Tanzania ya uchumi wa kati inahitaji haki kwa wakati

Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi alipozindua maadhimisho ya wiki ya Sheria na Utoaji Elimu ya Sheria alitoa rai kuwa mahakama zinapaswa ziwe huru bila kuingiliwa na chombo chochote na pia zitoe haki kwa wakati ili kuzifanya ziaminiwe na wananchi.

Muktasari:

Huo ni ukumbusho muhimu sana kwa mhimili huo muhimu katika mihimili mitatu ya kuendesha nchi ambayo ni serikali, bunge na mahakama.

Ni wazi kuwa amani na utulivu wa nchi unachangiwa na utoaji haki, nchi ambayo haina utoaji haki kwa kawaida huwa haina amani na utulivu kwa sababu wananchi wamekosa matumaini kwa kuwa haki zao hazina msimamizi au msimamizi aliyepo ameamua kuzivurunda.

Sehemu ambayo haina amani na utulivu bila shaka hata maendeleo yake yanadumaa, hivyo Tanzania inayojipanga kuingia katika uchumi wa kati inahitaji sana amani na utulivu na kufuata misingi ya utoaji wa haki.

Ndiyo maana kauli mbiu ya maadhimisho ya wiki ya sheria ya mwaka huu ni “Umuhimu wa utoaji haki kwa wakati, kuwezesha ukuaji wa uchumi.”

Uhuru wa Mahakama unamaanisha kuwa kila jaji au hakimu yuko huru kuamua kesi iliyopo mbele yake kwa mujibu wa sheria na ushahidi ulioletwa mbele yake, na katika kutekeleza majukumu hayo, hapaswi kuingiliwa, kushawishiwa au kushinikizwa na mtu au chombo chochote, ikiwamo bunge na serikali kama inavyoelezwa katika Ibara ya 107B ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977: “Katika kutekeleza mamlaka ya utoaji haki, mahakama zote zitakuwa huru na zitalazimika kuzingatia tu masharti ya Katiba na yale ya sheria za nchi.”

Hivyo dhana ya uhuru wa mahakama inaitaka mahakama kutekeleza majukumu yake bila woga wala upendeleo.

Rais Mstaafu Mwinyi ametoa angalizo kwamba mahakama zinapaswa zitende haki kwa wakati na zisiruhusu kuingiliwa katika hali yoyote ile.

Kimsingi haijaripotiwa kesi kuhusu mtu au serikali kuiingilia mahakama lakini watendaji wa mahakama kwa woga wao tu wanaweza kujikuta wakiacha sheria pembeni na kutumia ‘busara’ kufurahisha upande fulani.

Hivyo watumishi wa mahakama wanapaswa kuutumia uhuru wa mahakama kwa maslahi ya umma na wala wasiutumie uhuru huo kwa kufunika maovu.

Katika usimamizi wa sheria inapaswa haki itendeke na ionekane kuwa imetendeka, endapo wadau wataweka walakini katika utekelezaji wa haki, hiyo si ishara nzuri katika usimamizi wa mhimili huu muhimu katika jamii.

Msingi wa pili wa mahakama ni kutoa haki kwa wakati kwani haki inayocheleweshwa ni haki iliyokataliwa, angalau mahakama zetu zimeweka utaratibu mzuri wa kusikiliza kesi na kuhakikisha kuwa zinatolewa uamuzi mapema.

Mtu anapocheleweshewa shauri lake anacheleweshewa pia shughuli zake nyingine za maendeleo, hivyo msisitizo wa kauli mbiu ya mwaka huu ni umuhimu wa kutoa haki kwa wakati ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi.

Tunashauri kuwa kauli hiyo isiishie katika kauli mbiu pekee, bali ifanyiwe kazi ipasavyo kwa sababu mtindo wa kuahirisha kesi bila sababu zinazoonekana kuwa na mashiko, unaendelea katika mahakama zetu, hivyo kutoa taswira ya kuwa haki inawezekana kupatikana, lakini haionekani kama inatendeka.

toa haki kwa wakati ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi.