Taasisi za umma zilipe madeni ya Tanesco

Muktasari:

  • Hii ni kutokana na malimbikizo ya madeni linayodai kutoka kwa wateja, hasa taasisi na mashirika ya umma.

Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linapita katika wakati mgumu kiutendaji na kihuduma kutokana na upungufu wa fedha za kutekeleza miradi ya kusambaza huduma ya nishati ya umeme nchini.

Hii ni kutokana na malimbikizo ya madeni linayodai kutoka kwa wateja, hasa taasisi na mashirika ya umma.

Kwa mujibu wa Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani hadi wiki iliyopita, Tanesco ilikuwa ikidai zaidi ya Sh297 bilioni ya malimbikizo ya ankara za umeme kutokana na taasisi na mashirika ya umma.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Mwamashele wilayani Shinyanga, Dk Kaleman alitaja baadhi ya mamlaka za maji na usafi wa mazingira nchini kuwa miongoni mwa wadaiwa sugu wa Tanesco.

Alisema madeni haya yanakwamisha na kufifisha utendaji wa Tanesco katika utoaji wa huduma kwa wateja.

Kwa mfano alitaja deni la zaidi ya Sh2.2 bilioni ambalo Tanesco linaidai Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Kahama na Shinyanga (Kashwasa).

Malimbikizo ya madeni yamesababisha Tanesco kuzikatia huduma baadhi ya taasisi na hivyo kuathiri wananchi wanaotegemea huduma za taasisi hizo.

Kinachoshangaza ni kwamba Serikali na taasisi zake hutenga kwenye bajeti yake fedha kwa ajili ya malipo ya ankara za umeme, lakini deni linaendelea kulimbikizwa.

Nakumbuka katika moja ya hotuba zake akizindua baadhi ya miradi ya umeme nchini, Rais John Magufuli aliagiza Tanesco kutekeleza operesheni ‘Ka-Ta’ umeme kwa wateja wote wanaodaiwa malimbikizo ya ankara za umeme bila kujali hata kama ni ofisi yake.

Nadhani muda umefika kwa taasisi zote za umma zinazodaiwa malimbikizo ya deni Tanesco kulipa fedha hizo ili kuliwezesha shirika hilo kutimiza wajibu wake pia kuwaondolea adha ya huduma duni wateja binafsi wanaolipa ankara zao kwa wakati.

Ili kudhibiti ongezeko la deni, Tanesco iliyafungia mita za luku baadhi ya mashirika na taasisi zote zinazodaiwa ili matumizi yao ya sasa yalingane na malipo wanayofanya, juhudi ambazo zinatakiwa kuendelea na kuyafikia mashirika mengi zaidi na ikiwezekana yote yafikiwe.

Sambamba na hilo, juhudi za kuyabana mashirika na wateja wengine wanaodaiwa ziongezwe ili madeni hayo yakusanywe na kuongeza ufanisi na utendaji wa Tanesco na kuiwezesha kuwafikishia wananchi wengi zaidi umeme.

Pia juhudi na kupanua huduma hizi ziende sambamba na upanuzi wa miradi ya kupeleka umeme jijini kupitia mpango wa Rea.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Waziri Kalemani, hadi sasa ni vijiji 7, 800 kati ya 11, 183 vimefikiwa na umeme wa Rea.

Mpango huo unatarajiwa kutawaondolea asilimia zaidi ya 70 ya Watanzania wanaishi vijijini adha ya kutegemea nishati ya kuni, mkaa na mafuta taa, bali pia kutafungua fursa za kiuchumi kupitia uwekezaji kwenye miradi midogo na kati inayotumia nishati ya umeme.

Wananchi watafungua na kuendesha mashine za kusaga nafaka, kuchomelea vyumba na hata saluni ambazo ni kati ya maeneo yanayotoa fursa ya ajira kwa vijana.

Hii itafanikisha lengo la Serikali la kufikia Tanzania yenye uchumi wa kata kupitia maendeleo ya sekta ya viwanda ifikapo mwaka 2025.

Kamwe Tanesco isikubali lengo la ‘kuwasha’ vijiji vyote nchini kupitia mradi wa Rea na huduma bora ya Tanesco likwamishwe na malimbikizo ya madeni ya taasisi za umma. Wahusika wabanwe hadi walipe malimbikizo yote kwa sababu taasisi zao zinatenga fedha za kugharamia huduma za umeme kila mwezi. 0757 708 27