Sioni ubaya wa msomi kuuza nyanya au chapati

Muktasari:

  • Si mara ya kwanza, na mshangao wetu ulitakiwa kuishia kwenye tukio la Julai 13, 2014 la watu zaidi ya 10,000 kufurika Uwanja wa Taifa kufanya usaili wa nafasi 70 za kazi zilizotangazwa na Idara ya Uhamiaji.

Hakuna sababu ya kushangaa mkusanyiko wa watu 30,000 waliofika kufanya usaili kwa ajili ya nafasi 400 za ajira zilizotangazwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA).

Si mara ya kwanza, na mshangao wetu ulitakiwa kuishia kwenye tukio la Julai 13, 2014 la watu zaidi ya 10,000 kufurika Uwanja wa Taifa kufanya usaili wa nafasi 70 za kazi zilizotangazwa na Idara ya Uhamiaji.

Tatizo la ajira hasa kwa vijana liko takribani kote duniani, tofauti ni kwamba hapa kwetu limetegeshwa kama bomu ambalo mtegaji amepoteza uwezo wa kulitegua.

Hata viongozi wa Serikali na wanasiasa wameonyesha kuguswa na mkusanyiko huo wa kuwania nafasi chache za ajira na kutumia mitandao ya kijamii kutoa maoni yao.

Katika akaunti yake ya Instagram, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk Hamis Kigwangala aliweka picha ya mkusanyiko huo na kuweka ujumbe uliochochea mjadala.

Alihoji kwa kusema “je, hii inaashiria ukubwa wa tatizo la ajira nchini ama ni kwamba watu wetu wanachagua sana kazi za kufanya?” Ni hoja iliyopata mashambulizi kutoka kila kona kwa mtazamo hasi na chanya.

Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete naye hakuwa nyuma katika mjadala huo uliokuwa unagusa moja kwa moja changamoto za ukosefu wa ajira nchini.

Alisema: “Unaweza kudhani unauliza swali kumbe nawe unakuwa sehemu ya wachochezi.

“Mhe Waziri unaweza kuwa hujui kusoma lakini picha inatoa jibu sahihi. Kwamba lugha ya picha ilikuwa inaeleza kila kitu. Mamia ya vijana wanaopigana vikumbo kupata hata hiyo fursa ya kufanyiwa usaili na ofisa wa Serikali, achilia mbali ajira yenyewe.”

Hakuna kiongozi aliyekanusha maneno hayo kwenye akaunti zinazoonyesha majina yao na kusambaa kwenye mitandao tofauti ya kijamii, hakuna shaka hicho ndicho walichoandika.

Wakati wa usaili huo, Naibu Katibu wa Sekretarieti ya Ajira anayeshughulikia udhibiti na ubora, Humprey Mnyachi alisema wingi huo haumaanishi kwamba watu hawana ajira.

Alisema inawezekana wengi wanafanya kazi kwenye taasisi binafsi na leo wamekusanyika kwa kuwa wanatamani kupata ajira serikalini. Huu ni ukweli unaotakiwa kutiliwa shaka.

Ni kwamba watu wengi wana kazi, lakini hawana ajira kwa maana halisi ya kazi. Hili ni kundi linaoongezeka kila siku likiwa na shahada zao nyumbani.

Ni kundi la wahitimu wa vyuo vikuu ambalo bado lina ndoto ya kupata ajira serikalini kwa kuwa huko walipopitia mfumo haukuwaandaa kama wasomi wa kutumia ujuzi wao kutengeneza ajira kwa wengine.

Ni mfumo unaomuandaa mtaalamu wa kilimo kuona ana haki ya kwenda kuhudumia shamba la mkulima kama ofisa wa serikali na sio kuwa na shamba lake la mfano nyumbani.

Katika taasisi na mashirika binafsi sio wahitimu wote wanaopata ajira.Kundi kubwa linalobaki nje linatakiwa kutumia usomi wao kuyatawala mazingira kwa kuonyesha jambo tofauti kama wasomi. Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati wa hotuba ya mapitio ya mwelekeo wa kazi za serikali na makadilio ya mapato na matumizi ya kazi za Ofisi yake na Bunge hadi Marchi 2017, jumla ya ajira 418,501 zilikuwa zimezalishwa.

Alisema ajira 239,017 zilizalishwa na sekta binafsi huku sekta ya umma ikiwa ni pamoja na miradi ya maendeleo zikipatikana ajira 179,484.

Pamoja na changamoto zinaoikabili sekta binafsi ikiwemo kuyumba kwa mitaji na masoko,bado ndilo kimbilio kubwa la ajira wakiwemo wahitimu wa vyuo vikuu.

Ukweli ni kuwa msomi anayeuza nyanya, uwezo wake wa kuyatawala mazingira na kuzifikia fursa za kibiashara zilizopo mbele yake ni mkubwa zaidi kuliko aliyekaa tu.

Katika zama hizi ambazo ushindani wa nafasi za ajira unaongezeka kutokana na tofauti ya ubora na ongezeko la vyuo mbalimbali hakuna tena kazi ndogo kwa msomi. Hakuna miujiza yoyote iliyokuwa inafanywa na mchoma chapati kijana kutoka nchini Uganda aliyekuwa anashiriki maonyesho ya sabasaba mjini Bukoba hivi karibuni.

Amesoma kama vijana wengi wa nchi hii na kukosa ajira.Alijitofautisha na wauza chapati wote unawajua mjini Bukoba kiasi cha banda lake kufurika muda wote.

Alikuja na vifaa vichache vya kazi kutoka Uganda akiambatana na wafanyakazi wawili. Ngano na mafuta walinunua Bukoba.Kwenye banda alionekana kama mjasiriamali msomi na sio msomi anayepoteza muda baada ya kukata tamaa ya kukosa ajira.

Hatua ya kwanza ni kukubali kuwa kuna tatizo kubwa la ajira.

Wakati Serikali ikitakiwa kuja na mpango unaojibu tatizo la mitaji na masoko, wewe anza na ulicho nacho ili ikiwezekana uuze nyanya au chapatti.

Phinias Bashaya ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Kagera-0767489094