UCHAMBUZI: Serengeti Boys wafanyiwe haya, watatutoa tu

Muktasari:

  • Hali hiyo ni tofauti kabisa na ufanisi wa timu ya wakubwa ya mpira wa miguu, Taifa Stars ambayo imeshindwa kufuzu kwenye fainali za CAF na Fainali za Kombe la Dunia za Fifa .

Tanzania katika kipindi cha miaka takribani mitano imeshuhudia timu zetu za Taifa za Vijana (Serengeti na Ngorongoro) zikifanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.

Hali hiyo ni tofauti kabisa na ufanisi wa timu ya wakubwa ya mpira wa miguu, Taifa Stars ambayo imeshindwa kufuzu kwenye fainali za CAF na Fainali za Kombe la Dunia za Fifa .

Kama hiyo haitoshi, hata katika mashindano ya Cecafa imeshindwa kufanya vizuri.

Ni matumaini ya Watanzania wengi kwamba wachezaji wanaounda timu hizi mbili watafuatiliwa na kutunzwa ili wawe na manufaa yanayotarajiwa na wadau.

Hili linatokana na ukweli kwamba TFF na wadau wengine wametumia gharama kubwa kuzifikisha timu hizo katika ufanisi tunaouona sasa.

Ili yasitokee yale ambayo yaliwatokea wachezaji wazuri na ambao pia waliofanya vizuri kama hawa katika miaka, ni vyema kukawa na mkakati maalum.

Kama TFF wataendelea na programu hizi za kuwa na timu za Taifa za vijana, nashauri yafuatayo yafanyike ili mipango yao iweze kuleta matunda chanya kwenye timu hizo za Taifa za vijana na ile ya wakubwa.

Wachezaji wasomeshwe

Naamini kwamba baadhi ya vijana hawa wanaweza wakawa aidha hawakupata nafasi ya elimu ya sekondari na kama wote wako sekondari, wasaidiwe gharama za kusoma.

Siku zote elimu humsaidia binadamu yeyote katika kila jambo analolifanya. Hivyo endapo vijana hao watasaidiwa kusoma, tutakuwa tumewajengea misingi bora ya maisha yao ya kimpira na nje ya mpira ikizingatiwa kwamba kijana anaweza akaumia au akistaafu kucheza elimu ile itamsaidia.

Mipango ya kuwa na timu ya Taifa ya umri wa miaka 23

Kwa kuwa umri wa hawa vijana unaendelea kuongezeka, ni dhahiri kwamba itafika wakati hawatakuwa wanastahili kubaki kwenye makundi hayo mawili.

Ili wasianze kuhangaika na kusababisha kupotea, ni vyema TFF iangalie utaratibu wa kuwa na timu ya Taifa ya umri huo ili kuwe na mwendelezo wa kuviendeleza vipaji vyao wakiwa katika mazingira sahihi.

Hili likifanyika wachezaji wengi watakuwa ndani ya uangalizi maalumu na wachache kati yao wataanza kujumuishwa kwenye timu ya Taifa ya wakubwa.

Wachezji wa timu zote za vijana kushiriki Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza

Ili kuipunguzia gharama TFF kulazimika kuziweka kambini timu hizi kwa kipindi kirefu kila yanapotokea mashindano, ni vyema TFF ikawa na mpango wa kuwashikiza wachezaji hao kwenye klabu mbalimbali kwa makubaliano maalumu.

Wengi wa wachezaji wa Ngorongoro wamesajiliwa na klabu mbalimbali za Ligi Kuu na Daraja la Kwanza, lakini bila shaka wamekwenda kwa utaratibu wao wenyewe.

Mazingira kama hayo kwa vijana ambao bado ni wadogo yanaweza yakasababisha kutofanya vizuri.

Utaratibu unaofaa ilitakiwa TFF iwe na mikutano na wachezaji hao miezi kadhaa kabla ya ligi hizo kubwa mbili hazijaanza ili kuwaweka sawa wachezaji.

Aidha katika vikao hivyo, wachezaji wataweza kueleza matarajio yao ya kujiunga na klabu mbali mbali.

TFF inaweza kutumia muda huo kuwashauri wapi panaweza kuwa ni mahali sahihi pa kwenda kwa kipindi husika.

Baada ya hapo TFF inaweza kuwa na kikao na kila klabu na wachezaji ambao wanataka kujisajili ili kukubaliana masuala ya msingi ambayo yataingizwa katika mikataba.

Mathalani, baadhi ya masharti hayo yanaweza kuwa: mchezaji kupewa nafasi ya kucheza kwa muda fulani ndani ya mchezo.

Ninaamini haya yakifanyika, jitihada za TFF zitazaa matunda na baada ya miaka michache ijayo, tutakuwa na timu ya Taifa ya wakubwa tishio.