa 1,412 walipatikana na 777 walitibiwa. Mwaka 2015 wagonjwa 1,198 walibainika na 870 walipatiwa matibabu.

“ Kwa hiyo asilimia 27 ya wagonjwa wanaobainika kuwa na TB baada ya makohozi yao kupimwa hawatibiwi, hii ni kutokana na kwamba sisi hatuwasiliani na mgonjwa bali na hospitali husika,” anasema .

Anabainisha kutokana na hali hiyo hospitali zimekuwa zilipata changamoto kuwapata tena wagonjwa hao ili kuwapa majibu ya kipimo kilichofanywa na panya, kwa sababu walishawapa majibu ya vipimo vya mashine.

Anasema panya waliofuzu mafunzo hayo ya upimaji wa vidudu vya TB ni 42, kati yao 9 wapo kwenye kituo cha upimaji Dar es Salaam, 10 wamepelekwa nchini Msumbiji na wengine wapo SUA.

Makadirio ya gharama za matunzo kwa panya mmoja hadi anapofuzu mafunzo hayo ni dola za Marekani 1,000, wamesaidia kuongeza ugunduzi wa wagonjwa wenye TB kwa asilimia 40 ya wale wanaogundulika kwa vipimo vya hospitali.

Dk Mgode anasema walianza mradi wa panya wa vipimo vya TB walianzia kwenye hospitali 4 ambazo ni Mwananyamala, Amana, Tandale na Mnazi Mmoja , lakini sasa mradi umetanuka na kupatikana kwenye hospitali 28 .

“ Kati ya hospitali hizo 24 zipo jijini Dar es Salaam, tatu zipo mkoani Morogoro na nyingine moja ipo Pwani , Dar tunaipa kipaumbele kwa sababu kuna wagonjwa wengi kutokana na hali ya idadi ya watu kuwa wengi ikilinganishwa na mikoa mingine,” anasema.

kusanya sampuli

Anasema awali siku ya ijumaa ndiyo waliitumia kukusanya sampuli za makohozi kutoka hospitali kwenye hospitali kadhaa walizokuwa wanashirikiana nazo, ambapo walikusanya sampuli zaidi ya 800 za makohozi.

Anasema kuwa makohozi hayo huhifadhiwa kwenye majokofu maalum, kwa mpangilio mzuri wa kuweka alama maalum ya kutambua yamechukuliwa kutoka hospitali ipi ili kuweka rekodi ya majibu vizuri.

“ Hatua ya kukusanya hadi kufanya vipimo iliwakuwa inachukua siku 8 au 10 hadi majibu yapatikane, mara kwa mara hupokea sampuli zilizoonekana ‘negative’, lakini, panya wanapozipima upya huzibaini kuwa na vijidudu vya TB,”anasema.

Anasema kuwa kituo cha Apopo – SUA baada ya kubaini mafanikio ya huduma hiyo ya upimaji na jinsi inavyosaidia kuokoa wanaotambulika kuanza kutibiwa, wameamua kuisogeza kwa kujenga maabara yao Temeke jijini Dar es Salaam,

Dk Mgode anasema hata hivyo teknolojia hii ya kipimo cha panya bado haijapitishwa na Shirika la Afya Duniani, hivyo SUA wanaendelea kukusanya ushahidi wa kiutafiti wa teknolojia ili kuifanya iweze kutambulika na kutumiwa kimataifa .

Mojawapo ya tafiti tunazofanya ni kulinganisha na vinasaba vinavyopimwa na mashine culture ambapo unachukua kuotesha chakula cha mdudu huyo, culture ndiyo gold stardard test,”anasema.

Anasema kwa utaalam kila ugonjwa una kipimo chake kilichopitishwa kuotesha makohozi ili kupata wadudu wa TB ni kufanya hiyo culture.

Anabainisha kuwa utafiti huo wanaufanya kupitia Mpango wa Taifa wa kutokomeza kifua kikuu na ukoma chini ya Wizara ya Afya, ambao ndiyo wanatoa nafasi ya kuwakutanisha na wagonjwa.

Mmoja wa walimu wa mafunzo wa panya hao, Said Dibwe anaeleza kuwa wapo kuna panya ambao hufeli kwenye mafunzo hivyo kushindwa kutumika kwa shughuli zilizokusudiwa.

Anabainisha kuwa mafunzo kwa wanyama hao yamegawanyika kwa kuwa wapo pia ambao wamekuwa wakifundishwa kutambua mabomu na hao wa TB.

Dibwe anasema panya hao wanafanya mazoezi lakini ingawa wama mafunzo lishe tofauti kwani wale wa TB, kwenye lishe yao uongezewa zaidi tembe za vitamini, wakati wale wa mabomu hupewa ndizi na karanga zilizosagwa.

“ Kwa kawaida panya ambaye ni mwelevu huweza kufuzu mafunzo tunayowapa ndani ya miezi mitatu hadi sita, “ anasema.

Anafafanya kuwa “wapo tofauti na wale ambao wanaishi ndani ya nyumba hawa wanaishi kwenye mashimo tunawalisha chakula kiasi ili waweze kufanya kazi kwa kuwa wakishiba wanakuwa wavivu,” anasema Dibwe.

Anasema pia tayari wajulishwa kwamba wajiandae kuna mpango wa kuanza kuwafundisha panya wengine mafunzo ya utambuzi wa damu yenye malaria na dawa za kulevya, ikiwa ni hatua ya kuhakikisha kwamba tunaendelea kunufaika na uguduzi wa matumizi ya panya kuwa kipimo,” anasema Dibwe.

Dondoo

Kwa mujibu wa taarifa za wataalam wa panya wanabainisha kuwa wanyama hao ni muhimu na wamekuwa wakitumiwa kwenye nchi nyingi mfano mwaka 1895, Chuo kikuu cha Clark, Worcester, Massachusetts (Marekani) kilianzisha kundi kubwa la panya weupe kwa ajili ya kujifunza madhara ya chakula na mapungufu mengine ya mwili.

Kwa miaka mingi panya wametumika kama viungo vya tafiti za magonjwa mbalimbali na kuongeza ufahamu wetu kuhusu viasilia, magonjwa na madhara ya madawa, na mada nyingine ambazo zimechangia mambo makubwa ya afya ya mwili wa binadamu.

Uchunguzi wa mwaka 2007 umebaini kuwa panya wana uwezo na akili, ambapo hapo awali ulionekana upo kwa binadamu pekee na baadhi ya wanyama wa kale .

Pia wanabainisha kuwa panya wa kufugwa ni tofauti sana na wale wa mwituni, kwani ni wapole na hung’ata kwa nadra sana. Huvumilia uwepo wa watu wengi na huzaliana mapema na kwa wingi sana.