Septemba Mosi, macho yote Tanzania?

Muktasari:

  • Swai anaeleza si binadamu tu walioshtushwa na hali ile. Wanyama na ndege waliona hali ya utofauti kwani kuku walikimbilia mabandani, ndege waliokuwa katika safari zao wakaanza kurudi kwenye miti yao na ng’ombe walikimbia huku na kule.

Siku moja nilikuwa sokoni Kwasadala tunauza ndizi mbivu. Mara taratibu tukaanza kuona nuru inafifia. Mara giza linaanza kuingia.

“Tuliacha vitu vyetu sokoni na kukimbia. Watu walipiga mayowe walijua ni kiama. Dunia imekwisha,” Apaurulaly Mwanga, mkazi wa Roo, Hai mkoani Kilimanjaro anaelezea alichokishuhudia siku jua lilipopatwa ‘kamili’ Februari 16, 1980.

Godbless Swai ambaye kwa sasa ni mhasibu kampuni moja iliyopo jijini Dar es Salaam anaeleza kuwa tukio la kupatwa kwa jua liliibua taharuki kubwa kwa wakazi wengi wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Mwaka 1980 akiwa kidato cha pili shule ya sekondari ya wavulana ya Umbwe, tayari walikuwa wameshafundishwa mada ya kupatwa kwa jua na mwezi.

“Sikuwa na wasiwasi kwa kuwa walimu walikuwa wameshatueleza nini kitatokea siku hiyo. Kwa wale ambao hawakuwa na taarifa waliogopa. Walikimbia huku na kule wakijua ndiyo mwisho wa dunia,” mhasibu huyo anaeleza.

Swai anaeleza si binadamu tu walioshtushwa na hali ile. Wanyama na ndege waliona hali ya utofauti kwani kuku walikimbilia mabandani, ndege waliokuwa katika safari zao wakaanza kurudi kwenye miti yao na ng’ombe walikimbia huku na kule.

“Hali ile ilidumu kwa muda wa saa nne. Hatimaye hali ilianza kupambazuka taratibu na ikarudi kama kawaida,” Swai anaeleza.

Wakazi wa Kilimanjaro wakikumbushia hali ilivyokuwa Februari 18, 1980, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache ambazo zitashuhudia hali ya kupatwa kwa jua mwaka huu.

Ni miaka 36 imepita tangu lilipotokea tukio hilo hapa nchini na kuibua hisia tofauti huku wengi wakidhani kuwa ni mwisho wa dunia.

Linaelezwa kuwa ni tukio la kihistoria kwani si aghalabu kutokea. Mtoto aliyezaliwa 1980 au baadaye ameendelea kusimuliwa nini kilichotokea na tukio kama hilo linatarajiwa kutokea tena Septemba Mosi mwaka huu.

Tanzania ni moja ya nchi chache duniani ambazo jua litaonekana likipatwa kuanzia saa nne asubuhi hadi saa nane mchana.

Mtaalamu wa Idara ya Sayansi na Mazingira wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) Dar es Salaam, Dk Noorali Jiwaji anasema tukio hili ambalo limeshavuta hisia za wadau wa utalii kutoka sehemu kadhaa duniani litaanza kuonekana saa 4:17 asubuhi hadi saa 7:55 mchana.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, japokuwa maeneo yote ya Tanzania yatashuhudia utofauti mfano jua kufifia, lakini maeneo ya kusini mwa nchi hususan Mbeya na mikoa ya jirani ikiwamo Katavi, Rukwa,  Njombe, Ruvuma na Mtwara itashuhudia giza kwa takriban saa nne.

Kwa mantiki hiyo, wataalamu wa OUT wakiongozwa na Dk Jiwaji wamechagua mji wa Rujewa, uliopo Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya kuwa sehemu ya kuratibu tukio hilo la kihistoria.

Sababu za kuchagua eneo hilo ni kwamba hakuna wasiwasi wa kuathiriwa na hali ya hewa kama vile uwepo wa mawingu. “Uwezekano wa kuwapo mawingu katika eneo hilo ni asilimia 20 tu hivyo hakuna wasiwasi kuwa tutashindwa kushuhudia tukio hilo,” Dk Jiwaji anafafanua.

