Simba Day imefanikiwa, sasa viongozi Simba fanyeni haya

Muktasari:

  • Nilisema kuwa ningekuwa mmoja wa viongozi wa Simba, ningewakataa SportPesa kutupa Sh900milioni. Nilieleza sababu.

Baada ya Simba kupata udhamini wa SportPesa niliandika makala moja ambayo nilipata ujumbe mwingi ukitaka niirudie niendelee kuandika ili siku moja viongozi sio wa Simba tu, hata Yanga waupate.

Nilisema kuwa ningekuwa mmoja wa viongozi wa Simba, ningewakataa SportPesa kutupa Sh900milioni. Nilieleza sababu.

Oktoba 5, 2004, Shirika la Ndege la Emirates liliingia mkataba wa miaka 15 na Arsenal unaokadiriwa kufikia zaidi ya Pauni 100 milioni.

Mkataba walioingia ni pamoja na haki ya jina la uwanja baada ya Emirates wenyewe kuwajengea kwa makubaliano maalumu.

Arsenal ilikuwa inadhaminiwa na O2 na mkataba wake ulipomalizika, mwishoni mwa msimu wa 2005/06 jamaa wa Emirates hawakulaza damu. Wakazama jumla.

Kutoka uliokuwa uwanja wao wa Highbury, wakaja na uwanja mpya waliojengewa na hawa jamaa wa Emirates. Walijenga uwanja na kuwadhamini kwa jezi na mambo mbalimbali huku wakiendelea kumwaga pesa.

Kulikuwa tu na mizengwe ya kuuita Uwanja wa Emirates kwa waandaaji wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hawakutaka hilo jina kwa kuwa linaitangaza Emirates ambao hawakuwa wadhamini wao, lakini Emirates wakajiongeza, wakawa sehemu ya udhamini wa UEFA.

Mwanzoni UEFA walitaka jina la kawaida kama lilivyo la Uwanja wa Allianz Arena mjini Munich lakini isiwe Emirates, jina la biashara.

Haya. Ilipofika Novemba 2012, Arsenal na Emirates wakatangaza dili lingine la Pauni 150 milioni kwa kutumia tu jina la Emirates kwa uwanja. Ushirikiano wa Emirates na Arsenal pia umeingia kwenye udhamini wa mechi za ligi na mashindano, jina la mdhamini katika vifaa vya mechi na mazoezi, kwa miaka mitano inayomalizika mwaka huu.

Hivi ninavyosema, tayari wameingia mkataba mwingine, Emirates wanadhamini tena jezi za Arsenal kwa msimu wa 2018/2019 kwa Pauni 150 milioni (Sh436.5 bilioni). Ukiacha hiyo, kitendo cha kukubali kudhamini, Arsenal wakapigwa Pauni 30 milioni.

Ukirudi kwenye uwanja, kuna mkataba mwingine kwa klabu kutumia jina la Emirates ambao unamalizika 2028.

Nimerudia kuonyesha mfano mdogo tu wa Arsenal na nimesema ningepewa pesa za Sportpesa ningezikataa kwa sababu. Si kuzikataa tu kwa sababu nazikataa, ningeziundia mkakati. Ningewapeleka wadhamini hao Bunju. Kila mtu wa Simba ananielewa nikisema Bunju.

Nilishasema, ningemwambia anayetaka kunidhamini ninaoutaka ni wa huku Bunju. Arsenal wamepata uwanja na wanauita Emirates, wana hasara gani? Mfano, ukiitwa Uwanja wa SportPesa au EAG Stadium kuna ubaya gani?

Hilo ni moja, lakini la pili, niliiona Simba Day ilivyokuwa, watu walihamasika na hata kuingiza zaidi ya Sh200milioni. Hii ni historia kwa Simba kwani haijawahi kutokea Simba Day kuingiza fedha hizo.

Sasa, picha imeshaonekana, ianze kutafsiriwa. Isiwe kuwa picha inaonekana halafu inashindwa hata kupata tafsiri. Simba inaweza kuitumia Simba Day kuwekeza.

Mfano, inaweza kufanya Simba Day kwa Tanzania nzima na dhima iwe kwa ajili ya kuchangisha fedha za ujenzi wa uwanja wake, inaanza mapema na mechi ya mwisho Simba Day inabaki Agosti 8, Dar es Salaam.

Waandaaji wanaweza kuigawa Tanzania kwa Kanda nne; Nyanda za Juu Kusini, Mashariki, Kaskazini na Ziwa.

Mfano, Nyanda za Juu Kusini Uwanja wa Sokoine Mbeya unaweza kuandaliwa kwa Simba Day, matawi ya mikoani yanatumika kuhamasisha na kufanya shughuli za kijamii kuelekea Simba Day kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa tarehe yake. Timu ikatoka Zambia kwa mfano.

Vivo hivyo kwa mikoa ya Kati, Dodoma, Singida, Tabora inaandaliwa mechi Uwanja wa Jamhuri Dodoma au Ali Hassan Mwinyi Tabora. Timu ikatoka DR Congo au Rwanda au Burundi.

Pia kadhalika, kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa, ikaandaliwa mechi na timu ya Uganda, Kaskazini timu ikatoka Kenya. Mechi zinafanyika baada wanachama wa Kanda kufanya mambo yao kuelekea siku ya Simba.

Ninaamini maandalizi yakianza mapema, usajili ukafanyika kwa hatua gharama za mechi zitarudi na Simba itapata fedha zake za ujenzi wa uwanja. Mbona inawezekana ni mipango tu!

Sasa, hapo kuwe na mikakati ya usajili mapema na kila kanda itaandaa utaratibu wake kuitambulisha Simba.

Uwepo wa watu wa masoko ni muhimu kwa ajili ya kusaka wadhamini wa kuidhamini Simba Day pekee, pia kuuza jezi mpya na kila aina ya kifaa cha Simba. Hapo sasa wanatakiwa waadilifu kwelikweli na inaweza kutengenezwa kitu, ‘Road to Bunju’ kuwa safari yote ni uwanja wa Bunju.

Simba inaweza, lakini kwa staili hii, bila mabadiliko, bila kuchanganua akili itabakia ombaomba.

+255 655 264 003