Simba, Yanga jipangeni, mambo yameanza kuiva

Muktasari:

  • Ratiba hizo kwa mashindano hayo mawili, zitahusisha Simba na Yanga ambazo ndizo wawakilisha wa Tanzania katika michuano ya klabu Afrika.

Wiki hii, Shirikisho la Soka Afrika, CAF, litapanga ratiba ya michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.

Ratiba hizo kwa mashindano hayo mawili, zitahusisha Simba na Yanga ambazo ndizo wawakilisha wa Tanzania katika michuano ya klabu Afrika.

Yanga ambyo ilianza Ligi ya Mabingwa na kushuka Kombe la Shirikisho msimu uliopita, itakuwa na kazi kubwa kuonyesha kuwa inahusika na inaweza sanjari na Simba.

Watanzania hawataki kuona timu zao zinavuka raundi ya awali ikija raundi ya kwanza nje.

Imekuwa kawaida, zinakuja timu za Comoro, Shelisheli na Madagascar baada ya hapo labda unapigwa Botswana zikipelekwa Kaskazini, mchezo unamalizikia hapo.

Kiukweli hii ni fedheha ambayo inatakiwa klabu wawakilishi wetu, kujipanga na kutambua wajibu wao mbele.

Yanga na Simba ndiyo wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya klabu Afrika, Yanga ikishiriki Ligi ya Mabingwa wakati Simba inawakilisha Kombe la Shirikisho ikiwa ni mara ya kwanza baada ya miaka minne kufanya hivyo.

Tumeona timu hizi zikipimana mbavu katika usajili, timu zimekimbia kasi mno kunyang’anyana wachezaji, lakini wakati sasa wa kujiandaa.

Kama nilivyosema, hatutaki kuona baada ya Comoro, mambo ndiyo yamekwisha, liendelezwe hata zije timu za Kaskazini au Magharibi, zikija ni mabao na yote yatapatikana kwa maandalizi pekee.

Ni dhahiri kwamba baadhi ya timu zikisikia Simba, Yanga zinajua tu zimeshavuta, sasa kuonyesha kwamba mawazo yao siyo, ni kufanya maandalizi na kuzishangaza.

Katika maandalizi, kuna eneo wanajisahau. Simba na Yanga na hata Azam zinajisahau hapa.

Huwezi kucheza bila kumsoma mapema adui yako.

Baada ya ratiba kupangwa na timu hii na hii nani anacheza na nani, ni vema kuanza kuzichunguza.

Ukweli, hata timu ifanye maandalizi ya namna gani, inatakiwa kuwafahamu mapema, kuwafuatilia wapinzani wanacheza aina gani ya soka, wanatumia wakali wapi udhaifu na ukali wa wahusika uko eneo gani kitu kitakachowasaidia hata katika mechi zao.

Kuna umuhimu wa kujiandaa na zaidi kupata walau mikanda kuwajua wapinzani, ukali na udhaifu wao wanapokuwa uwanjani.

Pamoja na mabadiliko ambayo Watanzania, wanataka kuona timu zinatakiwa kufika mbali. Ni aibu, kila mwaka timu kuishia njiani.

Kumekuwa na kashetani katika vichwa kuamini timu za Kaskazini kuwa zinaweza, timu zinakata tamaa mapema zikisikia zinaelekezwa kaskazini, lakini kikubwa ni maandalizi na kujipanga na kama nilivyosema, kuzikata kilimi.

Maandalizi mazuri, kusoma timu na kufahamu data za mpinzani zinaweza kufikisha timu katika mafanikio kama yalivyo kwa TP Mazembe.

Kwani TP Mazembe wanafanyanye, ni haya haya tunayosema na ndiyo maana kila siku wanakula Dola za CAF.

TP Mazembe wametwaa Kombe la CAF na wamekomba Dola za Kimarekani 625,000 (Sh1.4 bilioni). Hizo ni za Simba ikifikia huko.

Anayeshinda Ligi ya Mabingwa hupewa Dola 2.5 milioni (Sh5.7 bilioni) ambapo kwa mwaka huu zawadi hiyo imekwenda kwa Wydad Casablanca ya Morocco.

Wanaopata wanapataje zishindwe Simba na Yanga? Kikubwa ni maandalizi na mengine yote yanayohusiana na maandalizi. Kubwa ni kumsoma mpinzani, inawezekana.