Simba na Yanga sijui zimerogwa na nani jamani

Muktasari:

  • Ndiyo! Simba au Wekundu wa Msimbazi, ukipenda waite Lunyasi au Taifa Kubwa ni miongoni mwa timu mbili zenye mashabiki wengi zaidi siyo tu hapa nchini, lakini katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki. Timu nyingine yenye mashabiki wengi ni Yanga, lakini Simba na Yanga hazina maendeleo.

Unaweza kusema, Simba ni klabu kongwe na kubwa isiyo na maendeleo, vivyo hivyo klabu ya Yanga.

Ndiyo! Simba au Wekundu wa Msimbazi, ukipenda waite Lunyasi au Taifa Kubwa ni miongoni mwa timu mbili zenye mashabiki wengi zaidi siyo tu hapa nchini, lakini katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki. Timu nyingine yenye mashabiki wengi ni Yanga, lakini Simba na Yanga hazina maendeleo.

Ukongwe wa klabu hizi mbili na hadhi zao haviendani kabisa na maendeleo yao. Klabu hizi ni kubwa na maarufu lakini hazina maendeleo ya msingi. Ukiacha mafanikio, hata suala la mafaniko katika mashindano ya Afrika unaweza kusema si sana.

Ninasema klabu hizi hazina maendeleo kwa sababu licha ya msingi wake mkuu kuwa soka, hazina viwanja vya mazoezi. Uwanja wa Kaunda haufai, wa Bunju unasuasua, zinakodi viwanja vya kuchezea mechi, hazina wadhamini wengi. Klabu inatakiwa kuwa na mdhamini mkuu, washirika katika udhamini, wadhamini kutoka sehemu mbalimbali, wadhamini wa mechi husika, hazina mabalozi wa klabu (zinatakiwa ziwe na angalau wachezaji nyota wanne kwa mwaka waliowahi kufanya vizuri katika klabu hizo, ili wawe wanafanya kazi ya kuwa mabalozi wa klabu hizo), hazina mifuko maalumu kwa ajili ya kuwasaidia wachezaji wao wa zamani (klabu inatakiwa kuwa na harambee za kutafuta fedha kwa ajili ya kulinda historia yake kwa kuwasaidia wachezaji wake wa zamani na wafanyakazi wake). Klabu hizi, hazina mpango wa kuwawezesha wachezaji wake kupata fursa mbalimbali za kutangaza biashara za kampuni (klabu za Simba na Yanga zina wachezaji wengi wanaochezea timu za taifa na wanaocheza mashindano mbalimbali ya Afrika ambao zinaweza kuwatumia kuingia mikataba na kampuni mbalimbali kwa ajili ya kutangaza bidhaa za kampuni hizo), hazina mipango ya bora ya kuibua vipaji na fursa mbalimbali, hazina mipango iliyo wazi ya kibiashara, hazina mipango bora ya kuwasaidia walemavu na watu wenye uhitaji, hazina vituo bora vya kutoa habari (kazi za vituo hivi ni kuelezea matukio mapya ya klabu na mikutano ya habari inayofuata, kutoa taarifa za mechi za klabu, kuelezea mazoezi ya klabu, kuelezea wachezaji n.k.

Klabu hazitangazi ajira ilizonazo hivyo kuwanyima fursa wanachama na mashabiki wenye uwezo kuomba ajira hizo katika mfumo ulio rasmi, hazina maduka ya bidhaa zao, bidhaa kama jezi za wachezaji, fulana, skafu, track suit na vitu vingine vingine kwa ajili ya mashabiki wanaume, wanawake na watoto (baadhi ya bidhaa zao zinazouzwa hivi sasa kama vile jezi zinauzwa na wajanja wachache na siyo klabu), hazina rekodi mbalimbali za wachezaji, viongozi n.k.

Hakika kuna vitu vingi vya kimaendeleo ambavyo klabu hizi za Simba na Yanga hazifanyi na hivyo kukosa maendeleo kulingana na umri na mashabiki zilionao.

Kila mwaka kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, klabu ya Simba huwa na wiki ya Simba, ambapo wiki hiyo humaliziwa kwa kufanyika kwa tamasha kubwa linaloitwa Simba Day ambalo kwa mwaka huu litafanyika kesho jijini Dar es Salaam.

Ndiyo, Simba hutumia wiki ya Simba kutembelea watoto yatima, kutembelea watoto wanaofanyiwa upasuaji wa moyo, kugawa mipira kwenye kliniki, kampeni ya mtaa kwa mtaa, wachezaji kuongea na mashabiki, na kutambulisha jezi mpya, na wachezaji wapya katika tamasha la Simba Day.

Kwa mtazamo wangu, Simba inachokifanya katika wiki ya Simba ni kitu kizuri na kinastahili kuungwa mkono na watu wanopenda michezo, lakini pia, ninawashauri wanachama na mashabiki wa Simba kuwasimamia na kuwafuatilia viongozi wao waweze kuwajibika vya kutosha, wawe na mipango kwa maendeleo ya klabu.