TFF imekiona kilichotokea nchini Kenya?

Muktasari:

  • Kenya iliyokuwa imepewa uenyeji wa mashindano hayo yanatoshirikisha timu 16 iliondolewa nafasi hiyo baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji ya Caf kilichofanyika juzi huko Accra, Ghana.

Shirikisho la Soka Afrika (Caf) limeondoa uenyeji wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) kwa Kenya kutokana na kutoridhishwa na maandalizi yake.

Kenya iliyokuwa imepewa uenyeji wa mashindano hayo yanatoshirikisha timu 16 iliondolewa nafasi hiyo baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji ya Caf kilichofanyika juzi huko Accra, Ghana.

Uamuzi huo ulitangazwa mbele ya waandishi wa habari mara baada ya kikao hicho kilichoongozwa na Rais wa Caf, Ahmad Ahmad kumalizika. Caf ilisema hatua hiyo imefikiwa baada ya kuona maandalizi kwa ajili ya mashindano hayo yanasuasua.

Mashindano hayo ya timu 16 zenye wachezaji wa ligi za ndani yalipangwa kuanza kutimua vumbi Januari 12 hadi Februari 4 mwakani.

Wakaguzi wa Caf walitembelea Kenya kuanzia 11 hadi 17 kuangalia maandalizi yanavyoendelea, lakini walikuta ni uwanja mmoja pekee kati ya vinne vinavyotakiwa kwa ajili ya mashindano hayo, ndiyo uliokuwa tayari kwa mechi zake.

Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) lilisisitiza kuwa lingefanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa mashindano hayo yanafanyika.

Lakini kutokamilisha viwanja kwa wakati kulitoa picha mbaya kwa Caf, ambayo haijatangaza mwenyeji mpya wa mashindano hayo badala ya Kenya.

FKF ilitoa taarifa yake juzi usiku ikionyesha masikitiko yake kwa kuondolewa mashindano hayo ambayo iliamini yangekuwa ya kihistoria kwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki.

Tanzania ndiyo waandaaji wa mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 (Afcon 2019). Tofauti na mashindano ya CHAN, Mataifa ya Afrika kwa vijana yanatumia viwanja viwili pekee.

Inawezekana kuonekana kuwa ni suala dogo kama ambavyo wengi tunadhani kwa sasa, lakini likawa baya kwa baadaye litakapofika shingoni. Tatizo lililotokea nchini Kenya si jambo la kupuuza kwa kuwaona wazembe, bali ni la kulichukua kama changamoto katika maandalizi yetu.

Ukisikiliza sababu za Kenya kutokarabati viwanja kwa muda unaotakiwa, utagundua kuwa jambo hilo lilisababishwa na bajeti ndogo ya fedha za Serikali yao na kutotoka kwa wakati.

Maandalizi ya mashindano makubwa kama haya hayaangalii sehemu moja ya kuchezea pekee, ingawa ndiyo kitu cha kwanza ambacho huangaliwa na Caf.

Tunaweza kuona kama 2019 ni mbali kwa ajili ya mashindano yatakayofanyika kwa viwanja viwili pekee.

Mashindano ya vijana yatakayofanyika nchini yatashirikisha timu nane pekee, uchache huu unaweza kuwa balaa na aibu kwa nchi kama hatutaanza mapema na kukimbia aibu kama iliyoikumba Kenya katika CHAN.

Naamini kuwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wameliona hili na kuona hatari ambayo inaweza kutukumba kama hatutakuwa na tayari kuonyesha kuwa tunataka heshima ya Afrika kupitia vijana.

Tayari tuna Uwanja wa Taifa, ambao bila shaka una sifa zote za kuchezewa mashindano makubwa kama hayo, lakini uwanja mwingine unatakiwa kuchaguliwa, kama ni CCM Kirumba wa Mwanza au mwingine.

CCM Kirumba ulishapitishwa na Caf kwa ajili ya michezo ya kimataifa, lakini 2019 kuna mwaka mzima wa Ligi Kuu kuchezwa katika uwanja huo.

Suala hapa ni utayari wa fedha kwa ajili ya marekebisho yatakayotakiwa, kwani kabla ya mashindano, Caf hutuma wakaguzi wao kuona kama kunahitajika marekebisho.

Naamini suala la viwanja viwili haliwezi kutushinda kama tutaamua mapema.

Linalowezekana leo lisingoje kesho.