Sikilizeni kilio cha watu hawa mkifanyie kazi

Muktasari:

 

  • Walibainisha kuwa baadhi ya watoto kutoka familia za watu wenye ulemavu hushindwa kufaidi fursa hiyo kutokana na umbali uliopo kati ya makazi yao na shule za msingi na sekondari. Familia hushindwa kugharamia usafiri kwa watoto hao.

Hivi karibuni, watu wenye ulemavu waliiomba Serikali kuwatazama katika jicho la pekee katika fursa iliyopo ya utekelezaji wa sera ya elimu bure inayotekelezwa kwa wananchi wote, kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha nne.

Walibainisha kuwa baadhi ya watoto kutoka familia za watu wenye ulemavu hushindwa kufaidi fursa hiyo kutokana na umbali uliopo kati ya makazi yao na shule za msingi na sekondari. Familia hushindwa kugharamia usafiri kwa watoto hao.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu ya Shirikisho la Vyama vya Watu wenyeulemavu Tanzania (Shivyawata), Doris Kulanga alitoa ombi hilo alipozungumza na gazeti hili na kuomba taasisi na Serikali kuangalia namna ya kuwasaidia kutatua changamoto hiyo.

Wakati mkurugenzi huyo akitaka kundi hili kutazamwa kwa jicho la huruma, takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi zinaonyesha kuwa hadi kufikia 2007, kulikuwa na watoto 24,003 wenye ulemavu walioandikishwa katika shule za msingi, sawa na chini ya asililimia moja. Kwa maana hiyo ni asilimia moja tu ya watoto wenye ulemavu ndio waliopata fursa ya elimu.

Lakini takwimu zinaonyesha pia hadi kufikia Juni 2008 kulikuwa na watoto wenye ulemavu wanaokaribia 34,661, wavulana 19,998 na wasichana 14,663. Na wengi walikuwa ni wale wenye ulemavu wa viungo na wa kusikia walioandikishwa walikuwa asilimia 21 huku wenye ulemavu wa akili walikuwa asilimia 17 pekee.

Lakini takwimu zilizotolewa na Moevt kwa 2008, zinaonyesha uandikishaji wa watoto hao wenye ulemavu kwa upande wa wavulana ulikua kwa asilimia 49.6, hali ambayo inaweza kuzua maswali ya uandikishaji kwa upande wa uwiano wa jinsi. Inawezekana tofauti hiyo ikawa ilichangiwa na mtazamo wa jamii yenyewe kuwapendelea watoto wa kiume wenye ulemavu badala ya wa kike.

Hata hivyo binafsi nazitazama takwimu hizi kuwa haziwezi kutoa picha halisi ya uwiano kati ya watoto wa kike wenye ulemavu na wale wa kiume walioandikishwa kwenda shule kwa kuwa hawakupata fursa.

Wakati nikiwaza haya, Kulanga anakiri kuwa kundi la wanawake lina changamoto zake, lakini kundi la wanawake walemavu lina changamoto kubwa zaidi kutokana na kukabiliana na vikwanzo mbalimbali vya kielimu, kiuchumi na hata huduma za nyingine za jamii.

Anasema ukiangalia elimu kwa sasa inatolewa bure kutoka darasa la kwanza hadi sekondari, lakini watoto kutoka familia za watu wenye ulemavu hawawezi kufaidi fursa hiyo kutokana na shule hizo kuwa mbali na maeneo wanayoishi, hali inayowafanya wazazi wao washindwe kugharamia usafiri wa kufuata elimu hiyo licha ya kuwa ya bure.

Kilio cha mwenyekiti huyo ambaye pia ni mlemavu wa macho, kinapaswa kusikilizwa na wadau wote wa elimu na Serikali kwa kuwa ni ukweli usiopingika kuwa familia nyingi za watu wenye ulemavu zina kipato duni, gharama kwao ni mtihani mwingine unaotakiwa kutafutiwa ufumbuzi wa haraka.

Mjumbe wa Shivyawata, Nasiria Ally ambaye ni kiziwi anasema kundi hilo limetelekezwa kielimu ikilinganishwa na makundi mengine.

Anasema shule nyingi za viziwi hazina vifaa vya kutosha na kwamba, hata ukiangalia kwenye vyombo vya uamuzi, walemavu hawashirikishwi. Anasema kundi hilo linashindwa kuingia hata katika ushindani wa siasa kutokana na kutokuwa na mazingira ya kuvutia kwa watu wa aina hiyo.

Kilio hicho kinanisukuma kutoa ushauri kwa wadau wa maendeleo, kuangalia usawa wa elimu na fursa nyingine kama zinaifikia jamii yote bila vikwazo ili kila mmoja anufaike.

Bado changamoto ya umbali wa shule za sekondari na ukosefu wa mabweni kwa shule nyingi za Serikali inaathiri zaidi kundi hili lenye kipato duni.

0713235309