Tahadhari ya mafuriko ifanyiwe kazi

Mkurugenzi mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi

Muktasari:

  • Mkurugenzi mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi alisema juzi kuwa mvua hizo zinazotarajiwa kuwa za kiwango cha kupita wastani, zitakuwa katika mikoa inayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka, kama Dodoma, Kigoma, Tabora, Rukwa, Katavi, Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa, Ruvuma, Lindi, Mtwara na kusini mwa Morogoro.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewataka wananchi na sekta zinazojishughulisha na mazingira kuchukua tahadhari za kukumbwa na mafuriko kutokana na mvua za msimu zinazotarajiwa kuanza kati ya Novemba 2017 na Aprili 2018.

Mkurugenzi mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi alisema juzi kuwa mvua hizo zinazotarajiwa kuwa za kiwango cha kupita wastani, zitakuwa katika mikoa inayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka, kama Dodoma, Kigoma, Tabora, Rukwa, Katavi, Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa, Ruvuma, Lindi, Mtwara na kusini mwa Morogoro.

Dk Kijazi alisema miezi hiyo inatarajiwa kuwa na vipindi vifupi vya mvua kubwa zitakazosababisha mafuriko katika maeneo baadhi ya maeneo. Pia, zinaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa kutokana na uhaba wa majisafi na salama pamoja na kuwapo kwa mfumo hafifu wa majitaka.

Pia, Dk Kijazi aliwatahadharisha wadau wa sekta ya uvuvi, kilimo, mifugo, chakula na wanyamapori kwamba wanatakiwa kufuatilia kwa ukaribu taarifa za hali ya hewa, kwa kuwa kufahamu mapema kutasaidia kujipanga kukabiliana na hali hiyo bila kukurupushwa.

Tahadhari hiyo pia imetolewa kwa wachimbaji wadogo wa madini ambao wametakiwa kuwa makini kwa kuwa ongezeko la maji kwenye udongo linaweza kuchochea mmomonyoko wa ardhi na kusababisha maafa.

Tunaungana na wito wa TMA wa kuzitaka mamlaka za miji kuchukua tahadhari ya kukagua mifumo ya kupitisha maji ili ifanye kazi muda wote kuepuka kutuama na kusababisha mafuriko.

Pia, tunasisitiza wito wa TMA wa kuzitaka mamlaka za maafa na taasisi za uokozi kuchukua hatua stahiki katika utunzaji wa mazingira ili kupunguza athari hasi zinazoweza kujitokeza.

Uzoefu unaonyesha miaka iliyopita mafuriko yanayotokana na mvua yalisababisha madhara makubwa kwa binadamu; kuna waliopoteza maisha, waliopata magonjwa ya mlipuko na waliopoteza makazi yao.

Mafuriko hayo pia yalisababisha madhara ya kiuchumi kutokana na wengi kupoteza mali, maeneo ya uzalishaji kama vile mashamba kuharibika, hata wanafunzi waliathirika kwa vitabu, madaftari na sare zao za shule kusombwa na maji.

Tunaamini kwamba, pamoja na kuiomba Serikali na taasisi zake kuchukua tahadhari, wananchi nao wanapaswa kuacha kufanya shughuli kwenye njia za maji kama ujenzi au tabia ya kuchimba mchanga.

Ni wazi yanapotokea majanga kama ya mafuriko waathirika wakubwa ni wananchi, hivyo ni muhimu kwao kuwa wa kwanza kutekeleza maagizo ya watalaamu, hasa katika suala la utunzaji wa mazingira na kuepuka ujenzi holela kwenye maeneo ya mabondeni.

Wananchi wanatakiwa kufahamu kuwa maelekezo ya wataalamu na viongozi wao huwa yanatolewa kwa nia njema. Hivyo, haina maana kuweka vikwazo hasa pale watu wanapotakiwa kuondoka kwenye maeneo hatarishi kama hayo ya mabondeni.

Hivyo, tunaamini tahadhari iliyotolewa na TMA na maelekezo yatakayotolewa na viongozi wa Serikali yatazingatiwa na watu wote watakaoguswa. Haitakuwa na maana kama tahadhari itatolewa mapema lakini hatua za utekelezaji zikafanyika mwishoni tena kwa hali ya dharura.

Tunaamini wahusika wote watajipanga vizuri katika kuchukua tahadhari iliyotolewa na TMA, hatutarajii kuona Serikali na taasisi zake ikichelewa kuchukua hatua.

Pia tuna uhakika wananchi nao watatekeleza yale yanayowahusu bila kushurutishwa wala kutupiana lawama.