Serikali isiwafumbie macho wakunga, wauguzi hawa

Muktasari:

  • Walalamikiwa wakubwa wa tatizo hilo ambalo limekuwa kilio cha muda mrefu kwa wagonjwa hasa wajawazito ni wauguzi na wakunga wanawake.

Tumefarijika kusikia Serikali ikikiri kuwapo kwa watumishi ambao wamekuwa na matatizo ya kunyanyasa wagonjwa wanaokwenda kujifungua.

Walalamikiwa wakubwa wa tatizo hilo ambalo limekuwa kilio cha muda mrefu kwa wagonjwa hasa wajawazito ni wauguzi na wakunga wanawake.

Juzi, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustin Ndugulile akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Emmanuel Mwakasuka alilieleza Bunge kwamba, “Ni kweli kuwa wapo wanawake watumishi ambao wamekuwa na manyanyaso kwa wanawake ambao wanakwenda kujifungua. Waziri wa Afya alishalitolea kauli jambo hilo, tunawafuatilia na tutashughulika nao.”

Mbunge huyo alitaka kujua kutoka kwa Serikali hatua ambazo inazichukua ikiwa inazo taarifa kuwa watumishi wanawake katika hospitali wamekuwa wakiwanyanyasa wanawake wenzao pindi wanapokwenda kujifungua.

Labda kwa kuwa swali hilo lilikuwa la nyongeza baada ya lile la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Hawa Mchafu aliyetaka kujua Serikali ilimaanisha nini kusema matibabu ni bure kwa wajawazito na waziri huyo kusema wajawazito ni moja ya makundi maalumu wanaostahili kupata huduma za matibabu kama ilivyo katika mwongozo wa uchangiaji wa mwaka 1997, uliopitiwa mwaka 2009/10 ambako imetamkwa kuwa huduma za afya kwa wajawazito ni bure.

Tunasema labda ni kwa kuwa lilikuwa swali la nyongeza kwa sababu kama Serikali inafahamu kuwapo kwa malalamiko hayo ambayo si ya mwaka jana wala juzi, ilipaswa walau kuja na majibu ya hatua kadhaa ambazo imekwisha chukua kukabiliana nalo.

Tulitarajia ikibainisha hatua ilizochukua katika kutoa elimu ya huduma kwa wateja kwa wakunga na wauguzi ili kuwajengea uwezo wa kuwajali wagonjwa wanaowahudumia, lakini pia hatua za kinidhamu ilizowachukulia wale ambao wameonekana kuendelea na tabia hiyo hata baada ya kuelimishwa na kuonywa. Tunaitaka Serikali kuandaa si majibu ya kina tu kuhusu tatizo hili, bali kuja na mkakati wenye nuru ambao kila jicho litauona kwamba umedhamiria kumaliza kabisa kero hii kwa mama zetu.

Tunasema hivyo kwa sababu kilio cha unyanyasaji wa wakunga na wauguzi achilia kwamba sio cha jana wala juzi, kinatoka karibu kila pembe ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hivi karibuni, mathalani, baadhi ya wadau wa afya mkoani Arusha walisema tatizo hilo ni kubwa maeneo ya pembezoni yakiwakumba zaidi wanawake wanaotoka katika jamii ya wafugaji.

Pia, mwishoni mwa mwaka jana, Naibu Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Harusi Said Suleiman akizungumza na wauguzi na wakunga wa jadi huko Mnazi Mmoja mjini Unguja, aliwataka kuacha kutumia lugha chafu akisema zinachangia baadhi ya wananchi wakiwemo kina mama kupoteza imani ya kwenda hospitali kutibiwa na wengine kujifungulia nyumbani.

Hatutaki kuona wananchi wanapoteza imani ya kupata tiba ya kisayansi kwani mbadala wake watakimbilia kwa wakunga wa jadi ambao aghalabu hawana vifaa vinavyoweza kuwahakikishia kina mama wanaojifungua usalama wao na watoto wanaozaliwa.

Lakini pia kupoteza huko kwa imani kunaweza kuwa sababu ya wagonjwa kukimbilia kwa waganga wa kienyeji, wengi wao wakiwa ni wapiga ramli chonganishi ambazo zimekuwa chanzo cha migogoro katika jamii. Tunaitaka Serikali isiwavumilie watumishi hawa wachache kwani wanaweza kuwaambukiza wengine na kusababisha tatizo hili kuwa kubwa na kusababisha madhara makubwa.