Siri iliyopo katika unyonyeshaji

Muktasari:

  • Maziwa ya mama ndiyo chakula cha kwanza kwa kila mtoto anayekuja duniani. Maziwa ni kinga ya magonjwa mengi kwa mtoto

Mvua kubwa iliyonyesha kandokando ya ziwa katika jiji la Mwanza, imelifanya eneo la Soko Kuu kutawaliwa na tope kiasi.

Tulijipenyeza katikati ya mkusanyiko watu wanaofurika sokoni hapo na kupita eneo zilipo mboga za majani na hatimaye tukakutana na Fauzia Musa akimnyonyesha mwanawe pembeni ya nguzo ya meza ya kuuzia nyanya.

Sekunde kadhaa hivi anamaliza kumnyonyesha mwanawe na kumbeba mgongoni, ili apate fursa ya kumhudumia mteja aliye mbele yake.

Nilimsogelea na kumuuliza kama alikuwa amekula chochote, ili kuimarisha uzalishaji wa maziwa yake, alinionyesha sahani tupu na chupa ya maji akiashiria kuwa kwa hakika alikuwa amepata lishe kamili.

Fauzia (26), anatambua umuhimu wa lishe bora na unyonyeshaji licha ya kubanwa na shughuli zake.

“ Huwa nakuja naye kazini mtoto wangu wa miezi nane, ili kuhakikisha kwa kila anapohitaji kunyonya nafanya hivyo. Kliniki ninakohudhuria wauguzi wamekuwa wakitueleza kuhusu umuhimu wa maziwa ya mama kwa afya ya mtoto,” anasema katika hali ya unyenyekevu.

Jirani yake yupo Miriam Hassan ambaye humsaidia kuuza wakati anapokuwa akimnyonyesha mwanawe.

Anasema anatambua ni kwa nini mama anapaswa kunyonyesha ili afya ya mtoto iimarike. Na kwa kuwa anaelewa umuhimu wa mtoto kunyonya maziwa ya mama, mara zote amekuwa akizingatia kula kwa wakati.

Hata hivyo, kwa Mariam Seneda anayefanya kazi ya uhasibu jijini Mwanza, suala la unyonyeshaji kwake lilikuwa siyo jambo rahisi.

“Mtaalamu wa lishe alinieleza kuwa chakula nilichokuwa nakula ndicho kilinifanya maziwa ninayotoa kuwa makavu na hali hii ilisababisha mwanangu apate tatizo la kuhara.Kwa maana hiyo niliacha kunyonyesha mwanangu akiwa na miezi minne,” anasema na kumtuhumu dada wa kazi aliyekuwa haandai lishe bora.

Kwa nini kina mama wanatakiwa kunyonyesha?

Licha ya faida zinazopatikana kwa mtoto kunyonya maziwa ya mama, watu wengi hawafahamu uhusiano uliopo baina ya lishe bora, usalama wa chakula na unyonyeshaji.

Kulingana na utafiti wa watu na afya wa mwaka 2015-2016 ni asilimia 59.2 ya watoto wa Kitanzania wanaotegemea unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee. Hiyo inamaanisha kuwa asilimia 40 ya watoto hawanyonyeshwi.

Mtaalamu wa lishe na mratibu taasisi ya masuala ya lishe nchini (Panita), Jane Msagati anaeleza kuwa maziwa ya mama ndiyo chakula cha kwanza kwa kila mtoto anayekuja duniani.

“Kila mtoto anapaswa kunyonyeshwa maziwa ya mama bila kupewa kitu kingine katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo na unyonyeshaji huo unapaswa kuendelea hadi anapofikisha umri wa miaka miwili. Inahimizwa hivyo kwa sababu maziwa ya mama ndiyo chakula kamili kwa mtoto,” anasisitiza Msagati akiongeza kuwa jambo hilo linasisitizwa pia na Shirika la Afya Duniani(WHO).

Anaongeza: “Inaposemwa maziwa pekee ya mama, inamaanisha kuwa hakuna maji, glukosi au kitu kingine kinachopaswa kuongezwa.”

Kwa mujibu wa Msagati, suala la unyonyeshaji siyo tu lina faida kwa mtoto pia, lina manufaa kwa mama.

“Kwa mfano, Moshi kuna mtori ambao hupikwa baada ya ndizi kulainishwa na kuchanganywa na nyama na kufanya supu laini. Mwanza kuna supu ya samaki, ugali na mchicha. Bukoba kuna ntula, samaki na ndizi,” anasema akisisitiza haja ya wananchi kuvirejea vyakula vyao vya zamani.

Nafasi ya vifaa tiba

Dk Richard Rumanyika ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ya kinamama katika Hospitali ya Bugando anasema faida mojawapo ya kunyonya maziwa ya mama, ni mtoto kuamsha hisia zake na kuimarisha ufahamu saikolojia yake.

Anasema ndiyo maana wataalamu mara zote hufuatilia mwenendo wa unyonyeshaji wa kinamama kwa watoto wao.

“ Tunawaandaa kinamama kwa ajili ya kunyoshesha wakati wanakaribia kujifungua na hata baada ya kujifungua na mara zote tunasisitiza kuhusu umuhimu wa lishe bora,” anasema Dk Rumanyika

Kwa upande wake, Dk Shafiq Mohammed, ambaye ni Mkurugenzi wa Hospitali ya Msasani Peninsula ya Dar es Salaam, anasema mama anayenyonyesha watoto wake anajenga hali ya ukaribu kwa watoto wake.

“Watu wengi hawajui kwamba unyonyeshaji huwalinda watoto dhidi ya matatizo kama ya upumuaji na utafiti unaonyesha kwamba unyonyeshaji huwaepusha watoto kukumbwa na magonjwa sugu kama vile kisukari,” anasema na kuongeza kuwa katika hospitali hiyo wameanza kufundisha kinamama jinsi ya kuandaa chuchu zao wiki 28 kabla ya kujifungua.

Nini kifanyike

Msagati anasisitiza kina mama lazima wazingatie suala la lishe bora, muda wa kupumzika na kupata uungwaji mkono katika ngazi ya familia.

“Lishe bora inapaswa kujumuisha vyakula vya kawaida vinavyopatikana kama vile maharage ili kupata protini, mchicha kupata vitamini, ndizi kwa ajili ya wanga na maji,” anashauri akiongeza kuwa sera ya lishe na chakula ya mwaka 1992, sasa inafanyiwa mapitio na wizara ya afya ili iweze kujumuisha afya na lishe.

Kadhalika anasisitiza haja ya kuwepo kampeni kuhamasisha umuhimu wa unyonyeshaji kwa watoto na hatimaye kubadili fikra potofu zilizojengeka miongoni mwa jamii kuhusiana na suala hilo.

Pia, anasema maziwa ya ziada yanayopatikana madukani yanayotumiwa na kinamama wengi kwa ajili ya kuwapatia watoto wao, yapigwe marafuku ili watoto wapate fursa ya kupata maziwa ya mama pekee.

Anatoa wito akitaka kufanyika kwa utafiti zaidi ili kubainisha faida azipatazo mtoto anaponyonya maziwa ya mama.

Anasema iwapo hayo yatafanyika, suala la kunyonyesha litatambuliwa na hivyo kuwa sehemu ya utamaduni wa kawaida kwa Watanzania.

Kituo cha kimataifa cha waandishi (ICFJ) mradi maalum