Watu watakaokuwa katika maeneo hayo na maeneo ya karibu kwa umbali usiozidi kilomita 100 wakitazama angani kwa kutumia miwani maalumu wataona mwezi umelifunika jua na kuacha umbo la pete. Inamaanisha kuwa tofauti na ilivyokuwa 1980 ambapo jua lilipatwa ‘kikamilifu’, Septemba Mosi, mwaka huu halitafunikwa lote.

Hivyo, umbo la pete linaloachwa na mwezi kwenye jua litaunda mfano wa pete, hali iliyowashawishi wataalamu kuiita aina hii ya kupatwa kuwa ni “kupatwa kipete.” Lakini hii itaonekana vema ikiwa chujio maalumu la kukinga macho dhidi ya miale ya jua wakati huo litatumika.

Barani Afrika, hali hiyo itaanzia Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo, kuja Tanzania na kuelekea Madagascar na jua litakuwa limejificha nyuma ya mwezi kwa asilimia zaidi ya 90.

Wakati gani jua linapatwa?

Kwa mujibu wa Wikipedia, kupatwa kwa jua kunatokea wakati dunia, mwezi na jua vinapokaa kwenye mstari mmoja mnyoofu. Wakati huo, mwezi hupita katikati ya dunia na jua. Katika hali hiyo, kivuli cha mwezi hutupwa kwenye uso wa dunia. Kivuli hiki hakifuniki dunia yote. Kwa hiyo kupatwa kwa jua kunaonekana kwa watu wengi kama kupungua kwa mwanga na sehemu nyingine watu hushuhudia giza.

Dk Jiwaji anataja aina za kupatwa kwa jua kuwa ni ‘kupatwa Kamilifu’ hutokea wakati mwezi unapofunika jua kabisa. Japo ni kwa muda mfupi, jua huwa halionekani kabisa. Aina ya pili ni ‘kupatwa Kipete’ na mwezi huacha sehemu nyembamba ya jua. Ile sehemu inayoachwa huwa na umbo mithili ya pete, hali iliyoshawishi wataalamu wa astronomia kuiita hali hiyo kuwa ni kupatwa kipete. Katika aina hii jua hufunikwa kwa zaidi ya asilimia 90.

Aina hii ndiyo itakayojidhihirisha Septemba Mosi katika ukanda wa kusini, hususan Rujewa wilayani Mbarali, Mbeya.

‘Kupatwa Hilal,’ mwezi hufunika sehemu ndogo ya jua na kutengeneza umbo la mwezi mchanga au mwezi mwandamo.

Historia ya Tanzania

Tukio la kupatwa kwa mwezi ni la mara kwa mara lakini kupatwa kwa jua limekuwa ni la historia ya kipekee. tofauti ya mambo haya mawili, kwa mujibu wa Dk  Jiwaji ni kwamba mwezi unapopatwa kivuli cha dunia huwa kimeufunika mwezi. Katika tukio hilo, kivuli cha dunia huonekana ni kikubwa, hivyo hushuhudiwa sehemu kubwa ya Dunia.

 Mtaalamu huyo anabainisha kuwa jua linapopatwa, kivuli cha mwezi huangukia duniani kinakuwa kidogo kwa hiyo ni watu wachache tu wataona jua likipatwa. Kwa mantiki hiyo, Tanzania imekuwa na bahati ya kipekee kuwa miongoni mwa nchi au maeneo machache duniani na tukio hilo litashuhudiwa, ikiwa ni miaka 36 imepita tangu hali hiyo kutokea hapa nchini.

 Historia ya hivi karibuni inasema tukio la kupatwa kwa jua liliwahi kutokea Tanzania Julai 31, 1962. Likatokea tena Aprili 18,   1977. Aina iliyotokea katika vipindi hivyo vyote viwili ni kupatwa kipete na mwezi haukulifunika jua lote.

Hivyo itakapotokea Septemba Mosi mwaka huu itakuwa imepita miaka 39 tokea tukio la mwisho.Wanasayansi wa mambo ya anga wanasema kuwa aina hii ya jua kupatwa kipete itatokea tena miaka 15 ijayo.

