Polisi msiharibu taswira yenu nzuri kwa jamii

Muktasari:

  • Sherehe hiyo iliyofanyika kwenye Kituo Kikuu cha Polisi ilihusisha hotuba, vinywaji baridi aina ya soda na furaha ya kurukaruka kwa ukakamavu ikiwamo kumbeba kwa juu juu Makonda.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda juzi alifanya tukio la kipekee kwa kufanya sherehe fupi ya kuwapongeza askari polisi kwa kufanikisha kazi ya ulinzi na usalama kwenye kipindi cha kampeni za uchaguzi wa Jimbo la Ukonga mkoani Dar es Salaam.

Sherehe hiyo iliyofanyika kwenye Kituo Kikuu cha Polisi ilihusisha hotuba, vinywaji baridi aina ya soda na furaha ya kurukaruka kwa ukakamavu ikiwamo kumbeba kwa juu juu Makonda.

Hatuna tatizo na sherehe hiyo kwa kuwa Makonda mbali na wadhifa wake wa ukuu wa mkoa, pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa.

Pia, hatuna nongwa na kitendo cha askari kupongezwa kwa kazi nzuri, kwani ni jambo zuri na linawatia moyo askari hao wenye jukumu la kulinda usalama wa raia na mali zao.

Hata hivyo, kinachotia dosari sherehe hizo ni kuwapo madai ya muda mrefu toka kwa vyama vya upinzani na wanaharakati wa masuala ya kijamii kwamba Jeshi la Polisi linatumika kupora demokrasia ya siasa za vyama vingi nchini.

Wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2015, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kupitia Mradi wa Kukuza Demokrasia (DEP), walitoa kitabu cha mwongozo kuhusu wajibu wa Jeshi la Polisi katika chaguzi za kidemokrasia.

Kitabu hicho kilichokuwa toleo la tatu la 2015, dibaji yake iliandikwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kwa wakati huo, Inspekta Jenerali (IGP) Ernest Mangu. Kwa sasa Mangu ni balozi wa Tanzania nchini Rwanda.

Baadhi ya maneno ya Mangu ni kwamba kitabu hicho kitumike kama marejeo katika kukuza mienendo ya kipolisi ya kidemokrasia ambayo ni lengo kuu la Jeshi la Polisi Tanzania.

Tunaamini polisi wote wanakisoma kitabu hiki ambacho kilitumika kuwapa mafunzo kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015. Pia tunaamini wameendelea kujikumbusha pale panapokuwapo na uchaguzi.

Kitabu hiki kinawaelekeza polisi kwamba wao ni wawakilishi wa Serikali na si vyama vya siasa na kwamba uchaguzi unapokuwa tulivu, huru na haki ndiyo jukumu lao la msingi.

Tunaamini polisi wameendelea kujikumbusha kwamba moja ya kanuni ya shughuli za kipolisi katika jamii ya kidemokrasia ni ile inayozingatia kwamba Jeshi la Polisi linatumikia watu na si dola.

Hivyo, kitendo cha askari wa Kituo Kikuu cha Polisi kuonekana hadharani tena siku moja baada ya uchaguzi hakuleti picha nzuri kwa jeshi hilo mbele ya jamii kwamba wanatekeleza majukumu yao kwa weledi.

Pongezi kwa askari hao kama zingeandaliwa na IGP au kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, isingekuwa shida kwa kuwa makamanda ndio wenye jukumu la kutoa amri na kuwasimamia walio chini yao huku wakitakiwa kuifanya kazi hiyo kwa kuheshimu maadili ya Serikali ya kidemokrasia.

Rai yetu ni kuwakumbusha polisi kabla ya kufanya mambo ambayo yanaweza kuharibu taswira yao mbele ya jamii, wanapaswa kujiuliza maswali kadhaa kwamba ni kitu gani kinachounganisha haki za binadamu na shughuli za kipolisi katika jamii ya kidemokrasia?

Wajiulize nini maana ya demokrasia? Au utawala bora unamaanisha nini? Pia, kwa nini ni muhimu maofisa wa polisi kuheshimu na kulinda haki za binadamu za wanajamii wote?

Tunaamini sherehe ya kujipongeza kati ya polisi na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ilikuwa ni kupitiwa kibinadamu, hivyo hali hiyo haitajirudia tena sehemu yoyote nchini. Pia tunasisitiza kwa kulitaka jeshi letu kujikita kulinda hadhi na weledi wake.