Friday, November 4, 2016

Rais Magufuli amekuwa malaika miezi miwili, binadamu miezi 10

 

By Luqman Maloto, Mwananchi

Unaweza kuugawa mwaka wa kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli, katika sehemu mbili; umalaika na ubinadamu.

Kuanzia Novemba 5, 2015 alipoapishwa mpaka Desemba 31 mwaka jana, Rais Magufuli alijitengenezea haiba ya umalaika. Watanzania kwa wingi wao walimuona ni malaika aliyeshushwa na Mungu kuja kujibu shida zao.

Katika miezi hiyo miwili, hakupatikana binadamu aliyethubutu kuzungumza kwa sauti kumkosoa Rais Magufuli. Mtanzania mzuri alijitambulisha kwa jinsi alivyokuwa anamuunga mkono.

Kati ya Novemba 5 na Desemba 31 mwaka jana, Rais Magufuli alikuwa Mtanzania anayesemwa vizuri na watu kuliko mwingine yeyote. Waliokuwa hawakubaliani naye, walinong’ona kwa kujificha.

Miezi hiyo miwili, Rais Magufuli alifanikiwa kulielekeza Taifa zima Ikulu kwa macho yenye matumaini. Watanzania walionyesha imani yao kwa Rais wao kuliko mtu mwingine yeyote. Kipindi hicho kama ulitaka upingwe na kushambuliwa, ungethubutu kumkosoa Dk Magufuli.

Rais Magufuli aliingia kwa mtindo uliovutia wengi wa kutumbua majipu kwa kushughulikia uozo na ufisadi serikalini kisha kuwaondoa kazini aliowabaini ni tatizo.

Kipindi hicho kama ungethubutu kumsema vibaya, ungeitwa mtetea majipu. Mabadiliko yalikuwa makubwa kwenye eneo la utawala. Haikuwa mazoea kwa Watanzania kumsifu mtawala kwa kiwango ambacho Dk Magufuli alisifiwa.

Miezi miwili ya mwisho ya mwaka 2015, kumsifu Rais Magufuli ndiyo ilionekana kwenda na wakati.

Ni kipindi ambacho upinzani Tanzania ulidhaniwa ungekufa. Kila eneo ambalo ndilo hasa lilikuwa na hoja zilizobeba uhai wa wapinzani lilishughulikiwa na Dk Magufuli. Ikatokea vyama vya upinzani kujitokeza na kusema kuwa alikuwa anatekeleza sera na ilani zao za uchaguzi.

 

Umalaika wa Dk Magufuli

Ni vyema ifahamike kuwa Watanzania walikuwa wamechoshwa na uleaji mkubwa wa vitendo vya rushwa. Walikuwa na chuki kubwa dhidi ya ufisadi, kwa hiyo hawakuwa wakitaka kuona wenye kuitwa mafisadi wanaendelea kuvumiliwa.

Hapa ikae kwenye mstari wake kuwa maisha ni magumu. Na kwa kawaida ugumu wa maisha husababisha chuki kati ya aliyenacho na ambaye hana chochote. Ambaye hana huamini kukosa kwake ni matokeo ya kupata kwa aliyenacho. Mtanzania maskini huamini kuwa wenye kuitwa mafisadi ndiyo wamemsababishia ufukara.

Sisi wa maisha ya kawaida tunajua kuwa kipindi ambacho chakula hakuna, tunapokutana kwenye sahani inakuwa rahisi kuona matokeo ya kupigana macho na kumtambua mwenye kukata tonge kubwa.

Kipindi ambacho chakula kipo kingi, kila mtu anakula kwa uhuru na hakuna anayemtazama mwenzake anakataje tonge. Na ikitokea kuna mtu anakata tonge kubwa, wenzake humsema anakata kubwa kwa mtindo wa utani.

Hali za kimaisha kwa Watanzania wa kawaida ni mbaya. Ndiyo maana baada ya kuaminishwa kuwa wenye maisha mazuri ni mafisadi ambao wananyonya jasho lao, chuki yao ikawa kubwa.

Wimbo wa ufisadi usingekuwa santuri bora kama wananchi wa kawaida wangekuwa wanajitosheleza kimaisha. Kila mtu kwa nafasi yake angekuwa anapata mahitaji yake muhimu.

Shida ni kuwa mwananchi anaambiwa kuna mtu ameiba Sh15 bilioni, wakati yeye maisha yake yote hajawahi kukamata Sh15 milioni kwa mkupuo mmoja. Hapo alipo, mwanaye hana ada ya shule na amelala njaa. Chuki kubwa imezaliwa kwa sababu hiyo ya kimaisha.

Rais Magufuli asingeonekana kiongozi mpendwa mithili ya malaika Novemba na Desemba, mwaka jana kwa mtindo wake wa kutumbua majipu kama wananchi wa Tanzania wangekuwa na maisha mazuri. Ugumu wa maisha huzalisha chuki kubwa.

Majipu ya nini wakati kila mtu anajitosheleza?

Hata habari za ufisadi na utumbuaji majipu zingekuwa zinachukuliwa kwa hali ya kawaida mithili ya mwenye kukata tonge kubwa nyakati za chakula kingi.

Hivyo basi, Rais Magufuli alivyokuwa anatumbua majipu, ndivyo na sehemu kubwa ya wananchi ilivyopata ahueni. Aliweza kuwakuna sehemu ambayo ilikuwa inawawasha kwa kitambo kirefu kabla yake.

