Rais Magufuli vita unayopigana ni kubwa, maombi pekee hayatoshi

Muktasari:

  • Umaarufu wa Rais Magufuli unaongezeka kwa kasi sana hasa nje ya mipaka ya Tanzania na majarida mbalimbali duniani yamekuwa yakimtaja kama mmoja wa viongozi maarufu kwa sasa barani Afrika.

Mwaka mmoja wa kuwa madarakani, Rais John Magufuli amejijegea heshima kubwa ndani na nje ya nchi kutokana na maamuzi magumu ambayo amekuwa akifanya.

Umaarufu wa Rais Magufuli unaongezeka kwa kasi sana hasa nje ya mipaka ya Tanzania na majarida mbalimbali duniani yamekuwa yakimtaja kama mmoja wa viongozi maarufu kwa sasa barani Afrika.

Hakika hizi sifa, anastahili kwani hata huku nyumbani, jina lake kwa sasa linaongozwa kwa kutajwa kila kona kwa sababu tofauti.

Rais Magufuli alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), huko alieleza changamoto nyingi zilizopo serikalini.

Hata hivyo, akasema anapochukuwa hatua ya kutumbua wanaobainika kwenda nje ya mstari, wananchi wanapaswa kumuunga mkono na hapo ndipo nakumbuka pia kauli zake za mara kwa mara za kuwaomba Watazania kumuombea.

Rais Magufuli anasema walipoingia madarakani, waliahidi kutoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari na zikawa zinatengwa Sh18.777 bilioni kila mwezi kugharamia elimu bure.

Hata hivyo, alisema baada ya elimu bure wakajitokeza wanafunzi hewa, walimu wanaorodhesha wanafunzi ambao hawapo na hadi sasa kuanzia darasa la kwanza hadi sekondari, wanafunzi hewa zaidi ya 65,000 wamepatikana.

Anasema katika elimu ya juu, mikopo ambayo ilikuwa inatolewa ilikuwa ni kiasi cha Sh340 bilioni, lakini imeongezea hadi kufikia Sh473 bilioni hivyo wanufaika wameongezeka kutoka 98,000 hadi kufikia 124, 349.

Hata hivyo, anasema nia ya Serikali kuwapa mikopo watoto wa familia maskini inahujumiwa kwani imebainika mikopo hewa zaidi ya Sh3.5 bilioni.

Anasema mwanafunzi anasajiliwa, lakini hasomi chuo, fedha zinachukuliwa hali ambayo inasababisha kukosekana fedha za kukopesha watoto wengine maskini.

Anasema katika elimu ya juu hadi sasa mikopo ambayo haijalipwa zaidi ya Sh3 trilioni, hii ni changamoto ndani ya Serikali.

Rais anasema katika uhakiki wa wafanyakazi unaoendelea hadi sasa wamebainika watumishi hewa 17,500 ambao walikuwa wanalipwa mishahara hewa, likizo hewa.

Anasema wakati wanahangaika na watumishi hewa, mikopo hewa na wanafunzi hewa imebainika pia kuna Kaya maskini hewa zinazolipwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) 42,000.

Alisema Serikali ilikopa fedha ili kuweza kusaidia kaya maskini, nchini lakini badala yake, zinatumiwa na wengine jambo ambalo halitakubalika.

Rais pia anasema kumekuwepo na matukio ya baadhi ya watendaji wakuu wa mashirika ya umma wanapopewa fedha za maendeleo, wanazichukua na kuweka kwenye akaunti maalumu za benki binafsi.

Anasema watendaji wa mashirika haya wamekuwa wakijipatia riba kati ya asilimia nne hadi nane katika fedha hizo, lakini Serikali kupitia Benki Kuu Tanzania (BoT) inakwenda kuzikopa tena hizo fedha kwa riba ya asilimia hadi 15 wakati ni fedha zake.

Rais anasema huu ndiyo umekuwa mchezo na karibuni amekuta Sh26 bilioni zilizokuwa zimetolewa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa matumizi yao, zikapelekwa benki tatu na bodi ikapitisha na sasa kaiondoa bodi na fedha zimechukuliwa na Serikali.

Alikwenda mbali zaidi na kueleza kuwa hadi sasa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ambayo ilianzishwa kwa mahitaji maalumu kusaidia elimu, kuna zaidi ya Sh30 bilioni zimewekwa kwenye akaunti hiyo (Fixed Term Savings Account) na akamtaka waziri wa Elimu kuchukua hatua.

Mifano hii, michache tu aliyoitoa Rais inaonyesha ni jinsi gani vita ambayo anapigana ilivyo kubwa na kuwamaliza maadui ilivyo vigumu kwani wengine ni wasaidizi wake.

Naamini kwa mfumo uliopo sasa, Rais wetu na watendaji wachache serikalini wanapigana vita kubwa sana kwani maadui wengi wapo ndani yao na wengine wamewateua wao.

Ingawa naamini Rais anajua ukubwa wa vita hii, ndiyo sababu amekuwa akiomba Watanzania kumuombea kwa Mungu apigane salama kwani nia yake hakika ni njema.

Naamini Watanzania wengi wanamuombea, lakini nadhani maombi pekee hayatoshi kwa kuwa ndani ya wapiganaji kuna wasaliti wengi.

Mfano Katiba ya wananchi, ilipendekeza nafasi za juu katika vyombo mbalimbali kama mashirika ya umma, bodi na wakuu wa taasisi za umma, wanaozitaka waziombe na kufanyiwa usaili na wataalam husika, badala ya kuteuliwa kama ilivyo sasa.

Mussa Juma ni mwandishi na mchambuzi wa gazeti hili. 0754296503/0715296503. Baruapepe: [email protected]