Suala la Lissu lisitugawe, lituunganishe

Muktasari:

  • Kila chama, kabla ya kuanza kampeni, kilikuwa na utaratibu wa kukabidhi shughuli zao kwa Mungu ili abariki. Utaratibu huo upo hadi sasa.
  • Wagombea na wapambe wao walitumia kila mbinu kuhakikisha wanapata wafuasi wengi wa kupiga kura kuwezesha kupata ushindi. Baada ya kampeni kali na zilizogharimu fedha nyingi CCM ndiyo ilishinda na kuunda Serikali.

Katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 vyama vya CCM, Chadema, ACT, ADC, UPDP, Chauma, NRA na TLP vilikuwa na wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi na vilifanya kampeni za kistaarabu.

Kila chama, kabla ya kuanza kampeni, kilikuwa na utaratibu wa kukabidhi shughuli zao kwa Mungu ili abariki. Utaratibu huo upo hadi sasa.

Wagombea na wapambe wao walitumia kila mbinu kuhakikisha wanapata wafuasi wengi wa kupiga kura kuwezesha kupata ushindi. Baada ya kampeni kali na zilizogharimu fedha nyingi CCM ndiyo ilishinda na kuunda Serikali.

Katika siku za karibuni, tumeshuhudia mabadiliko kwa vyama vya siasa kuzuiwa kuendesha shughuli zao zilizoainishwa kikatiba na kuruhusiwa kwa Sheria ya Vyama vya Siasa. Polisi wameanza kuzuia vyama kufanya mikutano ya hadhara.

Pia, polisi wakaingia hata kuzuia vikao vya ndani vya chama kwa madai kuwa ni “mikusanyiko isiyo halali” na matamshi ya viongozi kupinga au kulaani jambo fulani yamekuwa yakitafsiriwa kuwa ni “uchochezi”.

Hali ilivyo sasa ni kwamba hata mikusanyiko yenye lengo la kuomba kwa Mungu amani, utulivu na uponyaji kwa waliojeruhiwa inapigwa marufuku. Tumejaribu kujiuliza maswali mengi, lakini tumeshindwa kupata majibu.

Hivi ni kosa kukusanyika kufanya maombi? Tunafahamu Wakristo hufanya maombi katika ibada zao makanisani na Waislamu hufanya swala misikitini lakini pale wanapotaka kushirikiana kwa jambo kubwa la maombi yanayoshirikisha watu wa dini zote mahali sahihi huwa ni kwenye eneo kubwa la wazi.

Mwishoni mwa wiki, vijana kadhaa wa dini na vyama tofauti walipanga, wakatoa taarifa polisi juu ya kusudio lao la kukusanyika kwenye uwanja wa wazi kwa lengo la kumuombea mwanasiasa Tundu Lissu, ambaye polisi wamethibitisha alishambuliwa vibaya na watu wasiojulikana.

Taarifa ya polisi ilidai watawasaka kuhakikisha wasiojulikana wanajulikana. Wakati polisi wakiendelea kuwasaka, baadhi ya vijana waliamua kumuombea Lissu uponyaji wa haraka kwa Mungu.

Katika hili tulidhani polisi na vijana hao wana lengo moja, maana ikiwa atapona ataweza kusaidia polisi kuwataja wahusika au kusaidia upelelezi kwa njia yoyote ile ili polisi waweze kuwakamata, kuwahoji na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Viongozi wa Serikali siku zote huwa wanatoa wito kwa wananchi waombewe kwa Mungu. Kwa nini linapokuja suala la kuombea uponyaji kwa aliyejeruhiwa unaonekana ni uhalifu?

Sisi tunadhani katika hili, angalau watu wanaotaka kufanya maombi wangeachwa kufanya lakini kwa kufuata taratibu na bila kuvunja sheria za nchi.

Kama wanaoamini kuwa kwa kufanya maombi, mtu anayeumwa atapona basi waachwe wafanye wanachokiamini badala ya kuwazuia.

Badala ya polisi kuzuia maombi hayo kutokana na mikusanyiko, sisi tunadhani ifike mahali polisi wawe wanailinda mikusanyiko hiyo badala ya kutafuta suluhisho rahisi la kuikataza.

Huku tukitaka mambo yawe hivyo, tungependa pia kuchukua nafasi hii kuwasihi wananchi kuheshimu sheria na mamlaka kwa kutekeleza maagizo yake.

Amani tuliyonayo ni kitu adimu sana, nchi nyingi zimejikuta katika matatizo makubwa kwa sababu ya kukosa amani, na sehemu mmojawapo ambayo itatufanya tuwe na amani ni kwa wananchi kuheshimu sheria za nchi pamoja na mamlaka zake.

Badala ya pande mbili kuonyeshana umwamba au ubabe ni vyema yanapofikia baadhi ya mambo kuwe kunafanyika mawasiliano ya mara kwa mara ya pande zote ili kukubaliana kwa manufaa ya nchi.