Mtanzania wa kawaida alifurahia majipu kutumbuliwa kwa imani kuwa utumbuaji huo utasababisha nafuu kwake ya kimaisha. Kwa hali hiyo ilikuwa vigumu kuwageuza ghafla wananchi kumuona Rais Magufuli ni binadamu wa kawaida na ambaye anaweza kufanya makosa.

Dk Magufuli akawa anawamaliza kwa majibu yake kuwa wanaomsemasema nao ni majipu yanayohitaji kutumbuliwa. Na aliposema hivyo kila upande ulijawa vicheko kwamba anawaweza wakosoaji wake.

 

Taa nyekundu kwa wapinzani

Miezi miwili ya umalaika wa Dk Magufuli iliwapa wakati mgumu wapinzani. Wapo waliodiriki kutamka kuwa nchi haina haja ya upinzani tena, maana kile kilichokuwa kinapigiwa kelele na wapinzani Rais Magufuli alionekana anakitekeleza kuliko matarajio.

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe alipata kuisema kasi ya Dk Magufuli kwamba inahitaji kudhibitiwa na Bunge imara kwa kuwa bila hivyo Rais anaweza kufanya kila kitu anavyotaka.

Zitto alisema hivyo kutokana na kuona kasi ya Dk Magufuli ilivyokuwa inaungwa mkono na Watanzania.

Ni ukweli kuwa jinsi ambavyo Dk Magufuli alivyoanza na kasi yake, alionekana kufunika mihimili mingine. Hivyo, Bunge kama mhimili wenye jukumu la kuisimamia Serikali ulipaswa kujitambua.

Novemba mwaka jana, mhadhiri maarufu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Kitila Mkumbo aliandika kupitia akaunti yake ya Twitter akisema: “Siasa za upinzani hazina budi kubadilika. Siasa za kutafuta makosa ya CCM zimepitwa na wakati.”

Kitila, ambaye ni mshauri wa Chama cha ACT-Wazalendo aliyepata kuwa mjumbe wa Kati Kuu ya Chadema, alisema hayo kutokana na mtindo wa uongozi wa Rais Magufuli kujikita zaidi katika kushughulikia moja kwa moja kero za muda mrefu za Watanzania.

Novemba 20, mwaka jana wabunge wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), walitoka bungeni kususia hotuba ya Dk Magufuli kuzindua Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hata hivyo, ususiaji wao haukupata mapokeo makubwa kama ilivyokuwa wakati wapinzani waliposusa Bunge katika Serikali ya Awamu ya Nne.

Hizo zilikuwa alama kuwa Watanzania kwa wingi wao walikuwa wanamtazama Dk Magufuli kwa jicho la matumaini kuliko upande mwingine. Watanzania waliamini kuwa kumpinga Magufuli ni kupinga matumaini yao.

 

Ubinadamu wa Dk Magufuli

Januari, picha kuwa Dk Magufuli ni binadamu kama wengine ilianza kuonekana. Mkutano wa Pili wa Bunge la 11, Janauari mwaka huu uliibua hoja mbili zilizowapa uhai wapinzani dhidi ya Serikali.

Hoja ya kwanza ilihusu matangazo ya moja kwa moja ya shughuli za Bunge, Serikali haikutaka zionekane moja kwa moja, hii wapinzani waliibeba vizuri na iliwapa uhai wa kusikika tofauti na miezi miwili kabla yake.

Matangazo ya Bunge moja kwa moja ni mahitaji ya Watanzania, maana yamewarahishia kufahamu mengi kupitia malumbano bungeni. Kunyimwa matangazo hayo ni kuwarudisha gizani. Hapa ndipo Watanzania walianza kunung’unika kwa sauti dhidi ya Dk Magufuli.

Hoja ya pili ni katika mkutano huo wa Bunge wa Januari, badala ya kuwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, Serikali ya Dk Magufuli ikawasilisha Mwelekeo wa Mpango wa Maendeleo.

Zitto na Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu walishirikiana vizuri kuibana Serikali. Kilikuwa kipindi kigumu kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango ukizingatia ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kuwa ndani ya Bunge.

Hayo yalianza kuonyesha kuwa Dk Magufuli si malaika bali ni binadamu, kwa hiyo anaweza kutenda makosa na kukosolewa kama wengine. Kuanzia Januari, imekuwa rahisi kumkosoa Rais Magufuli na kueleweka tofauti na ilivyokuwa Novemba 5 hadi Desemba 31, mwaka jana.

Uamuzi wake wa kuzuia shughuli za kisiasa mpaka mwaka 2020, maneno yake makali kwa wafanyabiashara kuwa yeye si Rais wa matajiri, yalizidi kumpambanua kuwa ni binadamu na si malaika, kwamba anaweza kuteleza kwa ulimi au kifikra. Hakuna binadamu mkamilifu.

Julai, siku alipokabidhiwa uenyekiti wa CCM, Dk Magufuli alimwambia mtangulizi wake, Jakaya Kikwete kuwa ni mvulimivu kwamba ingekuwa yeye watu wanaoonyesha uasi kwenye chama kama walivyomfanyia JK mwaka jana kwenye mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM, nusu nzima ingepotea.

Maneno hayo pamoja na matamshi mengine mengi yaliyoibua utata ni kielelezo cha ubinadamu wa Dk Magufuli katika miezi 10 ya mwaka wake wa kwanza.

 

Mwandishi wa makala haya ni mwandishi wa habari, mchambuzi wa siasa, jamii na sanaa. Ni mmiliki wa tovuti ya Maandishi Genius inayopatikana kwa anuani ya mtandao www.luqmanmaloto.com

-->