Suala la sukari ya Zanzibar lifike kikomo

Hivi karibuni Serikali ilitoa ufafanuzi kuhusu malalamiko ya kiwanda cha kuzalisha sukari cha Zanzibar (ZSFL) kinacholalamikia kuzuiwa kuuza sukari yake upande wa Tanzania Bara.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas alitoa ufafanuzi huo kufuatia habari zilizoandikwa na vyombo vya habari likiwamo gazeti la Mwananchi kuhusu malalamiko hayo.

Dk Abbas alijikita zaidi kwenye takwimu za uzalishaji wa sukari upande wa Bara na Zanzibar ili kujenga hoja yake akikitaka kiwanda hicho kuuza sukari yake kwa soko la Zanzibar ambalo halijatoshelezwa.

Alisema takwimu za mahitaji ya sukari kwa Zanzibar kuwa ni tani 17,000 hadi 20,000, wakati uzalishaji unaofanywa na ZSFL ambacho kiwanda pekee visiwani humo ni tani 8,000, hivyo kuwepo kwa nakisi ya tani 9,000 hadi 12,000.

Kwa Tanzania Bara, alisema mahitaji ya sukari ni tani 630,000 ambapo kati ya tani hizo tani 485,000 ni kwa matumizi ya kawaida na tani 145,000 ni kwa matumizi ya viwandani. Hata hivyo, alisema wazalishaji wote wa ndani, Tanzania Bara wanazalisha jumla ya tani 306,226 zote ni kwa matumizi ya kawaida.

Kutokana na takwimu hizo, Dk Abbas alisema kiwanda cha ZSFL kina kila sababu ya kuendelea kuuza sukari yake Zanzibar badala ya kufikiria kuileta Bara.

Pamoja na takwimu hizo, mimi naona ushahidi wa takwimu uliotolewa na Serikali hautoshelezi kujenga hoja.

Naona kwa mtazamo huo, Serikali hawatendei haki Wazanzibari waliowekeza mitaji yao kibiashara wakitafuta fursa za masoko nje ya mipaka ya visiwa hivyo hasa Tanzania Bara.

Ningeshauri ufanyike utafiti wa kutosha ikiwa pamoja na kutembelea kiwanda hicho ili kuona hali ya uzalishaji na masoko yalivyo, ndipo utolewe msimamo wa Serikali.

Mgogoro huu ni wa muda mrefu ambapo awali ilidhaniwa kuwa kiwanda hicho hakizalishi sukari bali kinaiagiza kutoka nje ya nchi na kufungasha.

Ndipo baadhi ya taasisi za Serikali zilipofanya utafiti na kujiridhisha ili kuepuka sukari ya magendo kuuzwa Bara bila kulipiwa kodi.

Hata hivyo, licha ya kujiridhisha sukari ya kiwanda hicho imeendelea kuzuiwa kuuzwa Bara kwa visingizio kemkem.

Tatizo kubwa linalolalamikiwa na wenye kiwanda hicho ni masoko. Bei ya sukari ya Zanzibar iko chini ukilinganisha na bei ya Bara. Kwa mfano, mfuko wa kilo 50 kwa Zanzibar unauzwa Sh65,000 hadi Sh70,000, wakati Bara unauzwa Sh115,000.

Wakati bei ya sukari ikiwa chini Zanzibar, gharama za uzalishaji katika kiwanda hicho uko juu ambapo mfuko mmoja unazalishwa kwa Sh83,000. Kwa hiyo wazalishaji hao wanalalamika kupata hasara ya Sh18,000 kwa kila mfuko.

Huu ni ukweli ambao ama Serikali haiujui au imeamua kuukalia kimya.

Sababu ya pili ni nakisi anayoizungumzia Dk Abbas kwa upande wa Zanzibar, ambayo inazibwa na sukari inayoagizwa na wafanyabiashara kutoka nje ya nchi. Ndiyo maana licha ya kuwa na upungufu wa zaidi ya tani 10,000, bado bei ya sukari visiwani Zanzibar iko chini.

Kutokana na hasara hiyo, ZSFL imekuwa ikiomba kupewa kibali cha kuuza sukari yake kwenye soko la Bara ambalo bei yake ni nzuri. Hapo tatizo liko wapi?

Ni kweli kwamba, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nayo ina jukumu la kuihakikishia masoko ZSFL, lakini kama Tanzania ni muungano wa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar, kuna sababu gani ya kuwekea vikwazo bidhaa za Zanzibar kuingizwa Bara?

Katika taarifa yake hiyo, Dk Abbas amekiri kuwapo kwa kampuni nne zilizopewa vibali vya kuagiza sukari kutoka nje ya nchi ili kuziba pengo la mahitaji ya sukari. Hapa napo suala la muungano linaibuka, kwa nini sukari isiagizwe kutoka Zanzibar?

Ikiwa muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar uliofikisha miaka 54 na unapigiwa chapuo kila siku kwa nini biashara hizi zinakuwa na vikwazo vingi? Kwa nini wafanyabiashara wa pande mbili wasiwe huru kuuza na kununua bila vikwazo vyovyote?

Utashangaa hata baadhi ya taasisi za Serikali zinazohusika na ubora zinazidisha vikwazo visivyo na msingi. Kwa mfano ulikuwa na malalamiko ya Wazanzibari ya kukataliwa kwa bidhaa za Zanzibar na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) wakati tayari zimeshapitishwa na Mamlaka kama hiyo Zanzibar (ZFDA).

Ni muhimu kutambua kuwa hivi sasa tukio katika soko huria, ingawa sio holela, hivyo kila mfanyabiashara apewe fursa ya kufanya utafiri wa gharama zake za usalishaji na kutafuta masoko ya biodhaa zake. Pale inabidi kumsaidia iwe ni kuongeza soko la bidhaa zake badala ya kudhibiti sehemu ya soko kama ilivyo katika suala sukari Zanzibar.

Kuzuia ZSFL kuuza sukari Bara kunasikitisha na kukatisha tamaa. Hivyo suala hili ni muhimu lifanyiwe kazi.

0754 897 287