Taasisi za fedha ziwape kipaumbele wanawake, vijana

Muktasari:

  • Mwaka 1983, Grameen ilianza kutoa huduma za fedha na kufanikiwa kuwafikia watu wengi masikini na kuzalisha faida na kukuza mtaji ambao umeifanya kuwa na matawi mengi duniani.

Mapinduzi ya huduma za fedha kwa watu wa kipato cha chini yalianza baada ya kuanzishwa kwa benki ya Grameen nchini Bangladesh kutokana na ukame ulioathiri mazao na kipato cha wakulima miaka ya 1970.

Mwaka 1983, Grameen ilianza kutoa huduma za fedha na kufanikiwa kuwafikia watu wengi masikini na kuzalisha faida na kukuza mtaji ambao umeifanya kuwa na matawi mengi duniani.

Mpaka sasa hivi mamilioni ya watu wamenufaika na huduma za taasisi hii ambayo inaweza kuwa mfano mzuri kwa taasisi ndogo za fedha nchini kuinua maisha ya Watanzania na kuwaondoa kwenye lindi la umaskini.

Mwanzilishi wa benkii alikuwa na imani katika kuwainua wanawake kiuchumi kwa kuwapa nafasi ya upendeleo kwenye huduma. alichokuwa mwanzilishi huyo ni kwamba benki za biashara zimeelekeza nguvu zake kwa wanaume zaidi na kuwasahau wananwake.

Kwa msimamo huo, yeye na timu yake walithubutu kuanza kutekeleza hilo japokuwa wengi walikuwa na wasiwasi mwanzoni kutokana na imani ndogo kwamba wanawake hawana uwezo wa kumiliki fedha.

Baada ya muda fulani, wanawake nchini Bangladesh waliinuka na kuanza kuingia kwenye mifumo ya fedha haraka na kuwekeza katika maeneo tofauti ya kiuchumi.

Asasi ndogo za fedha zilikuwa mkombozi wao. Tanzania ina somo la kujifunza hapa kwa kuwapa nafasi wanawake kwenye huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi za fedha ili kuinua uchumi wa familia, kaya hata taifa.

Kugundua na kupeleka huduma hizo kwa watu wenye mahitaji zaidi ni muhimu kwa upanuzi wa taasisi husika. Kujitofautisha na benki za biashara nchini Bangladesh katika utoaji wa huduma, kuliipa nguvu Grameen hivyo kujiimarisha zaidi.

Grameen iliamini kuwa kundi kubwa la watu wenye kipato cha chini ndilo lina mahitaji makubwa ya huduma za fedha, hivyo ilikuwa ni lazima ielekeze huduma na ubunifu wao upande huo.

Taasisi ndogo za fedha nchini zinatakiwa kufikiria kuwafikia watu wenye kipato kidogo badala ya kuendelea kujaza huduma zake mijini na kuwasahau wenye fursa nyingi waliopo vijijini.

Kutokana na kundi kubwa la wananchi wa Bangladesh kutoelewa mambo ya fedha na matumizi sahihi wakati huo, ilikuwa ni lazima kutoa elimu kwa kuwafundisha maana, matumizi sahihi, mikopo midogo na urejeshaji wake.

Haikuwa kazi rahisi, lakini walifanikiwa kwa kiasi kwa kuwa wanawake wengi waliingia na kuachana na woga waliokuwa nao mwanzaoni. Mazingira haya hayana tofauti na hapa kwetu ambako kuna kundi kubwa la watu ambao bado hawana elimu sahihi ya masuala ya fedha.

Kugundua uwezo wa wajasiriamali wengi wadogo na kuhakikisha wanatoa ushauri wenye kuleta tija, ni jambo muhimu katika kukuza uchumi. Kila mtu ana chembechembe za ujasiriamali kwa kitu anachokipenda, hivyo kuhitaji uwezeshaji utakaofanikisha ndoto zake.

Hilo likifanyika wajasiriamali wengi wadogo watafanikiwa. Uwezeshaji huu utafanikiwa zaidi ukiongezewa elimu na ushauri wa mambo ya fedha kwa kundi hili hususan wanawake watakaosukumwa kuingia kwenye biashara na uwekezaji.

Ni lazima taasisi zetu zifanye haya. Sekta ya asasi ndogo za fedha inahitaji kuiga baadhi ya mambo kutoka Benki ya Grameen ili kiimarike na kukua ili kuwa mhimili kwa watu wenye kipato kidogo.

Mwandishi ni mtaalamu na mchambuzi wa taasisi ndogo za fedha. Kwa maoni na ushauri, anapatikana kwa namba 0657 157 122.