Tanzania katikati ya mgogoro wa Mashariki ya Kati

Muktasari:

  • Ni Taifa ambalo halina serikali yake. Sehemu kubwa ya ardhi yake imetwaliwa na Waisraeli. Umoja wa Mataifa (UN) haulitambui Taifa hilo kama nchi licha ya kuunda kamati ya kushughulikia mgogoro huo.

Palestina ni Taifa ambalo limekuwepo kwa muda mrefu lakini haitambuliki kama nchi popote duniani. Jumuiya za kimataifa hazilitambui Taifa hilo ambalo limemezwa na nchi ya Israel na halipo kabisa katika ramani ya uso wa dunia.

Ni Taifa ambalo halina serikali yake. Sehemu kubwa ya ardhi yake imetwaliwa na Waisraeli. Umoja wa Mataifa (UN) haulitambui Taifa hilo kama nchi licha ya kuunda kamati ya kushughulikia mgogoro huo.

Mgogoro wa kihistoria kati ya Israel na Palestina unatokana na ardhi. Sehemu kubwa ya ardhi ya Israel ilikuwa mali ya Wapalestina lakini kwa sababu ya wingi wa Waisrael, walijitanua na kuingia mpaka kwenye ardhi ya Wapalestina.

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kimataifa na Kikanda, Dk Augustine Mahiga anasimulia kwamba mwaka 1947, liliundwa Taifa la Israel na Palestina na Umoja wa Mataifa (UN) ilitambua uwepo wa mataifa hayo mawili tofauti.

Hata hivyo, Waisrael wengi walikuwa wakiishi nje ya nchi yao, hivyo Serikali ya wakati huo ilitoa wito kwa Waisrael wote waliosambaa duniani kurudi nyumbani. Wengi walirudi na kununua maeneo ya Wapalestina na kujikuta wanamiliki sehemu kubwa ya ardhi. Baada ya Wapalestina kubaini kwamba eneo kubwa la ardhi yao inakaliwa na Waisrael, walianza kudai ardhi yao, jambo lililosababisha mapigano ya mara kwa mara kati ya majirani hao.

Dk Mahiga anasema mwaka 1961 baada ya uhuru, Mwalimu Nyerere alitangaza kuitambua Israel, lakini pia alisema Tanzania inatambua haki za msingi za Wapalestina ambao walikuwa wakipigania uhuru wao kama baadhi ya nchi nyingine za kiafrika.

Katika ushirikiano huo, Dk Mahiga anasema Tanzania zilishirikiana katika mambo mbalimbali licha ya kwamba hakuna nchi iliyofungua ubalozi wake kwenye nchi nyingine.

Mwaka 1993, Dk Mahiga anasema Tanzania ilirudisha uhusiano wake na Israel baada ya Norway kujitahidi kutafuta suluhu na kurudisha uhusiano wa Taifa hilo na Jumuiya ya Kimataifa.

Hata hivyo, anasema katika uhusiano huo hawakuanzisha balozi bali Tanzania iliamua kutumia ubalozi wake wa Cairo, Misri kulingana na masilahi yake nchini Israel wakati Israel nayo ikitumia ubalozi wa Nairobi, Kenya kuangalia masilahi yake hapa nchini.

Licha ya kuanzisha uhusiano mpya na Israel, Tanzania bado inatambua haki za msingi za Taifa la Palestina ambalo halitambuliki kama nchi huru inayojitawala yenyewe.

Dk Augustine Mahiga ameieleza kamati ya Umoja wa Mataifa inayotetea haki za msingi za Wapalestina kwamba bado wanaamini Palestina inatakiwa kuwa huru katika kuamua mambo yake.

Akizungumzia uhusiano wa Tanzania na mataifa hayo, Dk Mahiga anasema msimamo wa Tanzania baada ya uhuru ulikuwa ni kuitetea Palestina ili iwe huru na kutambulika kama nchi nyingine duniani.

Kutokana na vita vilivyoanzishwa na Israel dhidi ya mataifa ya Uarabuni na kutwaa sehemu ya ardhi zao, Dk Mahiga anasema Tanzania haikuridhia jambo hilo na kuamua kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Israel mwaka 1967.

Anasisitiza kwamba licha ya kurudisha uhusiano wake na Israel, bado uhusiano wa miaka mingi wa Tanzania na Palestina uko palepale na inaunga mkono juhudi za kamati hiyo iliyoundwa mwaka 1975 na Umoja wa Mataifa kutafuta suluhu ya mgogoro huo.

Balozi wa kudumu wa Palestina - Umoja wa Mataifa (UN), Dk Riyad Mansour anaamini kwamba kamati hiyo itafanikiwa kuifanya Palestina itambulike duniani kote na kuwa na hadhi yake kama nchi huru.

Anasema wanazunguka sehemu mbalimbali duniani ili kuwafanya vijana waufahamu mgogoro huo na anaamini kwamba vijana wakizungumza na vijana wenzao Palestina wataamini na kufahamu mgogoro huo.

Ubalozi wa Tanzania kubaki Tel Aviv

Siku chache baada ya Marekani kuutambua mji wa Yerusalem kama Mji Mkuu wa Israel, ubalozi wa Tanzania utaendelea kuwa Tel Aviv kama ilivyo kwa UN na nchi mbalimbali duniani zenye uhusiano wa kidiplomasia na nchi hiyo.

Dk Mahiga amekanusha taarifa kwamba ubalozi wa Tanzania utahamia Jerusalem baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kutangaza kuutambua mji huo kama mji mkuu wa Israel na kuamua ubalozi wake uhamie huko.

Hata hivyo, waziri huyo amesisitiza kwamba msimamo wa Tanzania ni wa kutofungamana na upande wowote, itaendelea kushirikiana na Israel hasa katika diplomasia ya kiuchumi lakini pia itaendelea kutambua haki za msingi za Wapalestina ili nao wawe nchi huru.