Simba waifanyie kazi kauli ya Magufuli

Muktasari:

Mchezo huo ulitumika kuikabidhi Simba kombe la ubingwa wa ligi hiyo ilioutwaa hata kabla ya kumalizika kwa mechi zake.

Kwa mara ya kwanza tangu alipoingia madarakani, juzi Rais John Magufuli alihudhuria mechi ya mpira wa miguu alipokuwa mgeni rasmi katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Simba na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa.

Mchezo huo ulitumika kuikabidhi Simba kombe la ubingwa wa ligi hiyo ilioutwaa hata kabla ya kumalizika kwa mechi zake.

Kwa ubingwa huo, Simba itaiwakilisha Tanzania kwenye michuano ijayo ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayoanza Desemba mwaka huu baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kubadili utaratibu wa uendeshaji wa mashindano yake.

Katika mechi hiyo ya juzi, mashabiki wa Simba walishuhudia timu yao ikifungwa kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa ligi hiyo na kushindwa kulinda rekodi hiyo katika dakika za lala salama kwani sasa imebakiwa na mchezo mmoja, dhidi ya Majimaji ya Songea.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Rais Magufuli aliwapa neno wachezaji, viongozi na benchi la ufundi Simba akisema anataka kuona kombe la Afrika likija nchini.

Rais Magufuli alisema kombe la ubingwa aliloikabidhi timu hiyo linapaswa lizalishe vikombe vingine vya klabu Afrika ili kesho aitwe kama si kukabidhi basi kupokea kombe jingine kubwa zaidi.

Ni maneno mafupi lakini yanabeba ujumbe mzito ambao Simba inatakiwa kuupokea na kuufanyia kazi katika michuano hiyo mikubwa kwa klabu Afrika. Yanamaanisha kwamba inatakiwa kuanza sasa kujiandaa kwa michuano hiyo kwa kila hali.

Viongozi wa timu hiyo kongwe wanapaswa kuipokea kauli ya Rais kama deni ambalo kulilipa kwake ni kupata mafanikio katika michezo hiyo ya Afrika na ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, inayosimamiwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Kila mwanaSimba anapaswa kushangilia ushindi huo ambao timu hiyo iliukosa kwa mitano na ndani ya misimu minne, lakini wakati wakifanya hivyo, wakumbe deni hilo na kujiwekea mikakati ya kulilipa.

Ni wakati sasa kwa viongozi wakiongozwa na benchi la ufundi kutengeneza kikosi mapema. Sifa ya wanaostahili kuwamo katika kikosi hicho iwe uwezo wa kushindana Afrika.

Iangaliwe wapi pa kufumua, wapi pa kuongeza, lakini si kufumua kikosi kizima na kuanza moja.

Kwa wachezaji wa Simba, baada ya kutwaa ubingwa nao wanapaswa kufahamu kuwa wana deni kubwa mbele yao. Wamemaliza ligi na kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara, lakini kazi kubwa inayowasubiri iko katika michuano ya Afrika inawasubiri ndani ya miezi sita ijayo.

Kutwaa ubingwa wa Afrika si kazi rahisi, hivyo wachezaji wajiandae, wajifue wenyewe na kuongeza ushindani kikosini kwani kwa kufanya hivyo, watajihakikishia nafasi kikosini lakini pia fursa ya kuonwa na maskauti wanaosaka vipaji kwa ajili ya timu kubwa. Lakini si hilo tu kwani kadri watakavyofika mbali kwenye michuano hiyo, ndivyo watakavyopata fedha zaidi.

Hivyo, wakati tukiipongeza Simba kwa mafanikio iliyopata, tunaitaka itafakari hotuba ya Rais na kuichukulia kama hamasa ya kufanya vizuri Afrika.

Kadhalika, kauli hiyo ya Rais iwe chachu katika maandalizi ya wawakilishi wengine wa Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho kati ya Singida United au Mtibwa Sugar.