Pongezi Ecowas, jumuiya nyingine Afrika zifuate

Rais wa zamani wa Gambia, Yahya Jammeh.

Muktasari:

Jammeh, ambaye ameliongoza taifa la Gambia kwa takribani miaka 22, alikuwa amekataa kuondoka madarakani baada ya kushindwa kwenye Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana.

Rais wa zamani wa Gambia, Yahya Jammeh amekubali kuachia madaraka baada ya rais wa Guinea, Alpha Conde na wa Mauritania, Mohamed Ould Abdel Aziz kuongoza mazungumzo yaliyomfanya afikie uamuzi huo.

Jammeh, ambaye ameliongoza taifa la Gambia kwa takribani miaka 22, alikuwa amekataa kuondoka madarakani baada ya kushindwa kwenye Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana.

Awali, Jammeh alikubali matokeo hayo baada ya kutangazwa kwa matokeo, lakini siku chache baadaye akabadilisha uamuzi na kufungua kesi akipinga matokeo hayo.

Hata hivyo, Umoja wa Kiuchumi wa Nchi za Magharibi mwa Afrika (Ecowas), ulimtaka akubaliane na matokeo ya uchaguzi, ikiwa ni ishara ya kuheshimu demokrasia kwa kukubaliana na uamuzi wa wengi.

Lakini, kiongozi huyo aligoma na hata walipomwambia kuwa angepewa hifadhi nchini Guinea au Nigeria, hakutaka kusikiliza na badala yake akatangaza hali ya hatari.

Ecowas haikutaka uamuzi wa wengi upuuzwe na hivyo kukubaliana kupeleka majeshi yake ili kumuondoa Jammeh na kumuweka Adama Barrow, ambaye alishinda. Pia, Ecowas ikaamua Barrow aapishwe hata nje ya nchi wakati juhudi za kumuondoa Jammeh zikiendelea.

Baada ya jeshi linaloundwa na askari kutoka nchi wanachama wa Ecowas kuanza kuingia Gambia kwa ajili ya kumuondoa Jammeh, kiongozi huyo wa muda mrefu aliripotiwa kukubali kuachia madaraka.

Hata kama habari hizo zitakuwa hazijatimia, kuna somo ambalo tumelipata kutoka Ecowas. Jumuiya hiyo imefanya jambo la busara kuamua kuisimamia na kuitetea demokrasia badala ya utamaduni uliozoeleka wa wakuu wa nchi kuogopana kuambiana ukweli katika mambo ya msingi, hasa ya ukiukwaji wa demokrasia.

Ecowas imeonyesha umuhimu wa kusimamia, kuilinda na kuiheshimu demokrasia kwa kuamua hata kutumia majeshi ili kumuondoa mtu ambaye amedharau uamuzi wa wengi.

Hili ni jambo ambalo jumuiya nyingine za kikanda inabidi ziige katika kuimarisha demokrasia katika nchi wanachama ili kuharakisha maendeleo.

Tumeshuhudia katika nchi nyingi barani Afrika, demokrasia imekuwa ikipuuzwa, chaguzi kuchezewa na matokeo kuchakachuliwa na hivyo kupatikana viongozi ambao hawakubaliki.

Katika hali kama hiyo, wananchi wanakuwa hawaridhiki na hivyo, Serikali kulazimika kutumia nguvu nyingi katika kulinda ushindi huo, kutumia rasilimali za nchi kudhibiti wananchi badala ya kuzielekeza kwenye miradi ya maendeleo.

Matokeo yake huwa ni maendeleo kucheleweshwa na nchi kuendelea na umaskini miaka nenda rudi.

Jumuiya nyingine hazina budi kuiga mfano huo wa kuhakikisha demokrasia inalindwa kwa gharama zozote miongoni mwa nchi wanachama.

Hakuna haja tena ya kusubiri mataifa ya Magharibi yatuwekee vikwazo kutulazimisha kuheshimu demokrasia ambayo inatusaidia sisi wenyewe. Tunahitaji kudhibitiana sisi wenyewe kwa kutumia mbinu tofauti zitakazowafanya viongozi wa nchi wanachama wajione wana wajibu wa kuhakikisha wanajikita katika shughuli za maendeleo ili wananchi wawachague kutokana na maendeleo wanayoyaona badala ya kulazimika kutumia nguvu kujilinda.

Tunajua kuwa Katiba ya Umoja wa Mataifa iliweka kifungu kwenye katiba yake kinachokataza nchi kuingiliwa kwenye mambo yake ya ndani, lakini matumizi mabaya ya madaraka yamesababisha jumuiya ya kimataifa kutafuta mbinu nyingine ya kuhakikisha kifungu hicho kinaheshimiwa, lakini pia nchi zinadhibitiwa kutumia mamlaka hayo vibaya.

Moja ya mbinu hizo ni kama hiuyo iliyofanywa na Ecowas ya kuhakikisha nchi wanachama wake wanaheshimu demokrasia na pale wanapoonekana kutotaka kukubaliana na uamuzi wa wengi basi hata nguvu zitumike.

Jumuiya nyingine za kikanda barani Afrika hazina budi kuiga mfano wa Ecowas ili kuhakikisha wanachama wake wanaheshimu mambo ya msingi ya haki za binadamu.