UCHAMBUZI: TFF ijitathmini hii habari ya kufungia wadau vifungo vya maisha

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), linaongozwa na Rais Wallace Karia aliyeshinda kiti hicho katika uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 12, 2017 mkoani Dodoma.

Kama ulivyo uchaguzi mwingine, haikuwa kazi rahisi Karia kushinda, alipambana kuhahakisha anawashinda wapinzani wake akiwemo aliyekuwahi kuwa katibu mkuu wa TFF, Frederick Mwakalebela.

Wagombea wengine waliochuana na Karia katika uchaguzi huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mtakatifu Gasper ni Shija Richard, Ally Mayay, Emannuel Kimbe na Imani Madega.

Kimsingi ulikuwa uchaguzi uliovuta hisia za wadau wa soka ambao walikuwa na kiu ya kutaka mabadiliko baada ya kuona baadhi ya mambo ndani ya taasisi hiyo nyeti hayaendi vizuri.

Pamoja na kutaka mabadiliko, wadau wa soka walitaka kuona mpira wa miguu unapiga hatua hasa baada ya kupata viongozi thabiti ambao wataleta mageuzi na kurudisha hadhi ya mchezo huo nchini.

Itakumbukwa mara ya mwisho Tanzania kupata mafanikio makubwa katika soka ilikuwa mwaka 1980, Taifa Stars ilipokata tiketi ya kushiriki Fainali ya Kombe la Mataifa Afrika mjini Lagos, Nigeria.

Fainali hizo zilikuwa za kwanza na mwisho kwa Tanzania, ni miaka 38 sasa Taifa Stars haijawahi kushiriki mashindano hayo yenye hadhi katika soka ya Afrika.

Mbali na timu za Taifa, hatuna cha kujivunia kwa upande wa klabu, timu zetu hasa Simba na Yanga zinazopokezana kukata tiketi kushiriki mashindano ya kimataifa, zimeshindwa kufua dafu. Pia hatuna mfumo bora wa kuibua na kuendeleza vipaji vya soka kuanzia ngazi za shule ya msingi hadi vyuo ambako kuna idadi kubwa ya wanamichezo ambao kama wangepata msingi imara Tanzania ingekuwa tishio katika medani ya soka kwa sababu vipaji vipo.

Haya ni baadhi tu ya mambo yaliyochagiza wadau wa soka kutaka mabadiliko ndani ya TFF wakiwa na matumaini kwamba ujio wa akina Karia angalau unaweza kupunguza kama sio kuondoa ombwe la kichwa cha mwendawazimu katika mashindano ya kimataifa.

Karia ametimiza mwaka mmoja na miezi minne tangu alipoingia madarakani hadi sasa, lakini tayari kumeibuka malumbano baina ya kamati za taasisi hiyo na baadhi ya wajumbe wake wa kamati ya utendaji.

Kamati ya maadili ya shirikisho hilo imepata umaarufu kutokana na adhabu za vifungo ambazo imekuwa ikitoa mfululizo licha ya uongozi huo kuwa madarakani kwa kipindi kifupi tu.

Adhabu kubwa ambayo kamati hiyo imekuwa ikitoa kwa wadau wake ni kifungo cha maisha kujihusisha na soka na wengine siyo chini ya miaka mitano kulingana na kosa.

Kamati ya Maadili ya TFF chini ya Wakili Hamidu Mbwezeleni tayari imeshusha rungu kwa kuwafungia kujihusisha na soka wadau wake tisa kwa madai ya kukosa uadilifu.

Wadau waliofungiwa maisha kujihusisha na soka ni pamoja na aliyekuwa makamu wa rais wa TFF, Michael Wambura. Pia rungu hilo lilitua kwa wajumbe wawili wa kamati ya utendaji, Mbasha Matutu na Dastan Nkundi, mwenyekiti wa Chama cha Soka Arusha (ARFA), Peter Temu na katibu msaidizi wake, Mwarizo Nassoro.

Fungia fungia hiyo haikumuacha salama aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya shirikisho hilo, Wakili Revocatus Kuuli ambaye alifungiwa maisha kujihusisha na soka.

Wengine ni mweka hazina wa ARFA, Omari Nyambuka na mjumbe wa kamati ya utendaji ya chama hicho, Hamisi Issah ambao wamefungwa kujihusisha na soka kwa miaka mitano na aliyekuwa meneja wa Simba, Robert Richard akifungiwa mwaka mmoja.

Kwa mujibu wa maelezo ya kamati ya maadili ya shirikisho hilo, vigogo wote hawa wamefungiwa kwa madai ya kukosa maadili ya kiutendaji wakati wakiitumikia taasisi hiyo.

Kimsingi, sitaki kuingilia uamuzi wa kamati ya maadili kutokana na adhabu ilizotoa kwa wadau wake, lakini najiuliza hivi hakuna adhabu mbadala zaidi ya kuwafungia maisha.

Ulikuwepo uongozi wa Leodegar Tenga, Jamal Malinzi, hatukuwahi kushuhudia kasi kubwa ya kufungia maisha wadau wake kama ilivyo sasa ambapo Karia ana mwaka mmoja na miezi mine tu, lakini tayari zimeibuka vurugu zinazotishia ustawi wa soka letu. Tayari baadhi ya wadau waliofungiwa wamekwenda mahakamani kutaka tafsiri za kisheria kuhusu adhabu walizopewa na wameshinda, hii inaonyesha kuna tatizo kubwa ndani ya taasisi hiyo.

Fungia fungia ya kila kukicha haiwezi kumpa utulivu Karia na watendaji wake kufanya kazi kwa weledi kwa kuwa mara kwa watakuwa mahakamani au kwenye vyombo vya habari kujibu hoja zilizoibua mjadala. Abdallah Mweri ni mhariri wa michezo wa Mwananchi, anapatikana kupitia, [email protected]