Siku ya wanawake iwanufaishe pia vijijini

Muktasari:

  • Chimbuko la maadhimisho haya limeanzia mbali tangu Machi 8 mwaka 1857 baada ya wanawake waliokuwa wakifanya kazi kwenye kiwanda cha nguo jijini New York nchini Marekani kugoma kutokana kupinga mazingira magumu ya kazi.

Siku kama ya kesho, Machi 8 kila mwaka, wanawake nchini huungana na wenzao duniani kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.

Chimbuko la maadhimisho haya limeanzia mbali tangu Machi 8 mwaka 1857 baada ya wanawake waliokuwa wakifanya kazi kwenye kiwanda cha nguo jijini New York nchini Marekani kugoma kutokana kupinga mazingira magumu ya kazi.

Pengine mgomo huo usingepata umaarufu na heshima ulionao sasa iwapo uongozi wa kiwanda hicho usingechukua uamuzi wa kikatili na dhuluma kwa maisha ya wanawake hao kwa kuwafungia katika chumba na kuwateketeza kwa moto.

Inakadiriwa zaidi ya wanawake 129 walikufa katika tukio hilo lililoibua hisia kali kote duniani na masikitiko yao kuthibitishwa na maelfu watu waliohudhuria mazishi ya wanawake hao.

Mwaka 1910, kongamano kubwa la kuwakumbuka wanawake hao lilifanyika nchini Denmark ambako azimio lilipitishwa kuifanya Machi 8 ya kila mwaka kuwa siku ya kuwakumbuka waathirika wa tukio hilo ikiwa kama ishara ya kuamsha hamasa ya kupigania haki na maendeleo miongoni mwa wanawake.

Licha ya upinzani kutoka mataifa makubwa kupitia Umoja wa Mataifa, siku hiyo ilianza kuadhimishwa rasmi mwaka 1975 na baadaye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuitangaza kuwa ni Siku ya Wanawake na Amani kuanzia mwaka 1977.

Kupitia maadhimisho ya siku hiyo, UN pamoja na mashirika yake yanafanya kila linalowezekana kukuza ushiriki wa wanawake kama washirika sawa na wanaume katika harakati za maendeleo endelevu, amani, usalama na heshima kwa ajili ya haki za binadamu.

Kila mwaka, Tanzania inakuwa na kaulimbiu ya maadhimisho hayo na mwaka jana, ilikuwa “Tanzania ya viwanda; wanawake ni msingi wa mabadiliko ya kiuchumi.”

Tangu Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 na baadaye Tanzania baada ya Muungano, ushiriki wa wanawake katika shughuli za kisiasa ulikuwa mdogo kulinganisha na wanaume.

Kwa mfano, kati ya mwaka 1961 hadi 1965 ushiriki wa wanawake bungeni ulikuwa ni asilimia 1.9 huku wanaume wakiwa asilimia 98.1.

Hali hiyo imeendelea kwa miongo kadhaa hadi chaguzi za hivi karibuni ambapo kiwango hicho kimeongezeka hadi kufikia zaidi ya asimilia 22 na kwa mara ya kwanza nafasi ya makamu wa rais ikishikiliwa na mwanamke, Samia Suluhu Hassan.

Kabla ya nafasi ya makamu wa rais, nafasi ya juu katika mihimili ya dola iliyowahi kushikiliwa na mwanamke ni uspika wa Bunge kupitia kwa Anne Makinda na sasa unaibu unaoshikiliwa na Dk Tulia Ackson.

Mwaka 2005, Dk Anna Senkoro (sasa marehemu) aliweka historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza kuwania nafasi ya urais kupitia chama cha PPT-Maendeleo.

Anna mwingine, ambaye sasa ni mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira naye akawa wa pili kuwania nafasi hiyo kubwa mwaka 2015 kupitia ACT-Wazalendo.

Dk Asha-Rose Migiro aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Getrude Mongella aliyekuwa Spika wa Bunge la Afrika, Profesa Anna Tibaijuka aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-Habitat) ni miongoni mwa wanawake nchini walioweka historia ya kushika madaraka makubwa Kitaifa na Kimataifa.

Hata hivyo, swali kubwa ni jinsi gani idadi kubwa ya wanawake wanaoishi vijijini wanavyonufaika na harakati zinazoambatana na maadhimisho haya ya wanawake duniani.

Asilimia zaidi ya 70 ya watu nchini, wengi wao wakiwa wanawake wanaishi vijijini ambako pia umaskini umekithiri.

Huko ndiko hakuna huduma ya uhakika ya afya ya uzazi, maji, hakuna fursa sawa za kiuchumi na uongozi huku vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia vikiripotiwa kwa wingi kutokana na jamii kuendelea kushikilia mila na desturi kandamizi dhidi ya wanawake na watoto wa kike.

Muda sasa umefika kwa wanawake nchini kubadilisha njia na namna ya kuadhimisha siku hii muhimu kwa kuacha maandamano na makongamano kwenye mitaa na kumbi za mikutano, badala yake waende vijijini kukutana na kuzungumza wenzao ili kujua changamoto na kuzitafutia ufumbuzi.

Faraja kwa wanawake na wasichana vijiji ambao bado wengi wao wanatumia matambara kujihifadhi wakiwa kwenye hedhi, huku kundi hilo likiendelea kuwa wazalishaji bila kuwa na sauti juu ya wanachozalisha litapatikana iwapo harakati za ukombozi wa mwanamke zitajikita vijijini badala ya mijini.

0768920097.