MAONI: Serengeti Boys imefungua njia, wadau waiunge mkono

Muktasari:

  • Mchezo huo wa ufunguzi kwa Serengeti Boys ulichezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Jumamosi iliyopita.

Tanzania imeanza vyema mashindano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 (Cecafa 17) kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, baada ya kuilaza Burundi mabao 2-1.

Mchezo huo wa ufunguzi kwa Serengeti Boys ulichezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Jumamosi iliyopita.

Mabao yaliyofungwa na wachezaji Kelvin John na Agiri Ngoda yalitosha kuiweka Serengeti Boys katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kwenye mashindano hayo.

Pia ni mwanzo mzuri kwa Tanzania ambayo itakuwa mwenyeji wa mashindano ya kufuzu Fainali za Afrika kwa vijana (Afcon), zilizopangwa kufanyika nchini mwakani.

Mashindano ya Cecafa yanayoendelea yanatumika kama sehemu ya maandalizi ya Fainali za Afcon ambazo zitafanyika nchini kwa mara ya kwanza.

Shirikisho la Soka Afrika (Caf) liliipa Tanzania uenyeji wa fainali hizo ikiwa ni hatua muhimu katika kukuza soka la vijana na Serengeti Boys inashiriki moja kwa moja.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe ameunda kamati inayohusisha viongozi wa soka kwa ajili ya maandalizi ya fainali hizo.

Msingi wa kuundwa kamati hiyo ni kuhakikisha mashindano hayo yanachezwa kwa kiwango bora hatua ambayo itaipa sifa Tanzania kimataifa.

Ushindi wa Serengeti Boys dhidi ya Burundi umeonyesha vijana wetu wana uwezo wa kushindana na wamejiandaa kupeperusha vyema Bendera ya Tanzania katika mashindano ya kimataifa.

Pia, ushindi huo una maana kubwa, hivyo TFF na wadau wengine wa michezo wanatakiwa kuiunga mkono katika maandalizi ya Afcon.

Burundi sio timu ya kubeza katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuwa tumeshuhudia timu zao kuanzia ngazi ya klabu zikicheza kwa kiwango bora katika mashindano ya kimataifa.

Huu ni mwanzo mzuri kwa Serengeti Boys katika maandalizi ya fainali za Afcon na timu hiyo inapaswa kuungwa mkono na wadau mbalimbali ili kuwapa morali wachezaji kuongeza kasi ya ushindani.

Ni vyema mashindano yanayoendelea nchini yakutumika kuijenga timu imara ambayo itashindana kikamilifu mwakani kwa kuwa itacheza na timu zenye viwango bora Afrika.

Serengeti Boys ina mahitaji mengi katika maandalizi yake yanayoratibiwa na TFF ambayo ndiyo yenye dhamana ya kusimamia maandalizi ya timu hiyo kabla ya kuanza mashindano ya Afcon.

Tunaamini kwamba wachezaji wetu wakiandaliwa vyema kwa mafunzo na mbinu mbalimbali za ushindi, Serengeti Boys ina nafasi ya kufanya vyema katika mashindano ya Afcon.

Tumeshuhudia mara kwa mara wachezaji au makocha wa timu za Taifa kwa nyakati tofauti wakilalamikia maandalizi duni wanayopata baada ya timu kufanya vibaya kwenye mashindano husika.

Kwa kuwa mashindano ya Afcon yanabeba sura ya utaifa, ni vyema Serikali ikaweka mkono katika maandalizi ya Serengeti Boys.

Timu hiyo inatakiwa kuandaliwa sasa kupitia mashindano ya Cecafa ili kupata timu bora kwa kuwa vipaji tunavyo na hakuna sababu ya Tanzania kushindwa kufanya vyema katika mashindano ya Afcon.