KUTOKA BASATA : Sanaa zetu na fursa za masoko ndani na nje ya nchi

Muktasari:

  • Pamoja na haya tunahitaji kubadili dhana iliyojengeka miongoni mwetu kuwa sanaa ni kimbilio la wasiojiweza kiuchumi bali ni kazi inayohitaji ubunifu, akili, maarifa na ni muhimu katika kuinua pato la mtu husika na taifa kwa ujumla kwani inatoa fursa mbalimbali kama ajira, kuanzishwa kwa viwanda vidogo, kuendeleza na kukuza utamaduni wa Kitanzania na kuendeleza biashara ya ndani na nje ya nchi na kukuza pato la taifa kwa ujumla.

Sanaa imekuwa ikichukuliwa kama kimbilio kwa wasiojiweza hasa wanawake kama njia ya kujikwamua kiuchumi na kuendeleza utamaduni.

Pamoja na haya tunahitaji kubadili dhana iliyojengeka miongoni mwetu kuwa sanaa ni kimbilio la wasiojiweza kiuchumi bali ni kazi inayohitaji ubunifu, akili, maarifa na ni muhimu katika kuinua pato la mtu husika na taifa kwa ujumla kwani inatoa fursa mbalimbali kama ajira, kuanzishwa kwa viwanda vidogo, kuendeleza na kukuza utamaduni wa Kitanzania na kuendeleza biashara ya ndani na nje ya nchi na kukuza pato la taifa kwa ujumla.

Hali ya uzalishaji wa kazi za sanaa kama vile filamu, muziki, uchongaji na ususi imekuwa ikiongezeka, ingawa bado kuna changamoto zinazoikabili tasnia hii ya sanaa. Ni muhimu kutambua kuwa changamoto hizi zinaweza kubadilishwa kuwa fursa kwa wasanii na wadau wa sanaa. Pamoja na umuhimu mkubwa uliopo wa kazi za sanaa, bado soko la ndani la bidhaa za sanaa za Kitanzania ni dogo kiasi cha kutokuwa na tija ya kuongeza kipato na maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Kufanya utafiti wa masoko ili kubaini nini kinahitajika katika soko ili kuzalisha bidhaa inayoendana na mahitaji ya watumiaji pamoja na bei hizo kutokana na aina ya walaji unaowahudumia ni muhimu kwa kuwa walaji hutofautiana mambo mbalimbali kama vile mahitaji na kipato na hivyo bidhaa ni tofauti pia.

Ubunifu katika uzalishaji bidhaa lazima uongezeke na si kuendelea kuzalisha kwa kuiga. Ubunifu unasaidia kutofautisha mzalishaji mmoja na mwingine na hivyo kufanya mzalishaji kuwa wa kipekee katika soko na kuwafanya watumiaji kuwa tayari kupokea bidhaa za kipekee, kutoka kwa mzalishaji hivyo kumsaidia kuwa mshindani sokoni.

Wasanii na wajasiriamali wanatakiwa kujifunza matumizi ya teknolojia ya kompyuta na kutumia katika shughuli za kibiashara. Matumizi ya vifaa vya mawasiliano yatasaidia kupata taarifa mbalimbali za masoko, kubadilishana na kupeana taarifa mbalimbali pamoja na kujifunza kupitia mtandao (internet) kutoka kwa watu na nchi tofauti. Hivyo itasaidia kukua kwa biashara na kufahamu mbinu za ushindani katika soko la kimataifa.

Pia ni muhimu kuwa na taasisi za fedha zinazotoa mikopo ya masharti nafuu na hata riba nafuu, na ambayo haina mlolongo mrefu katika kutoa mkopo ili kumrahisishia mzalishaji kufanya kazi kwa haraka kutokana na muda na soko kwa ujumla kwa kuwa mahitaji ya soko yanabadilika mara kwa mara na kwa haraka. Pia hii itasaidia kuzalisha kwa wingi na kutumia vifaa bora vya uzalishaji.

Kuhamasisha soko la ndani ili liwe endelevu kwa kuhamasisha Watanzania kuwa wazalendo na kununua bidhaa za Tanzania, kutasaidia kuinua soko la ndani litakalomsaidia mzalishaji wa kazi za sanaa kupata kipato cha kutosha kitakachomuwezesha kuzalisha kazi nyingi na zenye ubora. Pia kutamsaidia kuwa na uwezo wa kuuza hata katika soko la nje na kuifanya Tanzania itambulike kwa kuzalisha bidhaa bora kimataifa.

Katika zama hizi za utandawazi, dunia imekuwa kama kijiji hivyo bidhaa nyingi zinatoka sehemu moja kwenda nyingine kwa wingi na kwa urahisi hali inayosababisha ushindani mkubwa katika soko, ushindani unaohitaji ubunifu na mbinu.

Tanzania ina fursa kubwa katika soko la nje kwa kuwa bidhaa zinazopelekwa katika masoko ya nje kupitia maonyesho zimeonekana kupendwa na watumiaji kwa kuwa zimenunuliwa kwa wingi, kuuliziwa na baadhi ya waliopeleka wamepokea oda na baadhi kuingia mikataba ya kufanya na wafanyabiashara kutoka nje ya mipaka ya Tanzania.

Ikumbukwe Watanzania tumekuwa tukishiriki maonyesho mbalimbali ya nje, kama ya China, Zimbabwe, Malawi (Solo exhibition), Madagascar (Expo Madagascar) na Rwanda.

Watanzania pia wamekuwa wakishiriki matamasha mbalimbali, kama la Jumuiya ya Afrika Mashariki (Jamafest) lililofanyika kwa mara ya kwanza Rwanda mwaka 2013, na mwaka 2015 lilifanyika Nairobi –Kenya. Mwaka huu litafanyika Uganda.

Kutokana na mifano ya fani mbalimbali zilizomo katika sanaa, tunakubaliana na usemi kuwa ni tasnia yenye uwezo wa kuleta ajira na kipato kwa mtu binafsi, jamii na taifa kwa ujumla.

Sanaa ni biashara na ni nyenzo muhimu kwa maendeleo endelevu katika nchi na inaweza kuhamasisha jamii yetu kuondokana na umaskini kupitia anuai za shughuli kama utamaduni wa kitalii, ununuzi na biashara mbalimbali za sanaa na malipo ya kodi. Wasanii na wadau wengi wa sanaa kwa juhudi zao wamejijengea umaarufu na kujipatia kipato kikubwa katika fani zao kwa kutumia vema fursa ya soko la ndani na nje ya nchi. Baadhi ya mifano hai ni Nasib Juma (Diamond Platinun), Steven Jacob (JB), Oregenesi Uiso (Mkurugenzi Karibu Art gallery), Afrika Sana, Mustafa Hassanali na wengine.

Mwisho tunaamini kuwa ili kuendeleza na kukuza sanaa za Kitanzania ni lazima kuwe na juhudi za ziada za kufanya bidhaa hizo zikubalike kwanza na watumiaji wa soko la ndani kuanzia ofisi za Serikali, taasisi mbalimbali, watu binafsi na jamii kwa ujumla watumie bidhaa hizo.

Ni wakati wa kuwahamasisha Watanzania kuwa wazalendo, kujali bidhaa zinazozalishwa Tanzania ili kujenga na kuinua pato la mzalishaji na taifa kwa ujumla na hivyo kumsaidia mzalishaji kuwa na uwezo wa kuzalisha zaidi na kwa wingi bidhaa zenye ubora ili kuweza kukabiliana na ushindani katika soko la Kitaifa na baadaye Kimataifa.