Thursday, September 14, 2017

Shirika lisilo la kiserikali lazima liendeshwe kwa kuzingatia sheria husika

 

By Justine Kaleb

Shirika lisilo la kiserikali (NGO) ni taasisi ya kijamii isiyofungamana na siasa, dini au Serikali ambayo haina hisa au umiliki wowote katika mashirika mengine. Lengo kuu la shirika hili, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ni kutatua changamoto zinazokwamisha maendeleo katika jamii na taifa kwa ujumla.

Ifahamike, mashirika haya si ya kibiashara hivyo hayaanzishwi kwa lengo la kujipatia fedha au faida zaidi ya kuisaidia jamii husika. Michango inayotolewa na wadau ni lazima ipelekwe kwa jamii husika kutatua kero na changamoto zilizopo.

Ili shirika liwe na nguvu kisheria ni lazima lisajiliwe. Nchini, mashirika haya husajiliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto katika ofisi ya msajili wa mashirika yasiyo ya kiserikali. Haya ni yale yanayofanyakazi nchini kote.

Wazo la kuanzisha taasisi hizi linaweza kutoka kwa mtu mmoja au kikundi cha watu ambao wanakuwa na maono katika kusaidia na kutatua changamoto walizoziona katika jamii inayowazunguka. Baadaye hushirikisha wengine watakaokuwa tayari kutekeleza maono hayo.

Miongoni mwa wanakikundi hicho hupatikana viongozi wa kukisimamia katika mchakato wa kukamilisha mapendekezo ya jina la shirika, kuandaa vikao muhimu mpaka usajili shirika.

Usajili wa mashirika haya hutofautiana kulingana na shughuli zinazotarajiwa kutekelezwa. Shirika linaweza likasajiliwa na kufanya kazi katika kata, hivyo kusajiliwa na ofisa mtendaji wa kata husika. Kwa shirika la kiwilaya, mkuu wa wilaya ndiye anayebeba dhamana ya usajili na yale yanayotaka kuhudumia mkoa mzima basi mkuu wa mkoa husika hufanya usajili.

Mashirika ya kitaifa au kimataifa, wizara inahusika na usajili wake. Ni lazima ifahamike, kuendesha shirika pasipo kusajiliwa ni kosa kisheria.

Wakati wa usajili wa shirika ni muhimu kuzingatia baadhi ya mambo ili kukamilisha mchakato huo haraka. Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na nakala tatu za katiba ya shirika zilizofungwa vizuri.

Katiba hii inapaswa kubainisha malengo, maono ya shirika na mbinu za utekelezaji wa maono hayo. Ndani ya katiba pia itaeleza idadi na aina ya mikutano ya shirika, muda wa viongozi kukaa madarakani na namna ya kusimamia mapato na matumizi ya fedha na rasilimali za shirika. Namna ya kutatua migogoro pia hubainishwa.

Jambo jingine muhimu ni muhtasari wa kikao unaoeleza idadi ya wajumbe na tarehe ya kuanzishwa kwa shirika husika, namba za simu za wajumbe, sahihi zao na viongozi wa taasisi hiyo. Ikumbukwe, viongozi ni lazima wawe katika nafasi ya mwenyekiti, katibu na mtunza hazina tu.

Wasifu wa viongozi nao unahitajika. Uimara na uadilifu wa viongozi ni nguzo ya maendeleo na mafanikio ya kila shirika hivyo ni lazima wajumbe wote watafakari kwa kina uwezo wa viongozi wanaowachagua kuliongoza shirika. Japo wazo la kuanzisha hutoka kwa mtu mmoja lakini si lazima mtoa wazo akawa sehemu ya uongozi.

Lazima iwepo barua ya utambulisho kutoka ofisi ya mkuu wa wilaya. Hii ni muhimu kwa usajili wa shirika hasa ngazi ya kitaifa. Barua hii humaanisha shughuli za shirika zitatambulika katika wilaya husika. Barua hutolewa na wilaya ambayo ofisi za shirika zinapopatikana.

Licha ya hiyo, inahitajika barua ya kuomba kusajiliwa pia. Shirika linatakiwa kuomba kusajiliwa kwa barua na anuani ya barua iendako itategemea ukubwa wa shughuli zake kama tulivyoona hapo mwanzo.

Fomu ya usajili wa shirika inayohusiana pia itahitajika. Fomu hii itapaswa kujazwa kikamilifu na kuwekwa sahihi na, mwenyekiti na katibu wa shirika husika. Fomu hii ni lazima iambatanishwe na stakabadhi ya ushuru wa forodha.

Ada ya usajili inapaswa kulipwa pamoja na kupendekeza majina yasiyopungua matano. Majina haya husaidia kuwa mbadala pale inapotokea kufana na mashirika mengine yaliokwishasajiliwa au kukataliwa kutokana na sababu nyinginezo za kiutawala na kimaadili. Malipo ya ada ni kielelezo cha kukubaliwa kwa usajili hivyo cheti kinaelekea kutolewa.

Ifahamike kuwa, endapo nyaraka tajwa hapo juu hazitakuwa na mapungufu yoyote, usajili wa shirika utaweza kukamilika ndani ya muda mfupi. Inakadiriwa, inaweza kuwa ndani ya mwezi mmoja mpaka miwili.

Baada ya usajili kukamilika, shirika hupewa cheti hivyo kuwa na nguvu ya kisheria kushitaki au kushitakiwa pamoja na uwezo wa kumiliki mali.

Shirika litekeleze shughuli zake kwa kufuata malengo, katiba na sheria na kuwasilisha ripoti ya maendeleo na kulipa ada ya kila mwaka.

Mwandishi ni wakili wa kujitegemea. Anapatikana kwa namba 0755 545 600 au jukwaalasheria@gmail.com

-->