Tuesday, September 12, 2017

Serikali izifyeke NGO zisizo na tija

 

By Raymond Kaminyoge

Uhakiki haujawahi kuwaacha watu salama. ndivyo unavyoweza kusema baada ya Serikali kutangaza kuwa itafanya uhakiki wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO).

Tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, kumekuwa na uhakiki wa aina mbalimbali ambao umeshafanyika na unaoendelea kufanyika.

Uhakiki mkubwa uliofanyika ni wa vyeti vya kidato cha nne ambavyo hutolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta).

Madhara ya uhakiki huo tumeshuhudia watumishi wa umma zaidi ya 9,000 wakifukuzwa kazi baada ya kubainika kuwa walitumia vyeti bandia ili kupata ajira serikalini.

Uhakiki mwingine ni wa wafanyakazi walio kwenye utumishi wa umma ambao waliokuwa wakipata mishahara wakati hawakuwapo kazini.

Wizara ya Fedha ilikuwa ikilipa mishahara ya wafanyakazi hewa kila mwezi lakini fedha hizo zilichukuliwa na watumishi wenye tamaa.

Uhakiki mwingine ni wa kaya maskini ambazo zilikuwa zikipata ruzuku kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (Tasaf).

Uhakiki huo ulibaini kuwa watu 32,456 ambao hawakuwa na sifa, lakini walikuwa wakipata ruzuku hiyo.Watu hao waliondolewa katika mpango huo huku baadhi ya watumishi wa mfuko huo wakichukuliwa hatua za kisheria na kinidhamu.

Matukio hayo ni baadhi ya uhakiki ambao umefanyika katika utawala tunaoendelea nao. Rais John Magufuli amekuwa akilalamika kuwa aliikuta nchi ikiwa na mambo mengi ambayo ni hewa.

Hivi sasa kuna uhakiki wa mashirika yasiyo ya kiserikali ulioanza Agosti 21 na na kutarajiwa kumalizika Septemba 4, mwaka huu.

Kwa mujibu wa msajili wa mashirika hayo kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, uhakiki utafanyika kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya na Dodoma.

Wawakilishi wa NGO’s kutoka kwenye mikoa hiyo na iliyo karibu walitakiwa kufika kwenye mikoa hiyo kulingana na kanda wanazotoka.

Kwenye uhakiki huo, walitakiwa kwenda wakiwa na vyeti vya usajili, mikataba au hati za makubaliano washirika wa shirika, Katiba ya shirika iliyoidhinishwa na msajili wa NGO na stakabadhi za malipo ya ada ya mwaka.

Tayari Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (Nacongo) na Mtandao wa Mashirika ya Kutetea Haki za Binadamu Tanzania (THDC) wameanza kutilia shaka uhakiki huo.

Katika taarifa yao iliyotolewa hivi karibuni, wameiomba Serikali kutotumia uhakiki huo ili kuyafuta mashirika yasiyo ya kiserikali.

Taasisi hizo zinaunga mkono uhakiki lakini zinasema mashirika yaliyokuwa yanaikosoa Serikali yasifutwe kwa sababu ya uhakiki huu.

Uhakiki huu utusaidie kufahamu idadi ya mashirika yanayofanya kazi kwa kufuata taratibu na sheria za nchi.

Licha ya takwimu kuonyesha kwamba kuna mashirika yasiyo ya kiserikali zaidi ya 8,000 yanayofanya kazi yanaweza kuwa pungufu.

Ni vizuri tukawa na mashirika machache lakini yanayosaidia `kuiamsha’ Serikali ili iweze kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi.

Shirika ambalo halijawahi kufanya kazi tangu liliposajiliwa linatusaidia nini Watanzania? Ni bora likafutwa.

Mashirika ambayo hayawasilisha taarifa za hesabu za mwaka bila sababu ya msingi, hayalipi ada ya mwaka yafutiwe usajili kama ambavyo Sheria namba 24 ya NGO ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa mwaka 2005 inavyoeleza. Uhakiki huu usiwaache wavunja sheria.

Raymond Kaminyoge ni mwandishi wa gazeti la Mwananchi

-->