Tanzania ya viwanda inahitaji maji

Muktasari:

  • Siku hiyo imeadhimishwa huku taarifa mbalimabi za kitafiti zikionyesha kuwa bado maeneo mengi nchini yanakabiliwa na uhaba wa huduma hiyo, idadi kubwa ya wananchi wanalazimika kutembea umbali mrefu kusaka maji.

Jana Tanzania iliungana na nchi mbalimbali duniani kuadhimisha siku ya maji.

Siku hiyo imeadhimishwa huku taarifa mbalimabi za kitafiti zikionyesha kuwa bado maeneo mengi nchini yanakabiliwa na uhaba wa huduma hiyo, idadi kubwa ya wananchi wanalazimika kutembea umbali mrefu kusaka maji.

Inasikitisha kuwa haya yote yanatokea katika nchi ambayo tafiti zinaonyesha kwamba ina kiwango kikubwa cha maji yaliyopo ardhini na hata juu ya ardhi.

Tunaweza kutoa sababu nyingi za kushindwa kutumia vyema rasilimali hii muhimu kwa maendeleo ya nchi ikiwamo ufinyu wa teknolojia, lakini kubwa kwa upande wetu ni kutojipanga kama Taifa. Tukitambua kuwa hakuna shughuli ya kibinadamu inayoweza kufanyika pasipo kuwa na maji, na kwamba mustakabali wa nchi yetu unategemea kwa kiwango kikubwa, uimara wa rasilimali hii bado haijawa kipaumbele chetu.

Ni kwa sababu hiyo, leo kila kona ya nchi kilio kikubwa cha wananchi ni pamoja na uhaba wa maji kama zisemavyo ripoti kuwa idadi ya wananchi wanaopata maji imeongezeka kutoka milioni 15.2 hadi milioni 21.9, sawa na asilimia 72 ya Watanzania. Lakini, takwimu hizo hazimaanishi kuwa lengo la kuwafikishia maji wananchi wengi limefanikiwa kwa kuwa idadi kubwa ya wanaopata huduma hiyo wapo mijini, ilhali zaidi ya asilimia 70 wanaishi vijijini ambako kuna uhaba mkubwa wa huduma hiyo.

Tanzania si tu kwamba ina tatizo la maji ya uhakika, safi na salama, lakini pia hata pale yanapopatikana tunakosa mifumo bora ya usimamizi wa rasilimali hiyo muhimu kwa taifa.

Kimsingi, shughuli zinazohusu matumizi ya maji majumbani, kwenye kilimo, viwanda, uchimbaji wa madini na uzalishaji umeme unategemea usimamizi mzuri. Taasisi za usimamizi wa maji nchini haziwajibiki ipasavyo katika mgawanyo wa maji, kudhibiti uharibifu wa vyanzo vyake ikiwamo kupungua na kuisha.

Matokeo yake kila mahali wananchi wanalia maji. Mpango wa kuhakikisha maji yanapatikana ndani ya mita 100 unaonekena kugonga mwamba katika maeneo mengi nchini.

Usimamizi mbovu wa maji umesababisha kupungua kwa maji na kuzuka kwa migogoro ambayo dhahiri inakwamisha vita dhidi ya umasikini na kuwa kikwazo dhidi ya uwekezaji. Ndio maana haishangazi kuwa hata juzi wakati wa mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara, wawekezaji walilalamikia mambo mengi ikiwamo ukosefu wa maji.

Tunaamini tatizo letu sio kukosekana kwa maji, bali mgawanyo, udhibiti na usimaizi wa rasilimali hiyo.

Ukweli ni kuwa katika mpango wa kwanza wa Maendeleo ya Sekta ya Maji, Serikali yetu haikuonyesha nia ya dhati katika usimamizi wa maji, kwani mpango wa usimamizi wa maji ulipata asilimia tano tu ya bajeti yake.

Maji ni mhimili muhimu wa Taifa letu. Tusipojirekebisha na kuchukua hatua tutajiangamiza sisi wenyewe. Kila mmoja wetu ajitoe kusimamia uhai wa taifa letu kwa kuhakikisha maji yanapatikana.

Tukiwa na maji ya uhakika katika kila kona ya nchi, dira, ndoto na matarajio ya Tanzania ya viwanda na ya uchumi wa kati havitokuwa na sababu ya kutofikiwa. Tuitengeneze Tanzania ya sifa hizi kwa kuanzia kwenye upatikanaji wa maji, kwa kuwa ndio damu ya Taifa.