Polepole unaikumbuka ‘Legitimacy ?

Muktasari:

Muktadha wa pili ile hali ya kiongozi kuwa na mamlaka ya kuamua jambo au mambo kisheria. Katika Makala haya, nitazungumzia Legitimacy katika muktadha wa uhalali wa kisiasa kwa watu anaowaongoza.


Legitimacy inaweza kutafsiriwa katika muktadha wa kisheria au uhalali wa kisiasa. Kwanza ni ile hali ya mwanasiasa anavyotazamwa katika jamii, uhalali wake kwa watu. Anakubalika vipi kimaadili, uongozi na vigezo vingine vinavyoshawishi kiongozi anayefaa.

Muktadha wa pili ile hali ya kiongozi kuwa na mamlaka ya kuamua jambo au mambo kisheria. Katika Makala haya, nitazungumzia Legitimacy katika muktadha wa uhalali wa kisiasa kwa watu anaowaongoza.

Tafsiri hii ilielezwa kwa kinaga ubaga na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alipokuwa akiendesha vita ya kumwangusha Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa asipate nafasi ya kuiona Ikulu.

Polepole aliyejizolea umaarufu zaidi katika mchakato wa Katiba mpya, baadaye aligeuka mkosoaji wa Chadema na Ukawa baada ya kumpitisha Lowassa kuwa mgombea urais wake. Lowassa alihama CCM baada ya jina lake kukatwa kwa madai ya kuwa na madoa kisiasa.

Agosti 9, 2015, saa tatu usiku kupitia kipindi cha Mada Moto, kinachorushwa na Channel Ten, Polepole alikutana meza moja na mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) kujadili mada iliyohusu ‘Edward Lowassa ndani ya Ukawa’.

Polepole alijenga hoja kwa kutumia msamiati wa Legitimacy na alitumia njia zote za mawasiliano katika mjadala ule, kuanzia hisia hadi kauli ambazo ziliingia kwenye kumbukumbu yangu.

Polepole alijenga hoja kwamba Lowassa ana madoa na hana uhalali wa kupewa dhamana na Watanzania kuongoza Taifa hili. Polepole akasema kama CCM ingeendelea na watu wenye madoa wangeambukiza na wengine. “Mtu huyu hafai kuwa kiongozi wa Taifa letu (Lowassa) kwa sababu ya maadili na huwezi kusema tunasuburi mahakama ithibitishe. Kuna tofauti kati ya Legality na Legitimacy, kwenye siasa kuna Legitimacy, haihitaji wewe tukusafishe kisheria ili tuseme wewe ni muadilifu, Legitimacy ni namna unavyoishi, Legitimacy haipimwi mahakamani.” mwisho wa kunukuu.

Hata hivyo, ni miezi 26 tu imepita tangu Polepole alipozungumzia Legitimacy kwa kiongozi. Siku chache zilizopita wateule watatu wa Rais John Magufuli na kada wa CCM katika halmashauri mbili mkoni Arusha wameingia kwenye kashfa ya tuhuma za rushwa.

Lakini, Polepole amenukuliwa na baadhi vyombo vya habari akiwataka wanaotuhumu CCM kutumia rushwa kununua madiwani watoe ushahidi hadharani.

Polepole anasisitiza madiwani hao wanahamia CCM kwa ushawishi wa Rais Magufuli kupitia utekelezaji wa sera na ilani ya chama.

Hata hivyo, video na sauti zilizoonyeshwa hadharani na wabunge Joshua Nassari na Godbless Lema zimeonyesha na kusikika wateule hao wakiwashawishi madiwani kuhama Chadema ili wajiunge CCM na baadhi waliahidiwa wangelipwa posho za vikao vyao vilivyobaki hadi 2020 na kukamilishwa miradi yao.

Kinachonishtua ni hii tafsiri ya Legitimacy aliyotumia kama silaha katika kipindi cha kumpata kiongozi wa Taifa na kuacha kutumika baada ya video kuwaonyesha wateule hao wakishawishi madiwani.

Sijamsikia Polepole akizungumzia au kukemea au kuahidi kuchukua hatua yoyote ile na kuhoji nini kimemkuta?

Kilichoshangaza mmoja wa wanaodaiwa kuhusika na kashfa ya kununua madiwani kashinda uongozi kwenye uchaguzi wa CCM. Hii ndiyo Legitimacy uliyokuwa unataka kuwaaminisha Watanzania? Ni wewe Polepole uliyekuwa unakemea rushwa uchaguzi wa ndani?

Ni heri kushauri ukweli ukanusuru chama kuliko kukaa kimya ukapoteza uaminifu kwa chama hapo baadaye. Siasa ni hesabu ya utafutaji uhalali wa kisiasa na ukusanyaji wa mitaji. CCM inapoharibu, upinzani unahesabu mtaji imara katika uchaguzi ujao 2020. Itafakari upya Legitimacy.

[email protected] Naomba kuwasilisha .0716186074