Serengeti Boys watawanywe klabu za Ligi Kuu

Muktasari:

Ilifungwa bao 1-0 licha ya kutoka suluhu na Mali na baadaye kuichapa Angola mabao 2-1. Mechi zote zilikuwa za kifundi, japokuwa kasoro za umakini katika lango zilionekana.

        Timu ya soka ya Taifa kwa vijana chini ya miaka 17, ilirejea nchini Jumatano iliyopita baada ya kutolewa na Niger katika mechi ya kumalizia mkondo wa kwanza makundi wa michuano ya Afrika.

Ilifungwa bao 1-0 licha ya kutoka suluhu na Mali na baadaye kuichapa Angola mabao 2-1. Mechi zote zilikuwa za kifundi, japokuwa kasoro za umakini katika lango zilionekana.

Baada ya kuwasili au hata kabla ya kutolewa, ilielezwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuwa timu hiyo inabadilika na kuwa Ngorongoro Heroes kwa maana ya timu ya U-20.

Mpango wake ni kushiriki mashindano ya vijana. Vijana hao watagawanyika, wengine ambao umri wao utawaruhusu, watabakia U-17 wengine watakuwa U-19 itakayokuwa kwenye mashindano ambayo Tanzania itakuwa mwenyeji mwaka 2019.

Wachezaji wengine tumeambiwa wataandaliwa kwa ajili ya kuingia kwenye timu ya U-23 kwa ajili ya kuwania kushiriki Michezo ya Olimpiki 2020 itakayofanyika Tokyo, Japan.

Mpango wa awali ulikuwa, Gabon hadi Kombe la Dunia, lakini sasa haupo na kinachoangaliwa sasa ni maisha mengine kwa vijana hao.

Tunadhani, hakuna sababu ya kuwaweka vijana hao kusubiri mashindano mengine, tunalishauri Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuziomba klabu kubwa kuwasajili na kutumia wachezaji hao kwenye mashindano mbalimbali. Chama cha Soka China (CFA), kimeteua wachezaji wa U-17 na kimeagiza timu za Super League ya China kuchukua watatu watatu na kuhakikisha wanacheza ili kupata uzoefu. Hata kwa Serengeti Boys, itakuwa ni mtazamo mzuri kwa kuwa watajengeka kimashindano kuliko kuwaacha kusubiri mashindano.

Kuna baadhi ya wachezaji waliotoka Mtibwa Sugar na Azam, hawa hakuna tatizo, lakini wapo ambao hawamo katika timu kubwa, ni jukumu la TFF kwa kushirikiana na timu za Ligi Kuu kufanikisha hilo kwa masilahi mapana ya Taifa.

Tunasema hivyo tukiamini kwamba kushiriki kwao katika Ligi Kuu kutawaweka tayari kimashindano kuliko kuwaacha wasubiri mashindano mengine ambayo baada ya hayo ya Gabon, yatachukua muda mrefu.

Pamoja na hayo, rai yetu kwa vijana hao ni mbili; mosi, pamoja na msingi huo wa kucheza Ligi Kuu au hata Daraja la Kwanza, sasa wanatakiwa kuwa na mawazo ya kucheza nje ya Tanzania kwa ajili ya kukuza viwango vyao. Itakuwa sumu kwao kukaa na kuwaza kucheza Ligi Kuu na kuishia hapo. Si kwamba tunaipoinda, la hasha, lakini itapendeza wakisaidiwa mawakala au hata kwenda kukaa kwenye akademi za nje wakijifunza huku wakisubiri kuingia timu kubwa.

Jambo la pili ni kwa wachezaji wenyewe, wanatakiwa kujiheshimu na kujitambua. Wanapaswa wafahamu kwamba wao ni hazina ya baadaye kuliko kujiingiza kwenye starehe zitakazomaliza mpira wao ilhali bado wadogo.

Misingi ya soka waliyopewa, utaratibu wa kuishi kama wachezaji wa kulipwa uanze sasa. Hili la nidhamu ni la msingi sana, liko katika maeneo mengi ikiwamo maisha ya ndani na nje ya uwanja.

Mfano mzuri, wachezaji wanaweza kujipanga wenyewe kufanya mazoezi kulingana na mazingira waliyopo. Mathalani, wale wanaoishi Dar es Salaam, wanaweza kukutana Uwanja wa Karume hivyo ndivyo iliyo kwa mchezaji wa kulipwa. Anajipangia ratiba ya mazoezi na hasubiri kusukumwa.