Kutokea baada ya miaka 48

“Tukio hili litatokea tena Tanzania mnamo Mei 21, mwaka 2031 na Februari 17, 2064 ikiwa ni baada ya kupita miaka 48. Kwa hiyo ni kitu kinachotokea kwa nadra sana na ndiyo maana ni cha kipekee kwa wananchi na vijana wa Tanzania,” anasema Dk Jiwaji.

Tukio lililovuma zaidi la kupatwa kwa jua ni lile lilitokea Februari 16, 1980. Hapa mwezi ulilisogelea jua kwa zaidi ya asilimia 90 hivyo maeneo mengi yalishuhudia kupatwa kwa jua hususan kwa wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro. Aina hii wataalam wanaeleza kuwa huko ni kupatwa kwa jua kamilifu.

Historia inaonyesha pia kuwa kwa miaka ya hivi karibuni, jua lilipatwa zaidi nchi za jirani; Kongo, Uganda, Kenya, Somalia mnamo Novemba 3, 2013 na siku hiyo Tanzania ilishuhudia hali hiyo kwa aina ya kihilali.Mwakani, jua litapatwa Februari 26, 2017 ambapo nchi za Angola, Zambia, Kongo.

Tukio lina maana gani?

“Tukio hili lina maana gani kwa Watanzania kwa ujumla? Kwanza kabisa matukio kama haya ya kupatwa kwa jua ni nadra sana kuonekana,” anaeleza Dk Jiwaji.

Kupatwa kipete kulitokea miaka 39 iliyopita, 1977 na jingine linatarajiwa kutokea miaka 15 ijayo (2031) jambo ambalo mtaalamu huyo anasisitiza kuwa Tanzania inapaswa kuitumia fursa hii kikamilifu.

Dk Jiwaji anayekiwakilisha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) katika uratibu wa tukio la kupatwa kwa jua katika kituo cha Rujewa anasema, tukio hili linawafundisha wanafunzi kwa vitendo sayansi ya astronomia na kuelewa namna jua na mwezi na dunia vinavyojipanga angani hadi kusababisha hali ya kupatwa kutokea.

Inatarajiwa kuwa wanafunzi wataelewa zaidi sayansi kivitendo kwani watakuwa wanashuhudia kwa macho yao wenyewe tofauti na sasa ambapo kupatwa kwa jua kunafundishwa kwa nadharia zaidi hususani kwa njia ya michoro.

“Watanzania wataona jinsi sayansi inavyoweza kueleza matukio ambayo kabla ya hapo walikuwa wanayaogopa kutokana na imani za kishirikina,” anasema Dk Jiwaji.

Mtafiti huyo wa mambo ya sayansi ya anga na mazingira anaendelea kubainisha kuwa kupitia tukio la Septemba Mosi, mwaka huu huko Rujewa, Mbeya, “wazazi wataelewa umuhimu wa kuelewa sayansi ya mazingira ya angani na kuwahamasisha watoto wao kufuatilia kusoma sayansi kwa bidii zaidi na kuwapa ushirikiano hata nyumbani.”

Hii ni fursa ambayo wanasayansi wanapata bahati ya kupata maabara ya nje kuweza kupima kiasi cha punguzo la mwanga na joto na athari zake katika anga za juu.

Manufaa kiuchumi

Uchumi nao hautabaki nyuma. Watalii wengi wanatarajiwa kushuhudia tukio hilo la kihistoria kwani kupitia sekta ya utalii, wageni kutoka nje ya Tanzania wanatarajiwa kuingia nchini kushuhudia kupatwa kwa jua.

Makampuni ya kitalii yameshaanza kuitangaza Tanzania kupitia tukio la kupatwa kwa jua litakalotokea Septemba Mosi, mwaka huu.

Ni fursa ya kipekee ya kuwaalika watalii kuvitembelea vivutio vilivyopo kusini kwa Tanzania, tofauti na sasa ambapo huishia kaskazini mwa nchi ama visiwani Zanzibar.

“Wazee watakumbuka mwaka 1980 Shirika la Utalii Tanzania (TTC) liliandaa mabasi maalum ya kuwapeleka wananchi Lembeni Tanga wakati jua lilipopatwa kamilifu Februari 16, 1980. Hivyo hivyo makapuni ya utalii yatoe nafasi kwa wananchi kwenda Rujewa kuangalia jua likipatwa kipete siku ya Septemba Mosi,”            anasema Dk Jiwaji.