Tanzania inahitaji kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kimataifa

Muktasari:

  • Mwelekeo na kiwango cha biashara ya nje pia kina uhusiano na nakisi ya bajeti ya Serikali mwenendo wa deni la taifa. Biashara ya nje pia, ni kielelezo cha uzalishaji wa viwanda vilivyopo nchini.
  • Mwenendo na mwelekeo wa biashara ya nje pia, ni kipimo cha umakini na usahihi wa mikakati ya biashara za kimataifa. Takwimu za mwaka 2007 hadi 2013 kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa (NBS), zinaonyesha kulikuwa na nakisi katika urari wa biashara ya nje ya wastani wa Sh7.8 trilioni.

Ni muhimu kufuatilia mwenendo wa biashara baina ya Tanzania na nchi nyinginezo duniani, kwasababu matokeo yake yana athari katika thamani ya shilingi, mfumuko wa bei na viwango vya riba katika soko la fedha nchini.

Mwelekeo na kiwango cha biashara ya nje pia kina uhusiano na nakisi ya bajeti ya Serikali mwenendo wa deni la taifa. Biashara ya nje pia, ni kielelezo cha uzalishaji wa viwanda vilivyopo nchini.

Mwenendo na mwelekeo wa biashara ya nje pia, ni kipimo cha umakini na usahihi wa mikakati ya biashara za kimataifa. Takwimu za mwaka 2007 hadi 2013 kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa (NBS), zinaonyesha kulikuwa na nakisi katika urari wa biashara ya nje ya wastani wa Sh7.8 trilioni.

Katika kipindi hicho, Tanzania iliuza nje bidhaa zenye thamani ya shilingi Sh38.1 trilioni 38.1 na kununua bidhaa za Sh92.7 trilioni 92.7. Ukijumuisha na bidhaa zilizoingizwa na kuuzwa nje ya nchi (re-exports), nakisi ya urari wa biashara ilikuwa wastani wa Sh7.8 trilioni.

Nakisi ya juu zaidi katika kipindi hicho ilikuwa mwaka 2013, Sh11.7 trilioni na ya chini zaidi ilikuwa mwaka 2009, Sh4.6 trilioni. Takwimu hizo pia zinaangalia nchi 20 zilizofanya biashara zaidi na Tanzania katika kipindi hicho ambazo zilinunua karibu asilimia 88 ya bidhaa zote zilizouzwa nje.

Kati ya nchi hizo 20, za Afrika ni Afrika Kusini, Jamuhuri Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Kenya, Zambia, Rwanda, Msumbiji, Congo na Uganda. Nje ni India, Switzerland, China, Japan, Ujerumani, Ubelgiji, Falme za Kiarabu (UAE), Uholanzi, Marekani, Italia, Singapore na Uingereza.

Katika kipindi hicho, Tanzania iliuza asilimia 30 ya bidhaa zake kwa nchi za Afrika na asilimia 70 katika nchi nyinginezo ulimwenguni. Afrika Kusini ilinunua asilimia 48.4 ya bidhaa zote zilizouzwa ndani ya bara hili na asilimia 14.3 ya bidhaa zote zilizouzwa katika soko la kimataifa.

Kenya ilinunua asilimia 19.4 ya bidhaa zote zilizouzwa Afrika au asilimia 5.7 ya bidhaa zote. DRC ilinunua asilimia 12.4 ya bidhaa zote Afrika au asilimia 3.7 ya bidhaa zote zilizouzwa nje.

Zambia ilinunua asilimia 4.8 ya bidhaa zote zilizouzwa Afrika na asilimia 1.4 ya bidhaa zote wakati Rwanda ilinunua asilimia 4.4 kwa Afrika au asilimia 1.3 kimataifa.

Uganda ilinunua asilimia 4.4 ya bidhaa zilizouzwa kwa nchi za Afrika huku Msumbiji ikifanya hivyo kwa asilimia 3.6 na Congo ikinunua asilimia 2.7 ya bidhaa zote zilizouzwa katika soko la Afrika.

Kwa upande mwingine, Tanzania ilinunua bidhaa kutoka nchi mbili tu za Afrika zilizokuwamo katika orodha ya nchi 20 ilizofanya nazo biashara zaidi ambazo zilitoa mchango wa asilimia 13 ya katika kipindi chote.

Asilimia 68.4 ya bidhaa zote kutoka katika soko la Afrika zilinunuliwa Afrika Kusini. Hizo ni sawa na asilimia 8.5 ya bidhaa zote kutoka nje kuanzia mwaka 2007 mpaka 2013. Asilimia 31.6 ya bidhaa zilizonunuliwa kutoka Afrika, zilikuwa za Kenya, sawa na asilimia 3.9 ya bidhaa zote ambazo Tanzania iliagiza kutoka nje.

Ndani ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC), Tanzania iliuza asilimia 9.3 tu ya bidhaa zote na ilinunua bidhaa asilimia 4.4. Kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) iliuza asilimia 21.5 na ilinunua asilimia 8.5.

Katika soko la SADC, Tanzania iliuza bidhaa zake Afrika Kusini kwa asilimia 78.5 na DRC kwa asilimia 21.5. Namba hizi ni muhimu kwa minajiri ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara baina ya Tanzania na nchi za nje.

Zinatoa uelekeo wa nani wa kushirikiana naye zaidi na nani wa kumuongeza kutokana na fursa zilizopo. Wakati tukijipanga kujenga uchumi wa viwanda, masoko ya bidhaa zetu ni jambo la kipaumbele.

Kuweka mikakati ya kufanikisha hilo ni lazima tuanze kujitathmini kuanzia tulipo ili kuondoa uwezekano wowote wa kukosea na kuchagua sehemu isiyo na mashiko.

Watunga sera hasa za nje na ushirikiano wa kimataifa wanapaswa kulitambua hili. Wafanyabiashara na wajasiriamali wazawa wanatakiwa kuziona fursa za kujitanua nje ya Tanzania na kukuza mitaji na kipato chao. Hilo linawezekana kama tunavyowakaribisha wawekezaji kutoka nje.

Kwa kuangalia mwenendo ulivyo, ni dhahiri bado kuna fursa nyingi za kukuza uchumi kwa kufanya biashara na nchi zinazotuzunguka. Kinachotakiwa ni kuongeza uzalishaji na kufungua mipaka.

Baada ya kukamilisha ukombozi wa bara hili, Tanzania inatakiwa iimarishe uhusiano wa kiuchumi sasa.

Mwandishi anapatikana kwa 0683 555 124.