Simiyu siyo pamba tu; Kuna choroko, mbaazi, dengu

Muktasari:

  • Taarifa ya mkuu wa mkoa huo inasema kwa mwaka Simiyu inazalisha tani 70 za pamba iliyo bora ambayo ni wastani wa zaidi ya asilimia 40 ya pamba yote inayolimwa nchini.

Simiyu ni miongoni mwa mikoa michanga nchini. Ulianzishwa mwaka 2012 baada ya kumegwa kutoka Shinyanga kwa upande wa mashariki.

Kwa kiasi kikubwa unategemea kilimo kwani kinachangia takribani asilimia 75 ya pato na zao kuu la biashara ni pamba likifuatiwa na mengine kama dengu, choroko na mbaazi.

Hivi karibuni Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba aliwapa ‘mtonyo’ wa maana wakulima wa na wananchi wa mkoa huo. Unajua aliwaambia nini? “Limeni kwa wingi dengu, choroko na mbaazi kwa sababu Serikali ya India kupitia kwa Waziri Mkuu, Nahendra Modi aliyezuru nchini hivi karibuni imesema inahitaji kati ya tani milioni sita hadi nane za choroko, dengu na mbaazi.”

Inazalisha karibu nusu ya pamba yote nchini

Taarifa ya mkuu wa mkoa huo inasema kwa mwaka Simiyu inazalisha tani 70 za pamba iliyo bora ambayo ni wastani wa zaidi ya asilimia 40 ya pamba yote inayolimwa nchini.

Kufufua kilimo cha pamba

Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini alisema kuna maofisa ugani 261 waliopangwa kwenye kata na vijiji ambao sasa wanasimamiwa kikamilifu ili kutimiza majukumu yao ya kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wakulima.

“Tumewekeza kwenye kilimo kwa vitendo ndiyo maana tunahakikisha wataalamu wetu wapo kila kona, tutakuwa mfano katika ukanda huu,” anasema na kuongeza kuwa Serikali imekusudia kutatua kero za wakulima wa pamba na kuwakikishia mazingira mazuri ya uzalishaji ikiwa ni pamoja na kupata mbegu bora, dawa na bei nzuri.

Mimea jamii ya mikunde

Katika siku za usoni, kilimo cha mbaazi, choroko, dengu, kunde, kitakuwa zao kuu la biashara hasa baada ya Tanzania kuingia makubaliano rasmi na India kuwa mnunuzi mkuu wa mazao hayo.

Zinahitajika tani milioni sita na Simiyu imeahidi kutoa asilimia 60 kati ya hizo ambazo ni wastani wa tani 3,600,000 kuanzia mwaka ujao.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka alisema moja ya vipaumbele vyake ni kilimo na kwamba jicho limeelekezwa katika soko hilo la India.

“Tunataka kuitumia fursa hii vizuri, tumeshajipanga kuhakikisha Simiyu inauza mazao ya jamii ya kunde kwa asilimia 60 kati ya zile tulizotakiwa kupeleka India,” anasema Mtaka.

Mimea na mazao jamii ya mikunde kwa miaka mingi imekuwa ikitumika kibiashara na mahitaji ya soko la ndani na hata nje yamekuwa yakiongezeka kila mwaka.

Sababu kubwa ni uelewa wa watumiaji hasa lishe bora (protini) inayopatikana kwenye mazao hayo ambayo ni sawa na inayopatikana kwenye nyama na kikubwa zaidi ni kwamba mazao hayo hayana lehemu.

Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha Kitropiki (IITA) inasema tani milioni nne za choroko zinatumiwa duniani kote kila mwaka na kwamba mahitaji ni makubwa zaidi.

Katika Afrika pekee, asilimia 70 ya kiwango hiki kinaliwa. Choroko, ambazo zilipuuzwa kwa miaka mingi na kusababisha uzalishaji kuwa mdogo na uhaba wa masoko, zimerejea kwa kasi ya ajabu kwa sababu ya kubainika kuwa na kiasi kikubwa cha protini, uwezo wake wa kukua katika mazingira ya mabadiliko ya tabianchi.