UCHAMBUZI: Shughuli za kisiasa zifanywe na vyama vya kisiasa

Muktasari:

  • Mwalimu Nyerere anaendelea kuandika: “Ni kanuni moja ya demokrasia kwamba kazi hiyo ifanywe na vyombo hivyo vya kijamii, isifanywe na chombo cha dola au mchanganyiko wowote wa vyombo vya dola.’’

“Vyama vya siasa ni vyombo vya kijamii, si vyombo vya dola. Kazi yao ni kuunda na kuelezea sera wanazotaka zikubaliwe na jamii.’’ Hii ni nukuu kutoka katika kitabu cha Mwalimu Julius Nyerere kiitwacho ‘Tanzania, Tanzania.’

Mwalimu Nyerere anaendelea kuandika: “Ni kanuni moja ya demokrasia kwamba kazi hiyo ifanywe na vyombo hivyo vya kijamii, isifanywe na chombo cha dola au mchanganyiko wowote wa vyombo vya dola.’’

Anaongeza, “Jitihada na hoja zote za kujaribu kuhamasisha kazi hii itoke katika vyombo vya kijamii na ifanywe na vyombo vya dola, ni jitihada na hoja za kujenga udikiteta.”

Nirudi kwenye nukta ya msingi. Bara letu la Afrika limejaaliwa utajiri wa malighafi nyingi zikiwamo zile adimu na muhimu kwa maisha ya binadamu.

Pamoja na yote haya, bara hili limejijengea sifa mbaya ya kuwapo kwa minyukano ya vyama vya kisiasa inayosababisha migogoro ya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka nenda rudi.

Historia inaonyesha nchi nyingi zilizokuwa na amani zimewahi kutumbukia katika machafuko ya kisiasa na kuziacha nchi hizo na historia mpya ya uvunjifu wa amani, vita, vifo, hali mbaya ya uchumi na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Matokeo ya kupotea kwa amani katika nchi nyingi barani Afrika hayakuwahi kuwa suluhu ya matatizo mengine yanayolikumba bara hili, bali yamezidi kuiteketeza amani na kulitumbukiza katika tanuru la matatizo.

Sasa tuna bara ambalo kila siku wakazi wake wanafikiria namna wanavyoweza kulihama. Kimbilio likiwa katika nchi za Ulaya na Marekani, wakiamini kuwa ndiko kwenye maisha bora na yenye neema.

Mwandishi nguli barani Afrika, Walter Rodney katika kitabu chake cha ‘How Europe Underdeveloped Africa’ aliandika na namnukuu, “Leadership is every thing” kwa tafsiri isiyo rasmi, Rodney alikuwa anamaanisha kuwa uongozi ni kila kitu.

Kwa sura hiyo, ni dhahiri kuwa kila penye maendeleo, haki, amani na utulivu ni matunda ya uongozi.

Vivyo hivyo pasipo na maendeleo, amani nayo hupotea, chuki hutawala na ukiukwaji wa utawala bora na wa sheria huyeyuka. Na haya yote ni matunda ya uongozi.

Nini kinatofautisha kati ya sehemu yenye maendeleo na ile isiyo na maendeleo? Bila shaka ni uongozi. Msitari unaotenganisha sifa za viongozi hawa ni kuwa mmoja ni kiongozi bora wakati mwingine ni bora kiongozi.

Viongozi wote wanatokana na mifumo ya kisiasa, tatizo huanza pale viongozi walio tayari madarakani kutokuwa tayari kuruhusu vyama vingine vya kisiasa kushika hatamu za uongozi. Hili ndilo ambalo Mwalimu Nyerere alitahadharisha wazi kuhusu matumizi vya vyombo vya dola katika kufanya siasa.

Katika hili huhitaji kuzunguka sehemu nyingi ndani ya Afrika kuangalia matumizi ya vyombo vya dola katika kufanya siasa, ukiukwaji wa katiba, sheria na utawala bora.

Haya yote yamekuwa kama ada katika maeneo mengi ya bara hili na matokeo yake ni kudumaa kwa maendeleo ya nchi na ustawi wa raia.

Sababu hasa ya matumizi ya nguvu dhidi ya upinzani, hasa nyakati za uchaguzi ni uchoyo na uchu wa madaraka. Kipindi cha uchaguzi ndipo matumizi ya dola hujidhihirisha, kiasi cha kukiuka misingi ya demokrasia.

Mwalimu Nyerere alitamani kuona vyama vya siasa vikitumia sera kama silaha ya kuishawishi jamii, ili kukuza na kustawisha shina la demokrasia na si kutumia vyombo vya dola.

Vyama vya siasa viwe na fursa sawa katika majukwaa ya kisiasa ili vipate idhini na kibali kutoka kwa wananchi kwa ushawishi wa sera, itikadi na falsafa za chama husika.

Aidha, wanachosahau viongozi wengi wa Afrika ni kwamba, uwepo wa taasisi imara za kisiasa na uwazi katika chaguzi ni kichochea cha uwajibikaji, uwazi na maendeleo hasa ya kiuchumi.

Nimesema wanachosahau, lakini katika uhalisia wengi wanatambua ukweli, ila kwa sababu ya uroho wa madaraka viongozi wamejivisha miwani ya chuma. Hawataki kuona ukweli hata ulio mbele yao.

Ni wajibu wa viongozi kutambua kuwa hakuna amani bila haki. Amani ni tunda la haki. Kama kuna mbegu mbaya imepandwa nchini, basi kwa masliahi mapana ya amani ya Taifa letu, hatuna budi kuing’oa.

Tanzania ni yetu sote, walio madarakani na wasio na madaraka. Hii siyo Tanzania ya vyama vya siasa au ya watu fulani maalumu.

Iwapo Watanzania tutaweza kujiepusha na siasa zisizo na maana katika maisha na maendeleo ya Taifa letu, hakika tutakuwa na nchi bora zaidi barani Afrika.

Noel Shao ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii. Kwa mawasiliano; [email protected] au 0769-735826