Taasisi ya Moi yazidi kuchanja mbuga katika matibabu ya kibingwa nchini

Muktasari:

  • Tangu kuanzishwa kwa matibabu hayo miaka miwili iliyopita, mafanikio yameonekana baada ya kuwatibu zaidi ya wagonjwa 314 kupitia utaalamu huo.

Mapinduzi katika tiba za kibingwa nchini yanazidi kufanikiwa baada ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa (Moi) kuanzisha matibabu ya kibingwa ya upasuaji wa magoti na mabega kwa njia ya matundu (Arthroscopy).

Tangu kuanzishwa kwa matibabu hayo miaka miwili iliyopita, mafanikio yameonekana baada ya kuwatibu zaidi ya wagonjwa 314 kupitia utaalamu huo.

Kufuatia kuanzisha huduma hiyo, Moi imefanikiwa kuokoa Sh2.8 bilioni ambazo zingetumika kuwapeleka wagonjwa hao nje ya nchi.

Daktari bingwa wa mifupa aliyebobea katika upasuaji wa matundu, Felix Mrita anasema baada ya mafanikio waliyoyapata kutokana na upasuaji wa goti, hivi sasa wamefanya upasuaji wa bega kwa wagonjwa 10.

“Upasuaji huu unahusisha matumizi ya hadubini maalumu inayoingizwa kwenye goti la mgonjwa kwa njia ya matundu, hali inayomfanya daktari arekebishe misuli na mishipa yenye hitilafu kwa kufuatilia kile anachokifanya kwenye runinga maalumu,” anasema Dk Mrita.

Anasema ikilinganishwa na upasuaji wa kawaida, aina hiyo ya matibabu huleta ufanisi mkubwa na kulifanya goti la mgonjwa kuwa salama na kupona kwa haraka.

“Kwa wanamichezo au mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji huu anaweza kurejea katika hali yake ya kawaida na kushiriki michezo, kutembea au kukimbia bila tatizo ndani ya kipindi kifupi,” anasema Dk Mrita.

Mkurugenzi Mtendaji wa Moi, Dk Respicious Boniface anasema gharama za upasuaji huo kwa hapa nchini zinagharimu Sh3 milioni ikilinganishwa na nje ya nchi gharama zake ni Sh12 milioni.

Dk Boniface anasema taasisi hiyo imefanikiwa kupunguza rufaa za kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa asilimia 95 na asilimia 5 zilizobaki zinatarajiwa kumalizika kipindi kisichozidi miezi sita ijayo.

“Aina hii ya upasuaji inawanufaisha wanamichezo na watu wengine ambao kwa bahati mbaya hupata maumivu makali ya goti na kwa kipindi kirefu wamekuwa wakilazimika kufuata matibabu hayo nje ya nchi kwa gharama kubwa,” anasema Dk Boniface.

Anasema uanzishwaji wa aina hiyo ya upasuaji umefanikiwa baada ya taasisi ya Moi kuwapeleka madaktari wake bingwa wa mifupa nchini Misri kujifunza katika kipindi cha miezi sita hadi mwaka mmoja walikojifunza mbinu za upasuaji huo.

Namna upasuaji unavyofanyika

Dk Mrita ambaye ni daktari wa wanamichezo pia, anafafanua zaidi, mara nyingi wagonjwa wa michezo majeraha yao huwa ndani ya goti, hivyo kupitia matibabu hayo ni rahisi mgonjwa kupona kwa uharaka na kurejea uwanjani ndani ya mwezi mmoja.

“Zamani tulikuwa tunalifungua goti, lakini kutokana na teknolojia, tunatoboa mashimo matatu moja linaingizwa kamera na mengine vifaa kwa ajili ya upasuaji,” anasema.

Anasema walio wengi hupata majeraha katikati ya mkunjo wa goti kati ya mfupa wa paja na mguu hasa kukatika, hiyo husababisha mgonjwa kusikia maumivu kila akikunja goti na wakati mwingine akitembea huanguka.

Anasema mara nyingi mgonjwa akipimwa kwa kutumia kipimo cha X Ray hatagundulika ana tatizo gani hadi afanyiwe kipimo cha MRI.

“Tunapofanya upasuaji huu, tunaingiza hadubini na vifaa vingine viwili kwa ajili ya kufanya upasuaji ndani kwa ndani na kama pamekatika na inahitajika kupiga msasa tunafanya hivyo, mgonjwa anapona na anatembea kama kawaida baada ya muda mfupi,” anasema Dk Mrita.

Anasema wapo wagonjwa ambao hukatika misuli ya ndani, awali ilikuwa lazima kulifungua goti kwa ajili ya kuzitengeneza, matibabu hayo yaliwasababishia jeraha kubwa na kupona kwake ilichukua muda mrefe tofauti na sasa.

Dk Mrita anasema kwa upande wa vifaa, kila mgonjwa hutumia vyakwake, lakini si gharama kubwa kwa hapa nchini kwani iwapo ana bima hulipiwa.

“Tunasonga katika huduma hii na tangu mwaka jana tulianza kupasua bega, tumewafanyia wagonjwa 10 na wengi ni wacheza mpira wa mikono na wa kikapu na wagonjwa wa kisukari.

Moja kati ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji huo, mchezaji wa Timu ya Afya Club, Bakari Msongamwanja anasema baada ya kufanyiwa upasuaji huo Septemba mwaka jana, ilimchukua mwezi mmoja kurudi uwanjani.

“Baada ya upasuaji, nililazwa siku moja nikaruhusiwa nikawa nafanya mazoezi ya kuchezesha mguu, baadaye nilianza kukimbia taratibu na baada ya mwezi mmoja nimerudi uwanjani nacheza vizuri namba yangu ni 6,” anasema Msongamwanja.

Hemed Salehe mkazi wa Bagamoyo alipata tatizo la goti na baadaye alifanikiwa kufanyiwa upasuaji huo.

“Nilifanyiwa upasuaji na nilipta nafuu ndani ya siku mbili, nilirudi nyumbani nilikoendelea na mazoezi kwa siku kadhaa, lakini baada ya mwezi mmoja niliendelea na shughuli zangu kama kawaida.”