Monday, August 7, 2017

Tanzania ina fursa pana kwa ujenzi wa viwanja

 

By Allan Goshashy

Kutokana na sababu za kihistoria, wananchi wa Tanzania hawakushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi kabla ya uhuru, kwa kuwa walinyimwa fursa.

Hali hii ilikuwepo wakati wa ukoloni na wananchi wengi waliwekewa vikwazo kushiriki katika uchumi ili watawalike kirahisi.

Wananchi walilazimika kujishughulisha na uchumi wa sekta isiyo rasmi wakati sehemu kubwa ya sekta rasmi ilishikwa na watawala wa kikoloni na wageni.

Wakoloni walitumia mbinu mahsusi kuwaendeleza wazungu na wananchi wachache. Mbinu hizo ni pamoja na utoaji wa mikopo, utoaji wa elimu, ugawaji wa ardhi na utoaji wa leseni za biashara.

Baadhi ya mbinu hizo zinaweza kutumika hivi sasa kurekebisha hali hiyo na kuwawezesha wananchi kumiliki sehemu kubwa ya uchumi.

Uhuru ulipopatikana mwaka wa 1961, wananchi walipata madaraka ya kisiasa, lakini sehemu kubwa ya uchumi bado ilibaki mikononi mwa wageni na baadhi ya Watanzania.

Hali hiyo ilileta kero na ni mojawapo ya sababu muhimu ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha, mwaka wa 1967. Azimio hilo lilikuwa mkakati muhimu wa kuhakikisha kwamba wananchi kwa pamoja kupitia dola wanashika njia kuu za uchumi. Shughuli zote za uzalishaji na utoaji wa huduma ziliundiwa mashirika ya umma.

Hata hivyo, mashirika ya umma mengi yaliendeshwa kwa hasara na yaliendesha shughuli za kiuchumi kwa kutumia mtaji na ruzuku kutoka Serikalini.

Mwaka wa 1992, Sera ya Ubinafsishaji ilianzishwa na Serikali baada ya kuona kwamba mashirika ya umma yalikuwa mzigo kwa Serikali ambayo haikuwa na fedha za kuyaendesha na kuyaendeleza hata kufikia uamuzi wa kuyarekebisha na mengine kuyabinafsisha.

Katika ubinafsishaji huo, sehemu kubwa ya wananchi hawakushiriki ipasavyo katika zoezi hilo kwa kuwa hawakuwa na elimu ya biashara, ujuzi na mitaji.

Pia, mwaka 1992 Tanzania iliingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa hivyo kuondoka katika mfumo wa kuwa chini ya chama kimoja cha siasa ambacho ni Chama cha Mapinduzi (CCM) kilichokuwa na dhamana ya kuunda Serikali na mpaka sasa kina dhamana hiyo.

Baada ya kuingia katika mfumo wa vyama vingi, ilibidi mali za Serikali na CCM zitenganishwe hivyo viwanja vyote vya michezo vilivyopo mikoani vilivyojengwa wakati nchi yetu ilipokuwa ikiongozwa na chama kimoja vilihodhiwa na CCM na mpaka sasa bado vipo chini ya CCM.

Siyo mbaya, ila kwa mtazamo wangu umefika wakati sasa viwe na utaratibu mpya wa usimamizi kwa ajili ya kusaidia Watanzania wengi, viwanja hivi wapewe watu binafsi kuviendeleza kwa manufaa ya umma.

Athari kubwa ya viwanja hivyo kumilikiwa na chama cha siasa ni kwamba haviendelezwi na hivyo hali yake kubaki duni, majukwaa yake yamechoka, sehemu ya kuchezea ni mbovu, hali ya vyoo ni mbaya huku vikiingiza mapato kidogo kwa sababu ya kukosekana ubunifu wa kuviendesha.

Ndiyo, pia umefika wakati sasa kwa watu binafsi wenye uwezo na nia wajitokeze kuomba dhamana ya kuviendesha viwanja hivi vinavyomilikiwa na CCM.

Vilevile, watu binafsi wenye uwezo wa fedha na mali hapa nchini wanaweza kuchangamkia fursa kubwa iliyopo nchini ya kujenga viwanja vya michezo vyenye hosteli na kumbi zenye sifa za kitaifa na kimataifa sehemu mbalimbali nchini.

Viwanja vinahitaji na zaidi ni katika maendeleo ya mchezo katika eneo husika.

-->