Tanzania haihitaji siasa za kuchapana makonde

Muktasari:

  • Lakini sasa matukio haya yanaonekana kutaka kuwa kama ada. Ile dhana ya ushindani na uvumilivu wa kisiasa inaelekea kupotea nchini.

Sio desturi ya wanasiasa nchini kuhasimiana kiasi cha kufikia hatua ya kutwangana makonde. Kama yapo matukio haya, huwa ni kwa nadra.

Lakini sasa matukio haya yanaonekana kutaka kuwa kama ada. Ile dhana ya ushindani na uvumilivu wa kisiasa inaelekea kupotea nchini.

Kitendo cha madiwani wa Chadema, CUF na CCM kufikia hatua ya kushikana mashati juzi wakati wa uchaguzi wa naibu meya wa Manispaa ya Ilala, kinaashiria hali mbaya ya harakati za siasa nchini.

Kama tulivyoripoti jana, chanzo cha vurugu hizo kilitokana na madiwani wa upinzani kudai kuwapo kwa kura zilizoharibika, huku msimamizi wa uchaguzi akipinga madai hayo.

Ni kitendo kinachopaswa kupigiwa kelele na kila anayelitakia mema Taifa letu. Nasi hatumo nyuma katika hili. Tunawanyooshea kidole madiwani hawa na wanasiasa kwa jumla; tunawaeleza kuwa vitendo vyao haviwasaidii wananchi waliowachagua wala kuiletea nchi maendeleo.

Tulifikiri kama nchi tulishafika mbali katika safari ya demokrasia ya ushindani wa vyama vingi. Hata hivyo, hali haiko hivyo; kuna kila dalili kuwa safari hiyo bado ni ndefu, hasa linapokuja suala la uendeshaji wa chaguzi kwa misingi ya haki na uhuru.

Lakini kwa nini tumefika hapa? Watu wazima wanapofikia hatua ya kuchapana makonde tena hadharani, sio bure kuna jambo. Hili ndilo linalopaswa kufanyiwa kazi, vinginevyo tutaendelea kushuhudia vurugu kila uchaguzi unapowadia.

Wapo wanaoamini kuwa michakato ya uchaguzi nchini haipo sawa. Kuna upande ambao mara zote umekuwa ukipendelewa na mamlaka zinazosimamia shughuli za uchaguzi.

Aidha, kama sio mgombea kuzuiwa kufanya kampeni au kuwekewa mapingamizi hata yasiyo na maana, kuna atakayelalamika mawakala wake kutolewa kituoni. Mwingine atadai kura zilizopigwa hazioani na idadi ya watu walioandikishwa. Wapo pia wanaofikia hatua ya kudai vyombo vya dola vinaingilia uchaguzi. Msururu wa kero na vitimbi vya uchaguzi ni mrefu, na si vya leo wala jana. Ni kilio cha muda mrefu ambacho ni kama vile wahusika wameweka nta masikioni, hawataki kukisikia.

Ni kilio ambacho tunavyozidi kukidharau, tuna shaka kuwa pengine kinaweza kuzalisha makubwa zaidi kuliko makonde ya madiwani pale kwenye ukumbi wa Arnaoutoglou.

Ikiwa tumeikubali demokrasia, lazima tuwe tayari kukubali gharama na zake. Mojawapo ya gharama hizo ni kuhakikisha kuwa kila mshiriki sio tu anawekewa mazingira sawa ya kushiriki, bali kila mmoja anayaona mazingira hayo.

Tunadhani ipo haja ya kufanyika kwa tathmini juu ya hili kwani kama tulivyowahi kusema siku za nyuma taasisi husika zikomeshe vilio hivi vya kufanyiwa ‘rafu’ za uchaguzi kila mchakato huo unapofanyika. Badala yake tuone kila hatua hiyo inapomalizika, wagombea wanashika mikono na kupongezana na tukifanikiwa katika hilo, tutajinasubu kwamba tumepiga hatua katika suala zima la demokrasia.

Tanzania yetu haihitaji wanasiasa mahodari wa masumbwi. Tunataka wanasiasa walio hodari katika ujenzi wa hoja za ushawishi kwa wapigakura, wawajibikaji na wanaotekeleza mambo waliyowaahidi wananchi.