TCU ijitathmini inapofanya uhakiki huu wa wanafunzi wa elimu ya juu

Muktasari:

  • Baada ya kuwabaini, imewasilisha orodha ya majina ya wanafunzi hao katika vyuo husika na kuwataka wanafunzi wanaoendelea na masomo kwenye vyuo vya elimu ya juu kutazama matokeo ya uhakiki wao kupitia kiunganisho (link) ilichokibainisha katika ripoti yake.

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imeutangazia umma kwamba kazi ya uhakiki wa sifa za wanafunzi wanaoendelea na masomo kwenye vyuo vya elimu ya juu nchini kwa mwaka wa 2016/2017 imekamilika kwa baadhi ya vyuo na kubaini kuwa kuna wanafunzi waliodahiliwa katika programu ambazo hawana sifa.

Baada ya kuwabaini, imewasilisha orodha ya majina ya wanafunzi hao katika vyuo husika na kuwataka wanafunzi wanaoendelea na masomo kwenye vyuo vya elimu ya juu kutazama matokeo ya uhakiki wao kupitia kiunganisho (link) ilichokibainisha katika ripoti yake.

TCU imewataka wote ambao majina yao yatakuwa yameorodheshwa, wawasiliane na vyuo vyao ili kuthibitisha sifa zao kabla ya Februari 28, vinginevyo hawatatambuliwa na TCU hivyo kukosa sifa za uanafunzi.

Tumesikitishwa na mambo kadhaa kuhusu tangazo hilo. Mosi, uharaka wa kuthibitisha sifa hizo hasa ikizingatiwa kwamba tangu jana baada ya kusambaa kwa taarifa hizi, mtandao wa TCU wa www.tcu.go.tz umezidiwa hivyo huenda baadhi wakashindwa kufanya hivyo kutokana na tatizo la kiteknolojia.

Lakini pili, tumeshangazwa na hatua hii ya TCU kwa kuwa Julai mwaka jana, ilitangaza utaratibu mpya kwa watahiniwa wa mwaka mpya wa masomo wa 2016/2017 wanaochukua shahada, utaratibu ambao ulikuja miezi miwili tangu kuondolewa kwa watendaji waandamizi Tume hiyo kutokana na kudahili wanafunzi wasio na sifa na kusababisha kupewa mikopo na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

Utaratibu huo mpya uliainisha sifa na vigezo vipya vya wanafunzi wanaopaswa kudahiliwa katika vyuo, lakini tangazo hili limewagusa nao pia.

Tunadhani kwamba suala hili lilipaswa kufanywa kwa utaratibu ambao hautakuwa na usumbufu kwa wanafunzi hawa hasa wale wa mwaka wa kwanza ambao walipita katika chujio la Tume hiyo na wazazi pamoja na HESLB kuingia gharama kubwa.

Lakini pia utaratibu huu unaondoa utulivu wa wanafunzi kwa kuwa wanakuwa katika hali ya wasiwasi wa kuondolewa vyuoni hasa wakati huu wanapojiandaa na mitihani ya kumaliza mwaka, hivyo kuwepo na uwezekano mkubwa wa kuathirika kimasomo.

TCU inapokwenda mbele na kurudi nyuma, inayumbisha pia mipango ya wanafunzi na wazazi kimaisha.

Tunaishauri TCU kufanya kazi yake kwa weledi, umakini na uhakika ili kuepuka kutumia fedha chache zilizopo kufanya kazi moja mara mbili na kuvuruga mipango ya wengi.

Hawa vijana wanahitaji kutulia na kupanga mambo yao na hivyo TCU inapokuwa makini inawasaidia kuwa na uhakika na mipango hiyo na kutumia vyema rasilimali chache walizonazo kutengeneza maisha ya baadaye.