Pilipili manga, mdalasini vyaweza kusaidia kuokoa ndoa

Wengi wa wagonjwa hawa huwa na aibu kufika katika huduma za afya kwa ajili ya uchunguzi wa tatizo hilo wakihofia kunyanyapaliwa lakini jambo hilo halipo kwa wataalam wenye taaluma ya tiba za binadamu.

Muktasari:

> Pilipili manga, mdalasini, figo, makoma manga, kweme na njugu mawe huongeza nguvu za kiume

Baada ya kuona makala mbalimbali zimekuwa zikizungumzia sababu zinazochangia matatizo ya nguvu za kiume, sasa ungana nami kusoma kipengele muhimu kinachohusu suluhisho la matatizo ya nguvu za kiume.

Kikubwa unachotakiwa kufanya ili kuweza kupata msaada wa tatizo hilo ni kuwa tayari kuweka wazi tatizo lako kwa watoa huduma za afya wa tiba za binadamu na sio kwa watoa huduma wasiotambulika. Hata kama ikitokea tatizo lako linaweza lisitatulike, ni vizuri ukakubaliana na hali hiyo, tambua kuwa kukosa nguvu za kiume si mwisho wa maisha yako.

Uwapo wa matangazo mengi mtaani ya dawa za kuongeza nguvu za kiume haumanishi kuwa yanaweza kutatua tatizo lako, hiyo ni biashara ya wajanja wa mataani.  Unaweza ukawa unatumia dawa hizo na kupata nafuu na ukadhani kuwa umepona, lakini kumbe ukawa unaudhuru zaidi mwili wako bila kujua.

Dawa hizo  hazijathibitishwa wala kupendekezwa kama ni salama na Taasisi ya Chakula na  Dawa (TFDA), yapo kila mahali mitaani na wengi hujikuta wakinunua na kuyatumia kiholela.

Tayari imeshawahi kuripotiwa kuna watu wamepoteza maisha baada ya kunywa dawa hizo kiholela pasipo kuzingatia ushauri wa wataalamu wa tiba.

Tatizo la nguvu za kiume linaweza kutibiwa au likapunguzwa makali kwa matibabu mbalimbali baada ya kufanyiwa uchunguzi na wataalamu wa afya.

Yapo matatizo ya nguvu za kiume ambayo hayatatuliki kwa njia yoyote, hivyo mtu mwenye tatizo hilo huwa ni ulemavu wa kudumu.

Kabla ya kufika huko, ni vizuri ukatambua kuwa yapo matibabu salama unayoweza kuyafanya kuimarisha hali ya tendo kabla ya kumfikia daktari.

Mazoezi ni moja ya kitu  muhimu kwa mtu mwenye tatizo hilo, kwani humsaidia kuwa imara.

Yawezekana amekua mtu mzima lakini akifanya mazoezi mepesi ya kutembea yanaweza kumsaidia.

Lakini unene pia ni chanzo kingine cha kupata maradhi kama kisukari, magonjwa ya moyo, mishipa ya damu na shinikizo la damu. Maradhi haya ndio yanayoharibu mishipa ya damu na mishipa ya fahamu na ndio chanzo kikuu cha kupungukiwa kwa nguvu za kiume.

Aina ya vyakula

Vyakula vya nafaka ambavyo vimesheheni nishati nyingi, nafaka zenye nyuzinyuzi (fibre) na sukari (complex sugar), husaidia kutunza uzito wa mwili.

Nafaka husaidia kuzalisha homoni za testosterone kwenye damu na huwezesha mtu kuwa na nguvu hatimaye kuongeza nguvu zake za kiume.

Kula nafaka zisizokobolewa kama vile brown bread badala ya white bread, pia kula nafaka halisi badala ya cornflakes ni jambo zuri kiafya. Zina saidia kutokuupa mwili mafuta mengi. Ikumbukwe kuwa uwapo wa mafuta mabaya mwilini huharibu mishipa ya damu ikiwamo ya uume.

Tangawizi ni aina ya kiungo ambacho mizizi yake husisimua mfumo wa mzunguko wa damu mwilini. Mzunguko unapokuwa mzuri huwezesha damu kwenda sehemu za viungo vya uzazi bila tatizo.

Tangawizi hutumika sana maeneo ya Asia kwa ajili ya wanaume wenye tatizo la nguvu za kiume.

Viungo ambavyo viko katika pilau ni mojawapo ya vitu ambavyo miaka na miaka vimetumika katika maeneo ya Asia na Amerika Kaskazini kama vyakula vinavyoimarisha nguvu za kiume.

Vyakula vinginevyo.

Pemigranate ni aina fulani ya matunda yenye rangi nyekundu yenye mwonekano kama apple.

Tunda hili husaidia kuamsha mishipa ya fahamu na kuweka mawasiliano sahihi ya mwili, hivyo kumuongezea mtu uwezo wa kufanya tendo la ndoa kwa hamasa kubwa. Humfanya mtumiaji kupokea hisia za mapenzi kwa urahisi zaidi.

Mvinyo mwekundu unatajwa pia kuwa na uwezo wa kuuchangamsha mwili na kuongeza msukumo wa damu huku ikimuondolea mtu uchovu kabla na baada ya tendo la ndoa.

Hii ndio sababu kubwa inayofanya iwekwe vyumbani katika mahoteli makubwa duniani. Nchi kama Italia, mvinyo ni kinywaji ambacho hakikosekani mezani kutokana na kuaminika miaka kwa miaka.

Unywaji wa kiasi unaweza kuwa na faida kubwa kwa kuchochea na kuamsha hisia na kuweza kwenda mizunguko kadhaa.

Mchanganyiko wa mbegu mbalimbali za matunda ikiwamo tikiti maji, mbegu za maboga  pia husaidia kuondoa ACID mwilini na kumfanya mtu ajione ni mwenye afya njema.

Vanila husaidia kuamsha hamasa mwilini, vanila ni aina ya kirurubisho ambacho huwa ndani ya vyakula  kama ice cream.

Asali, ina madini yanayoitwa boron ambayo husaidia mwili kutumia homoni.

Hata vitabu vya dini hueleza ulaji wa asali na masega yake kama mlo wenye kuupa mwili nguvu. Zipo tafiti lukuki kuhusu faida za asali ikiwamo ya kuongeza nguvu za kiume.

Karanga huhusika moja kwa moja na kutunza mfumo wa mzunguko wa damu kuwa na afya. Husaidia kuimarisha mzunguko wa damu katika maeneo ya uzazi, hivyo, kuongeza msisimko wa tendo.

Pia, karanga zina madini muhimu kama ya magineziamu , tindikali ya foliki na madini ya zinki ambayo ni muhimu sana katika uzalishaji wa mbegu za mwanaume na kuongeza hisia. Ulaji wa Chokoleti pia huongeza uchangamfu mwilini unaomuwezesha mtu anayeshiriki tendo la ndoa kuwa na mguso sahihi kwenye fikra zake.

Imeandaliwa na Hadija Jumanne