Piga tu kura ipo siku utacheka

Muktasari:

Kutokana na ushindi huo wa kishindo kuna watu wamekuwa na imani tofauti wakisema kwamba hakuna sababu ya kushiriki kupiga kura kwa sababu kila wanapopiga chama tawala -CCM kinashinda.

Septemba 16, mwaka huu ilikuwa mshikemshike kwenye majimbo ya Ukonga jijini Dar es Salaam na Monduli mkoani Arusha, ambapo wananchi walishiriki kupiga kura baada ya waliokuwa wabunge wa majimbo hayo kujitoa na kujiunga CCM, na kushinda tena.

Kutokana na ushindi huo wa kishindo kuna watu wamekuwa na imani tofauti wakisema kwamba hakuna sababu ya kushiriki kupiga kura kwa sababu kila wanapopiga chama tawala -CCM kinashinda.

Ukweli ni kwamba kura ni haki ya msingi ya kila raia mwenye akili timamu na aliyetimiza umri wa kupiga kura na akiacha kupiga kura afahamu kabisa kwamba haki yake inapotea.

Suala la uchaguzi unaweza kuufananisha na timu za mpira zinapokuwa uwanjani kwenye mchezo wa fainali ambapo ni lazima moja ifungwe na nyingine ishinde - isherehekee ushindi wake.

Wengine wanadiriki kusema kwamba walipiga kura huku wakifahamu kwamba ushindi ni wa nani, lakini kwa sababu wanatimiza wajibu wao walilazimika kupiga tu kura.

Jimbo la Ukonga aliyekuwa mgombea Mwita Waitara wa CCM aliibuka kidedea kwa kupata kura 77,795 akifuatiwa na mgombea wa Chadema, Asia Msangi aliyeambulia kura 8,676.

Katika Jimbo la Monduli mgombea wa CCM, Julius Kalanga alipata kura 65,714 akifuatiwa na mgombea wa Chadema, Yonas Laizer aliyepata kura 3,187

Kwa matokeo hayo wapinzani walijitokeza wakisema kwamba hawana sababu ya kupiga kura tena kwenye chaguzi nyingine wakidai wamekata tamaa na matokeo hayo.

Walisikika wakisema kwamba kitendo cha mawakala wao kutolewa kwenye vituo vya kura ni chanzo cha wao kushindwa kwenye chaguzi hizo, ambazo zinafanyika mara kwa mara nchini kutokana na baada wabunge na madiwani kujitoa na kuhama vyama hasa wakihamia CCm.

Ninachouliza ni kwamba wakati wa uchaguzi kunakuwa na mshindi wa kwanza na wa pili, sasa ikiwa yule wa kwanza ameamua kujiuzulu inakuwaje asichukuliwe yule mshindi wa pili akaapishwa kuwa mbunge wa eneo husika?

Ingawa hili ni suala la kisheria, lakini inawezekana kuzibadilisha ili mshindi wa pili ashike nafasi.

Huenda hii ndiyo inawakatisha tamaa baadhi ya wanasiasa kushiriki chaguzi zinazofuata.

Ushauri wangu ni kwamba mshindi wa pili ni vyema apewe nafasi ya kuwa mbunge mara tu inapotokea aliyekuwapo ameamua kujiuzulu kwani, kwanza gharama zitapungua na zile fedha za kusimamia uchaguzi zinaweza kufanyia mambo mengine ya maendeleo. Upo upungufu wa vituo vya afya, shule, barabara nyingi hazipitiki, ukosefu wa umeme na maji kwenye baadhi ya mikoa.

Hakuna mtu ambaye hataki maendeleo na maendeleo hayaji bila kuwa na viongozi bora, kwa hiyo ikiwa umechaguliwa na wananchi ujue umekubalika, lakini unapoamua kujiuzulu unarudisha nyuma maendeleo na kusababisha hasara kwa Taifa.

Hawa wanaojiondoa kwenye vyama wakisema wanaunga mkono Serikali kwa jitihada zake wanakosea kwa sababu wanaweza wakatumia nafasi walizonazo kwenye vyama vyao kuunga mkono pia jitihada za Serikali.

Kabla mtu hajaondoka kwenye chama chake ajiulize kuwa jamii itamchukuliaje kwanza au amewafanyia nini wapiga kura wake ambao anakwenda kuwaomba tena kura kwa mara nyingine.

Hili jambo linakatisha tamaa ndiyo hata idadi ya wapiga kura wanapungua kwa sababu wanadhani ni mchezo wa kuigiza kwa wanasiasa kuhamahama vyama badala ya kusimamia maendeleo ya wananchi.

Ikiwa mtu ana nia ya kuunga mkono Serikali, basi aiunge kwelikweli hata kama yuko upinzani kwa sababu sauti yake itasikika tu hata akiwa chini ya kabati, lakini siyo kuhama chama akiwa bado anawatumikia wananchi wake.

Ikiwa mtu amekomaa sawasawa kisiasa hawezi kuhama chama kwa kujivua ubunge au udiwani wakati anakubalika kwa wananchi.

Ushauri wangu nautoa kwa viongozi wa vyama vya siasa kuhakikisha wanachunguzana kwanza kabla ya kupitisha majina ya wagombea ili kuepuka adha hii kwa wananchi ya kupiga kura mara ya pili.

Kuna sababu ya watu kupiga kura mara ya pili mojawapo kubwa ikiwa ni kifo cha mbunge au diwani, lakini suala la kujiuzulu ni bora tu sheria ziruhusu apitishwe yule aliyepata nafasi ya pili.