Sido, Tirdo zituongoze Tanzania ya Viwanda

Muktasari:

  • Kiongozi huyo alisema ikiwa wajasiriamali hao watapata mafunzo ambayo yatawawezesha kuanzisha viwanda vidogovidogo, upotevu wa mazao usiokuwa wa lazima utapungua.

Juzi, katibu tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresia Mmbando alifunga mafunzo ya ujasiriamali yaliyoendeshwa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) na kulitaka kuwaandaa wajasiriamali kuanzisha shughuli za kiuchumi ambazo zitakuwa na mchango kwa Taifa.

Kiongozi huyo alisema ikiwa wajasiriamali hao watapata mafunzo ambayo yatawawezesha kuanzisha viwanda vidogovidogo, upotevu wa mazao usiokuwa wa lazima utapungua.

Tunaunga mkono wito huo tukiamini kwamba huo mwelekeo sahihi wa kufikia lengo la Tanzania ya viwanda na ndiyo njia sahihi na ya uhakika ya kukuza uchumi wa Taifa na watu wake.

Tunasema hivyo tukiamini kwamba matumizi ya teknolojia rahisi yatakuwa chachu ya uzalishaji mashambani hivyo mazao ya wakulima ambao ni zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania wote, si tu kwamba yatapata soko, bali yataongezewa thamani hivyo kuuzwa kwa bei nzuri zaidi.

Ili kufikia lengo hilo, tunaamini kwamba ikiwa Sido itajengewa uwezo na kutoa mafunzo ya utengenezaji wa zana rahisi za uzalishaji na uchakataji wa mazao, kazi ya kuiendea Tanzania ya viwanda itakuwa na mafanikio makubwa.

Tumekuwa tukiona katika mitandao ya kijamii, video mbalimbali zikionyesha mashine rahisi za kulimia, kupalilia, kuweka dawa na kuvuna mazao baadhi zikiwa zinatumia mikono. Tunaamini kwamba hizi zikitengenezwa na kusambazwa kwa wingi nchini, uwezo wa wakulima kulima maeneo makubwa, kuyapalilia, kuweka dawa na kuvuna utakuwa mkubwa zaidi hivyo kuongeza uzalishaji ambao bila shaka matokeo yake yatakuwa ni kuongezeka kwa kipato.

Vivyo hivyo, mashine rahisi za kuchakata mazao kama alizeti, muhogo, karanga, kahawa, pamba na mazao mengine ya chakula na biashara kazi zitasaidia kuongeza thamani ya mazao.

Tunafahamu kwamba kazi hii inafanywa pia na Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (Tirdo) ambalo linashughulika na utafiti wa teknolojia za viwandani na kutoa ushauri wa masuala ya kiteknolojia katika sekta ya viwanda, lakini hapa tunataka uwepo msukumo mkubwa zaidi na uwekezaji katika sekta hii.

Tirdo inafanya utafiti unaolenga kuongeza thamani ya malighafi inayopatikana nchini kwa ajili ya matumizi ya viwanda vya ndani na kuuza nje ya nchi, tunaamini kazi hiyo ikifanywa chini ya mkakati wa ‘operesheni viwanda’, matokeo yake yataakisi hali za wananchi ndani ya kipindi kifupi.

Tirdo kwa mfano, imeshawahi kufanya tafiti mbalimbali ambazo kwa mujibu wa taarifa ya miaka 50 ya Sekta ya Viwanda Tanzania ni pamoja na kuboresha uyoga, unga wa muhogo na matumizi bora ya nishati na kutengeneza mashine mbalimbali zikiwamo za kuparaza muhogo, kukamua mafuta ya mawese kutoka katika mchikichi na urejeshaji taka.

Tunataka kuona jitihada hizi zikiungwa mkono na kuwa sehemu ya ajenga ya nchi kuelekea katika uchumi wa kati. Tunaamini kuwa kwa kuiinua sekta ya kilimo hususan wakulima wadogowadogo ambao ndiyo wengi zaidi nchini, upatikanaji wa malighafi za kutosha kwa ajili ya viwanda vyetu na hata vya nje utaongezeka.

Na hiyo maana yake ni kwamba tutakuwa tumewapatia soko wakulima wetu hivyo kuneemeka zaidi, sambamba na kuongeza ajira zitakazotokana na wingi wa malighafi.