UCHAMBUZI: Tanga imeteleza wapi maambukizi ya Ukimwi?

Muktasari:

  • Mbali na kutafakari, wadau hao walikutana kwa lengo la kuweka mikakati ya kuyapunguza maambukizi ya virusi hivyo ambavyo havijapata kinga wala tiba.

Hivi majuzi wadau wa mapambano dhidi ya Ukimwi wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela walijifungia kwa siku tatu kutafakari wapi waliteleza hadi kusababisha maambukizi ya virusi hivyo kwa mkoa huo kuongezeka kutoka asilimia 2.4 hadi asilimia tano.

Mbali na kutafakari, wadau hao walikutana kwa lengo la kuweka mikakati ya kuyapunguza maambukizi ya virusi hivyo ambavyo havijapata kinga wala tiba.

Kwa mujibu wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Zena Said, hadi sasa bado wanakuna vichwa kutafuta kiini hasa cha kuongezeka haraka kwa maambukizi hayo ili kuweka mikakati itakayoyapunguza na kuokoa nguvukazi ya Taifa inayoteketea.

“Tunakuna vichwa maana tunashangaa nini kimetokea. Ni kukosewa kwa takwimu, ni kuporomoka kwa maadili, elimu juu ya njia za kujikinga na maambukizi imepungua au ni suala zima la kutofuata matumizi sahihi ya dawa za kufubaza virusi,” alisema Zena.

Akinukuu utafiti wa viashiria na matokeo ya Ukimwi nchini kwa mwaka 2016/2017, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Asha Mahita alisema maambukizi yamepanda kutoka asilimia 2.4 ya awali hadi tano na kuufanya Tanga kuwa miongoni mwa mikoa 11 yenye ongezeko la kasi la maambukizi hayo.

Utafiti huo wa kitaifa ulifanyika katika ngazi ya kaya kuanzia Oktoba 2016 hadi Agosti 2017 chini ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali - Zanzibar na ICAP Tanzania kwa kushirikiana na wadau wengine.

Wadau hao ni Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) na ya Zanzibar (Zac) pamoja na Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, Uhakiki, Ubora na Mafunzo (NHL-QATC); Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (NACP) na Kitengo Shirikishi cha Ukimwi, Kifua Kikuu na Ukoma, Zanzibar (ZIHTLP).

Pamoja na utafiti, wakati wa utekelezaji suala hilo zilitolewa pia huduma za ushauri nasaha, upimaji wa virusi vya Ukimwi na wa utoaji wa majibu.

Pia kulikuwapo na ukusanyaji wa taarifa za kaya na binafsi za wanakaya, upatikanaji wa huduma na matibabu kwa wanaoishi na maambukizi ya virusi hiyo.

Utafiti huu uliopima maambukizi mapya na kiasi cha virusi vya Ukimwi mwilini kwa wanaoishi na VVU, ni wa kwanza kufanyika nchini ambapo matokeo yake yanatoa taarifa katika ngazi ya Taifa na mikoa kwa ajili ya ufuatiliaji na udhibiti.

Mikoa mingine ambayo utafiti huo uliofadhiliwa na Serikali ya Marekani umeonesha maambukizi ya VVU kuongezeka ni Dodoma kutoka asilimia 2.9 hadi tano na Mwanza (asilimia 4.2 hadi asilimia 7.2) huku mikoa inayoongoza ikiwa ni Mbeya asilimia 9.2, Njombe 11.6 na Iringa asilimia 11.2.

Wakati mikoa mingine maambukizi ya VVU yanapungua, Tanga imeingia katika rekodi ya ile ambayo yanaongezeka kwa kasi ambayo imeleta mshtuko wa hali ya juu. Niwapongeze wadau wa masuala ya mapambano dhidi ya Ukimwi waliojifungia kuweka mikakati ya kuhakikisha maambukizi yanapungua huku nikiwaomba wasiishie tu kuweka mikakati, bali waendelee mbele katika kuitekeleza.

Matokeo haya yawe ni sababu ya wakazi wa Tanga kujitafakari na kubadilisha mienendo yao na kuangalia ni wapi waliteleza hadi kuwepo kwa ongezeko hilo.

Vitendo vinavyofanyika kwenye ngoma za vigodoro, kupuuza matumizi ya kondomu na kuporomoka kwa maadili katika jamii ikiwamo wimbi la wenye ndoa kuchepuka na vijana, ni wazi vimechangia ongezeko hili.

Maeneo hayo yote ni muhimu kuyasimamia vizuri huku wanaotumia dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi nao wakiangaliwa kwa kupewa maelekezo yanayofaa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha dawa zao zinapatikana muda wote.

Na hii isiwe kwa Tanga pekee, bali kwa mikoa yote iliyoonyesha kuathirika zaidi.

0658376434