Shule za umma zinahitaji mikakati ya kukuza taaluma na ufaulu

Jackline  Masinde

Muktasari:

  • Niwarejeshe katika makala hayo yaliyotoka katika gazeti hili siku za nyuma. Niliandika kuhusu utaratibu wa shule hiyo kuanza vipindi vya masomo usiku, mbinu ambayo uongozi wa shule na hata viongozi wanasema imekuwa na tija kwao hasa upande wa taaluma.

Nilipoandika makala kuhusu mbinu inayotumiwa na uongozi wa shule ya St Anne Marie ya jijini Dar es Salaam kukuza taaluma na ufaulu, wapo wadau wa elimu ambao hawakukubaliana na mbinu hiyo.

Niwarejeshe katika makala hayo yaliyotoka katika gazeti hili siku za nyuma. Niliandika kuhusu utaratibu wa shule hiyo kuanza vipindi vya masomo usiku, mbinu ambayo uongozi wa shule na hata viongozi wanasema imekuwa na tija kwao hasa upande wa taaluma.

Yalipotoka matokeo ya mtihani wa darasa la saba yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) hivi karibuni, shule hiyo ilitajwa kushika nafasi ya nane kitaifa. Mwaka 2015 ilishika nafasi ya kwanza.

Inawezekana sababu za ufaulu huo mzuri zikawa nyingi, lakini naamini mbinu hiyo ina mchango mkubwa katika mafanikio ya shule hiyo.

Kwa wengi inaonekana kuwa ni mbinu ya ajabu na inawezakana wasikubaliane nayo, lakini ukweli unabaki kuwa uongozi wa shule hii angalau umekuna kichwa na kuja na mkakati wanaofikiri unaweza kuwasaidia kitaaluma.

Kimsingi, hiki cha St Anne Marie ndicho kinachopaswa kufanywa na kila shule inayotamani mafanikio. Haijalishi mbinu hiyo inatazamwaje na wengine.

Angalau shule nyingi binafsi zimekuwa zikijihimu kuwa na mbinu mbalimbali za kukuza ufaulu; ndio maana haishangazi kuona kuwa kila mwaka shule hizi zinafanya vizuri zikiziacha kwa mbali shule za umma.

Kuna haja sasa ya shule za umma kuwa na mikakati imara ya kukuza taaluma hata kama mikakati hiyo itaonekana kwa mtazamo tofauti na wengine.

Ukizungumza na wanafunzi wa St Anne na hata wazazi wao, wote wanaonekana kuafiki utaratibu wa wanafunzi kuanza masomo usiku.

Wadau wa shule za umma yaani wazazi, viongozi wa Serikli na wengineo nao wanaweza kukaa kitako na walimu kubuni mbinu za kukuza taaluma.

Zamani shule nyingi za umma zilikuwa zikiendesha masomo ya ziada kwa wanafunzi wa madarasa ya mitihani kama vile darasa la nne na la saba. Utaratibu huu ambao pamoja na ukweli kuwa ulisukumwa na walimu kujipatia kipato, angalau uliweza kuonyesha tija katika baadhi ya shule.

Lakini, kwa sababu ya walimu kujali zaidi fedha na wakati mwingine kutowajibika ipasavyo, utaratibu huu ukawa kikwazo kwa wanafunzi wengi. Hatimaye kuja kwa sera ya elimu bila ada ukaua utaratibu huu.

Hivi sasa shule nyingi hazina mikakati, mianya ya walimu kupata fedha haipo na wala hawaoni tena haja ya kukuna vichwa kubuni mikakati ya kukuza taluma shuleni.

Ni kweli hivi sasa elimumsingi ni bure, lakini naamini bado shule zina nafasi ya kukaa pamoja na wadau kwa ajili ya kubuni mikakati ya kukuza taaluma.

Siyo lazima mikakati hiyo ihusishe fedha, lakini kilicho muhimu ni mipango ya kuboresha elimu.

Kwa mfano, wakati ada na michango ikipigwa vita shuleni, viongozi wa shule kwa kibali maalumu wanaweza kutafuta wafadhili katika maeneo yao wanaoweza kufadhili programu za kukuza taaluma shuleni kama ilivyokuwa zamani.

Sidhani hili la kutafuta wafadhili linaweza kukataliwa kwa hoja kuwa sasa ni zama za elimu bure. Ieleweke kuwa hapa fedha au rasilimali za uendeshaji programu hizo hazitoki kwa wazazi bali kwa wafadhili.

Kusitishwa kwa michango kusiwe sababu ya walimu katika shule za umma, kukataa kuwa na mikakati ya kukuza taaluma.

Zipo shule hasa maeneo ya mijini zenye vitega uchumi vinavyoingiza mamilioni, lakini viongozi wa shule hizo hawaoni haja ya kutumia mapato hayo kufadhili programu za kuboresha taaluma.