Si kila maumivu ya matiti ni saratani

Muktasari:

Kama ilivyo kwa aina nyingine za saratani, kugundua dalili za mapema ni hatua muhimu kukabiliana nayo.

Saratani ya matiti ni miongoni mwa zinazosababisha vifo vingi nchini. Hivyo, ni muhimu kufahamu namna ya kuepuka vihatarishi vyake.

Kama ilivyo kwa aina nyingine za saratani, kugundua dalili za mapema ni hatua muhimu kukabiliana nayo.

Moja ya njia rahisi ya kuzitambua dalili za mapema za saratani ya matiti ni kujichunguza kwa kujishika matiti mara kwa mara ili kubaini dalili ndogondogo kama vile uvimbe na kutoka matone kwenye chuchu (self breast exam) kabla ya kufanya vipimo hospitalini.

Wanawake wengi hupata hofu wanapopata maumivu ya matiti kwa kudhani yanaashiria saratani ya matiti. Dhana hii imetawala akili za wanawake wengi huenda ni kutokana na hofu au kutokuwa na uelewa wa kutosha.

Dalili ambazo hupaswi kuzifumbua macho ni uvimbe kwenye titi, ngozi ya titi kubadilika rangi, kutokwa na matone kweye chuchu na maumivu kwenye chuchu. Hata hivyo, kama unapata maumivu kwenye matiti, ondoa hofu.

Maumivu hutokana na sababu mbalimbali, leo nitaeleza aina tatu.

Aina ya kwanza ni ‘cyclical breast pain’. Maumivu haya mara nyingi huwa yanakuja na kupotea kwa vipindi tofauti. Maumivu haya hujitokeza mara nyingi wakati wa hedhi na hutoweka wakati hedhi inapokoma. Hivyo ni kawaida kwa mwanamke anapokuwa kwenye mzunguko wa hedhi na hasa akiwa kwenye umri wa miaka 30 hadi 40 na wakati ambao mwanamke ameshafika umri wa kutoweza kuzaa tena.

Maumivu pia yanatokea kwa sababu baadhi ya tishu za kwenye matiti zinapokea mabadiliko malimbali ya homoni wakati mwanamke anapokuwa kwenye mzunguko wa siku zake na ndiyo maana wanawake wanaotumia vidonge vya uzazi wapo hatarini sana kupata maumivu ya aina hii.

Lakini habari njema ni kwamba mwanamke hana haja kuwa na hofu kuhusu maumivu haya ya matiti yanayojitokeza wakati wa hedhi kwa kuhofia huenda yakawa ni dalili za saratani.

Aina ya pili ni maumivu kwenye matiti ni ile inayojitokeza mara kwa mara bila wakati maalumu. Aina hii kwa kitaalamu inaitwa non-cyclical breast pain. aina hii ya maumivu huwapata wanawake wenye umri uliozidi miaka 40 na wale ambao wamefikia umri ambao hawawezi tena kuzaa. Hii inaweza kutokea kwenye titi moja au yote. Ni muhimu kuchunguza kama maumivu haya yanatoka kwenye matiti yenyewe au kwenye misuli. Na ni vyema kupata msaada wa daktari ili kutambua.

Na aina ya tatu ni maumivu yanayotokana na maambukizi ya magonjwa mbalimbali, inaitwa mastitis and shingles kwa kitaalamu.

Maambukizi haya mara nyingi hutokea wakati wa ujauzito kutokana na mabadiliko ya mfumo wa homoni yanayojitokeza kwa mjamzito mara kwa mara. Mjamzito anashauriwa kupata ushauri wa kitaalamu katika kipindi hiki ili maambukizi na maumivu haya kwenye matiti yasiathiri afya yake na mtoto.

Hata hivyo, ni muhimu kufuatilia mara kwa mara mabadiliko madogomadogo yanayojitokeza kwenye matiti ili kubaini tatizo lolote lile la kiafya kwenye matiti mapema zaidi.

Njia rahisi ya kufuatilia maendeleo ya afya ya matiti yako ni ile ya kujifanyia vipimo asilia. Njia hii hufanywa na mwanamke mwenyewe. Mwanamke anashauriwa kuyashika matiti yake mara kwa mara kwa kufanya kama anayakamua ili kuweza kubaini dalili za uvimbe na mabadiliko mengine madogo madogo.