MAONI: Sababu za kuadimika saruji zifanyiwe kazi

Muktasari:

  • Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kutokuwepo kwa saruji ya kutosha katika maduka ya vifaa vya ujenzi kwenye maeneo ya Mwenge, Tegeta na Buguruni.

Katika ya gazeti hili toleo la jana kulikuwa na habari iliyohusu uhaba mkubwa wa saruji jijini Dar es Salaam ambao umesababisha bidhaa hiyo kupanda bei kutoka Sh13,500 hadi Sh18,000 kwa mfuko wa kilo 50 katika baadhi ya maeneo.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kutokuwepo kwa saruji ya kutosha katika maduka ya vifaa vya ujenzi kwenye maeneo ya Mwenge, Tegeta na Buguruni.

Kimsingi, bidhaa yoyote ya viwandani inapoadimika jijini Dar es Salaam, maeneo mengine ya nchi yanakuwa katika hali mbaya zaidi. Kwa maana nyingine ni kuwa saruji katika sehemu zingine mikoani itakuwa inapatikana kwa bei kubwa zaidi.

Bei inakuwa kubwa zaidi mikoani kwa sababu Dar es Salaam ndiyo mji pekee mkubwa wa kibiashara hapa nchini, ambao kila muuzaji na mnunuzi hukumbilia kutoa/kupata bidhaa au huduma auzayo au aitakayo.

Baadhi ya wamiliki wa maduka ya saruji jijini humo wanasema kwa zaidi ya wiki nne hawajapata bidhaa hiyo kutoka kwa wazalishaji, licha ya kuagiza mara kadhaa, jambo ambalo limesababisha ipande ghafla kutokana na kupungua kwake sokoni.

Hata hivyo, kwa wale waliozungumza na gazeti hili wanasema hawajui sababu na hata zile wanazozisikia juujuu hazijakata kiu yao ya kujua kwa undani kulikoni bidhaa hiyo muhimu na nyeti katika ujenzi iadimike, ilhali kuna viwanda vingi vinavyoizalisha hapa nchini.

Yote kwa yote ni kuwa, mwananchi ndiye anayeumia kwa sababu hapati saruji kwa bei anayoimudu na pia kwa wakati kutokana na uhaba uliopo.

Ingawa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amewataka wananchi kuwa watulivu kwa sababu wazalishaji walipunguza uzalishaji kwa ajili ya kufanyia matengenezo mitambo yao. Hata hivyo, majibu hayo hayatoshi kukata kiu ya wanaotaka saruji kwa ajili ya shughuli zao.

Mwijage anasema wazalishaji hivi sasa wameanza kuzalisha, hivyo tatizo lililopo litaondoka hivi karibuni. Lakini tunajiuliza, kwa nini bidhaa hii iadimike nchini wakati tunavyo viwanda vikubwa vinne na vidogo zaidi ya vitano?

Tunasema hivyo kwa sababu suala la ujenzi ni endelevu na linawahitaji wadau kama wazalishaji wa saruji ili kusukuma mbele maendeleo yanayotarajiwa.

Tunajiuliza, kwa zaidi ya mwezi mmoja wa uhaba wa saruji ni miradi au shughuli ngapi za wananchi zimeathirika kwa kukosa huduma? Hakika ni nyingi.

Ni vyema wazalishaji wa saruji wakaazimia kutosababisha tena uhaba wa bidhaa hii kwa sababu wanakwaza maendeleo ya wananchi na Taifa zima.

Kutozalisha saruji kwa kiwango kinachotakiwa na soko (la ndani tani 13,000 kwa siku), kumeathiri mambo mengi katika sekta ya maendeleo kijamii na kiuchumi.

Mbali ya wao kuazimia, tunaitaka Serikali iangalie namna bora ya kuhakikisha bidhaa hii haiadimiki tena, kwa kuhakikisha kwamba wazalishaji hawawi na ratiba ya pamoja ya matengenezo ya viwanda vyao na kusababisha uhaba kama huu.

Pamoja na hayo, tunadhani kwamba ipo haja kwa Serikali kufanya uchambuzi wa kina katika sekta hiyo na ikibidi, kutokana na unyeti wake kwa jamii na taifa kwa ujumla, iangalie namna bora ya kudhibiti bei na upatikanaji wake kwani kuachwa hivihivi, kunaweza kusababisha matatizo makubwa kama hayo yaliyojitokeza.