Saturday, July 15, 2017

TUONGEE UJANA : Binti anaweza kuvuka vikwazo hivi

 

Katika karne hii tumeshuhudia baadhi ya wanawake waliopanda hadi ngazi za juu sana ulimwenguni kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya maendeleo ya binadamu.

Katika jamii zilizogubikwa na mila na desturi zilizowanyima wanawake fursa, hakuna aliyewahi kuwaza kuwa mwanamke kutoka barani Afrika angeweza kupanda hadi kushika wadhifa mkubwa sana duniani kama Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Wala hakuna aliyewahi kuota kuwa mwanamke angeweza kupanda hadi kufikia wadhifa wa kuwa mgombea wa urais wa Taifa kubwa na tajiri sana duniani kama Marekani. Hivi leo tunaposikia kiongozi wa nchi fulani ni mwanamke kama Rais au waziri mkuu, si jambo la kushangaa kama ilivyokuwa zamani.

Katika zama zetu ambazo katika baadhi ya nchi bado zipo chembechembe za tamaduni zisizo rafiki kwa wanawake, wale wanaopiga hatua hadi ngazi za juu wanafanya kazi inayostahili sifa za pekee. Mara nyingi wanakuwa wamevuka vikwazo vya aina nyingi ili kufikia sifa kama nyota inayong’aa katika anga la giza.

Katika makala hii tunajadili kuhusu baadhi ya vikwazo ambavyo mwanamke hana budi kuviruka katika mbio zake za kuelekea ngazi za juu za mafanikio katika maisha.

Kukataa kukwazwa na kasumba ya zamani

Kwa vizazi kadhaa, wanawake barani Afrika na nchi nyingine za ulimwengu wa tatu wameathiriwa na mila na desturi ambazo zimekuwa zikiwaweka katika daraja la pili baada ya wanaume.

Walikuwa wakiwekewa mipaka ya mambo ambayo ni wanaume tu waliokuwa wakiruhusiwa kuyafanya. Hata katika nchi zile zilizokuwa na ukandamizaji mkubwa wa wanawake, leo wana uhuru ulioainishwa katika sheria za nchi. Mwanamke yuko huru kuamua aina ya elimu anayotaka na kuchagua aina ya kazi anayoona inafaa kwa kutekeleza malengo yake ya maisha.

Hata hivyo, bado kuna wanawake ambao mawazo yao bado yanaathiriwa na kasumba ya wakati uliopita. Hiki ni kikwazo kimoja ambacho mwanamke hana budi kukivuka katika safari yake ya kuelekea kwenye maendeleo yake. Hana budi kutambua mageuzi makubwa yaliyotokea katika hadhi ya mwanamke. Ni lazima atupilie mbali mzigo wa kasumba ambayo ilijengeka katika mawazo yake. Ahakikishe anaishi maisha ya kisasa huku akiwa na dhamira ya dhati ya kudhibiti maendeleo yake.

Kujenga uwiano kati ya mila na mtazamo mpya

Wanawake wengi hujitazama kama wahanga wa mkanganyiko kati ya mila na desturi na wimbi la maendeleo ya kimamboleo.

Tangu akiwa mwari, msichana anasikia kauli inayosema “wewe ni msichana, unapaswa kutii na kuafikiana na matakwa ya jamii yako”. Anapokua na kuolewa anasikia kauli nyingine ikisema “wewe ni mke au mama, unapaswa kuwa na akili na maarifa ya kuhakikisha unatoa malezi bora kwa mumeo na wanao. Kama mlezi unalazimika kuiweka familia pamoja na kubeba dhamana ya kuhakikisha kaya yako inatambua mila za ukoo na utamaduni wa Taifa.”

Pamoja na uvumilivu na usamehevu mwanamke ni lazima awe na busara ya kuweka uwiano mzuri kati ya wajibu wake kwa maadili ya kimila, kidini na kitaifa na mustakabali wa maendeleo ya maisha yake. Hii ina maana kwa wazazi na wakwe zake na jamii inayomzunguka asionekane mtovu wa mila na maadili.

Lakini, desturi na mila hizo azichanganue ili azitekeleze kwa kuhakikisha zisiathiri shughuli zake za kutafuta maendeleo yake, familia yake na jamii yake.

Itaendelea Jumamosi ijayo...

Na Abeid Sakara

-->