UCHAMBUZI: Rais watumishi wa Serikali wamo katika hali tete

Novemba Mosi, nilifurahi kukuona mbashara Rais wangu ukiwa ndani ya Ukumbi wa Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Ulikuwa nawe ni mmoja wa washiriki katika kongamano lile kuhusu uchumi na siasa.

Naomba kukumbusha jambo Rais wangu. Siku ile ulipopata asilimia 87 ya kura za wajumbe wengi wa CCM kuwa mgombea wa urais, nilipata matumaini mapya kuwa hatimaye tumempata Rais mpambanaji na mwenye uchungu na nchi.

Naomba nikuhakikishie kuwa wananchi wengi tunaridhika na mapenzi yako makubwa kwa Watanzania. Jitihada zako zinaonekana.

Hata hivyo, wahenga wanasema, “Kilio huanza na mfiwa.’’ Siku ile kama ningepata nafasi kuna jambo moja nilitamani nikueleze kwa niaba ya Watanzania wanaokutakia mafanikio katika vita dhidi ya rushwa na umaskini.

Naomba nitumie lugha ya picha kujaribu kujenga hoja yangu.

Katika kijiji fulani, kulitokea baba mmoja aliyekuwa amesafiri kwenda nchi ya mbali alichelewa kurejea nyumbani. Aliporejea nyumbani akagundua kuwa wanakijiji wenzake wameshalima na kupanda mashamba yao. Akaingiwa na hofu kuwa watoto wake watakufa njaa asipochukua hatua kwa haraka.

Akaamua kuwafunga punda wake wawili siku iliyofuata na kuwaweka shambani, ili walime shamba lake kwa kutumia jembe la kukokotwa na wanyama.

Alilenga kuwa kesho yake punda wale watumike pia kupanda. Kazi iliyotakiwa kufanyika kwa wiki mbili, yeye alitaka ifanyike kwa siku mbili.

Aliwatumikisha wale punda kwa siku nzima lakini waliweza kulima ekari 10 tu kati ya 50 alizokusudia.. Baadaye akaamua kuwalaza punda wale shambani waendelee kulima lakini waliishia kugoma na kulala chini. Hata alipowapiga fimbo nyingi mgongoni punda wale hawakuamka. Waliishia kugoma.

Siyo kwamba punda hawakujua kufanya kazi, la hasha ila lilikuwa tatizo la mkulima ambaye hakujua kuwa uwezo wa punda haukuwa kulima lile shamba kwa siku moja.

Pia alipaswa kujua kuwa si matakwa yake peke yake ndio ya msingi, bali alipaswa kuwajali punda wake wanaomfanyia kazi.

Yeye hakuwapumzisha wala kuwapa chakula ili wawe na nguvu za kufanya kazi. Alichopaswa kufanya ni kutafuta msaada wa punda wengine wamlimie mashamba mengine na hivyo siku zingepungua na si kuwatesa waliopo.

Mheshimiwa Rais, naelewa kuwa unapenda kuona nchi hii inapata maendeleo na kuwa na uchumi wa kati.

Watumishi wa umma ndio watu wako wa kukusaidia ufikie malengo hayo.

Hawa wapo na bahati mbaya wana maumivu mengi kuliko inavyoweza kufikiriwa. Nimeamua kukudokeza hivi kwa nia njema kabisa kwa sababu mimi ni mtu ninayekutakia mafanikio.

Watumishi wako, yaani watumishi serikalini wana njaa na wala hawana motisha ya kufanya kazi. Wengi tangu mwaka 2015 hawajaonja mishahara mipya.

Wengine wana madai yaliyorundikana kiasi cha kukatisha tamaa wakiwa wanaishi kwa matumaini ya kuwa labda ipo siku moja watalipwa.

Tufanyeje? Tukifanya mambo kadhaa tutaweza kuimarisha utendaji wa watumishi wa umma nchini.

Kwanza ni kuboresha huduma za afya na elimu nchini. Elimu ikiwa bora na huduma za afya zikiimarika naamini watumishi wengi wataridhika na mishahara yao na kutokuwa na wasiwasi kuhusu elimu ya watoto wao na watakuwa hawana hofu ya afya za familia zao.

Pata picha kidogo; muuguzi ambaye ambaye maisha yake magumu huko Ludewa, Namtumbo, Ngara, Ikungi, Kasulu na kwingine anampeleka mtoto wake kwa mwalimu ambaye naye ana hali ngumu.

Hasira za mwalimu anazihamishia kwa mtoto wa muuguzi. Muuguzi naye hasira zake anazihamishia kwa mtoto wa mwalimu.

Pia, wafanyakazi wa Serikali wanahitaji mafunzo ya mara kwa mara ili waweze kuboresha utumishi wao serikalini.

Bahati nzuri wewe unaelewa kuwa mgomba haushindwi na mkunguwe. Mimi ni mfiwa ninayeanza kulia.

Sisi ni kama punda wako shambani, huwezi kufikia malengo yako ya kuitengeneza Tanzania kama hutajali masilahi ya watumishi wako ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakiishi kwa matumaini.

Faraja Kristosmus ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. 0787-525396